5
1 Kristo alitupa uhuru akataka tubaki huru. Basi, simameni imara wala msikubali tena kuwa chini ya nira ya utumwa.
2 Sikilizeni! Ni mimi Paulo ninayesema nanyi! Kama mkikubali kutahiriwa, Kristo hatawafaidia chochote.
3 Nasema tena wazi: kila anayekubali kutahiriwa itambidi kuishika Sheria yote.
4 Kama mnatazamia kukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Sheria, basi, mmejitenga mbali na Kristo; mko nje ya neema ya Mungu.
5 Kwa upande wetu, lakini, sisi tunatumaini kwamba kwa nguvu ya Roho tunakubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya imani.
6 Maana ikiwa tumeungana na Kristo Yesu, kutahiriwa au kutotahiriwa hakuna maana; cha maana ni imani ifanyayo kazi kwa mapendo.
7 Mwenendo wenu ulikuwa mzuri! Nani, basi aliyewazuia kuuzingatia ukweli?
8 Aliyesababisha hali hiyo si Mungu ambaye amewaiteni.
9 “chachu kidogo tu huchachusha donge lote la unga!”
10 Kutokana na kuungana kwetu na Bwana, nina tumaini kubwa kwamba ninyi hamtakuwa na msimamo tofauti nami. Tena yeyote huyo anayewavurugeni—awe nani au nani—hakika ataadhibiwa.
11 Na kwa upande wangu, ndugu zangu, kama bado ninahubiri kwamba kutahiriwa ni lazima, kwa nini basi, bado ninadhulumiwa? Kama ingalikuwa hivyo, mahubiri yangu juu ya msalaba wa Kristo yasingalileta aibu yoyote.
12 Laiti hao wanaowavurugeni wangejikatakata wenyewe!
13 Ninyi, ndugu, mliitwa muwe watu huru. Lakini uhuru huo usiwe kisingizio cha kutawaliwa na tamaa za kidunia; ila mnapaswa kutumikiana kwa upendo.
14 Maana Sheria yote hutimizwa katika kushika amri hii moja: “Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.”
15 Lakini ikiwa mtaumana na kutafunana kama wanyama, jihadharini msije mkaangamizana wenyewe kwa wenyewe!
16 Basi, nasema hivi: mwenendo wenu na uongozwe na Roho, nanyi hamtafuata tena tamaa za kidunia.
17 Maana, tamaa za kidunia hupingana na matakwa ya Roho; na matakwa ya Roho hupingana na tamaa za kidunia. Mambo hayo mawili hayaafikiani; kwa sababu hiyo hamwezi kufanya yale mnayotaka ninyi wenyewe.
18 Kama mkiongozwa na Roho, basi, hamko tena chini ya Sheria.
19 Basi, matendo ya kidunia yanajulikana: uzinzi, uasherati, ufisadi;
20 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, choyo, mabishano, mafarakano;
21 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine kama hayo. Nawaambieni tena kama nilivyokwisha sema: watu wanaotenda mambo hayo hawatakuwa na nafasi yao katika ufalme wa Mungu.
22 Lakini matokeo ya kuongozwa na Roho ni mapendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu,
23 upole na kuwa na kiasi. Hakuna Sheria inayoweza kupinga mambo hayo.
24 Wale walio wa Kristo wameisulubisha hali yao ya kidunia pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.
25 Tukiishi kwa msaada wa Roho, na tuufuate mwongozo wake.
26 Basi, tusijivune, tusichokozane wala kuoneana wivu.