10
1 Yesu alitoka hapo akaenda mkoani Yudea na hata ng'ambo ya mto Yordani. Umati wa watu ukamwendea tena, naye akawafundisha tena kama ilivyokuwa desturi yake.
2 Basi, Mafarisayo wakamwendea, na kwa kumjaribu wakamwuliza, “Je, ni halali mtu kumpa talaka mkewe?”
3 Yesu akawajibu, “Mose aliwapa maagizo gani?”
4 Nao wakasema, “Mose aliagiza mume kumpatia mkewe hati ya talaka na kumwacha.”
5 Yesu akawaambia, “Mose aliwaandikia amri hiyo kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu.
6 Lakini tangu kuumbwa ulimwengu, Mungu aliumba mwanamume na mwanamke.
7 Hivyo mwanamume atawaacha baba yake na mama yake, ataungana na mkewe,
8 nao wawili watakuwa mwili mmoja. Kwa hiyo, wao si wawili tena bali mwili mmoja.
9 Basi, alichounganisha Mungu, binadamu asitenganishe.”
10 Walipoingia tena ndani ya nyumba, wanafunzi wake walimwuliza juu ya jambo hilo.
11 Naye akawaambia, “Anayemwacha mkewe na kuoa mwingine, anazini dhidi ya mkewe.
12 Na mwanamke anayemwacha mumewe na kuolewa na mwingine anazini.”
13 Watu walimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse, lakini wanafunzi wakawakemea.
14 Yesu alipoona hivyo, alikasirika akawaambia, “Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu walio kama watoto hawa.
15 Nawaambieni kweli, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hataingia katika Ufalme huo.”
16 Kisha akawapokea watoto hao, akawawekea mikono, akawabariki.
17 Yesu alipoanza tena safari yake, mtu mmoja alimjia mbio, akapiga magoti mbele yake, akamwuliza, “Mwalimu mwema, nifanyeje ili niupate uzima wa milele?”
18 Yesu akamjibu, “Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila Mungu peke yake.
19 Unazijua amri: Usizini; Usiue; Usiibe; Usitoe ushahidi wa uongo; Usidanganye; Waheshimu baba na mama yako.”
20 Naye akamjibu, “Mwalimu, hayo yote nimeyazingatia tangu ujana wangu.”
21 Yesu akamtazama, akampenda, akamwambia, “Umepungukiwa na kitu kimoja: nenda ukauze vitu ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.”
22 Aliposikia hayo, alisikitika, akaenda zake akiwa na huzuni, kwa maana alikuwa na mali nyingi.
23 Yesu akatazama pande zote, akawaambia wanafunzi wake, “Jinsi gani itakavyokuwa vigumu kwa matajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu!”
24 Wanafunzi walishangazwa na maneno yake. Yesu akawaambia tena, “Watoto wangu, ni vigumu sana kuingia katika Ufalme wa Mungu!
25 Ni rahisi zaidi ngamia kupenya katika tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.”
26 Wanafunzi wake wakashangaa sana wakaulizana, “Ni nani basi, atakayeweza kuokoka?”
27 Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa binadamu haiwezekani, lakini kwa Mungu si hivyo, maana kwa Mungu mambo yote huwezekana.”
28 Petro akamwambia, “Na sisi je? Tumeacha yote, tukakufuata!”
29 Yesu akasema, “Kweli nawaambieni, kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu, au dada, au mama, au baba, au watoto au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya Habari Njema,
30 atapokea mara mia zaidi wakati huu wa sasa nyumba, ndugu, dada, mama, watoto na mashamba pamoja na mateso; na katika wakati ujao atapokea uzima wa milele.
31 Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.”
32 Basi, walikuwa njiani kwenda Yerusalemu, na Yesu alikuwa anawatangulia. Wanafunzi wake walijawa na hofu, na watu waliofuata waliogopa. Yesu akawachukua tena kando wale kumi na wawili, akaanza kuwaambia yale yatakayompata:
33 “Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu, na huko Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa makuhani wakuu na walimu wa Sheria, nao watamhukumu auawe na kumkabidhi kwa watu wa mataifa.
34 Nao watamdhihaki; watamtemea mate, watampiga mijeledi na kumwua. Na baada ya siku tatu atafufuka.”
35 Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, walimwendea Yesu wakamwambia, “Mwalimu, tunataka utufanyie kitu tutakachokuomba.”
36 Yesu akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”
37 Wakamjibu, “Uturuhusu tuketi mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande wako wa kushoto katika utukufu wa Ufalme wako.”
38 Yesu akawaambia, “Hamjui mnachoomba! Je, mnaweza kunywa kikombe nitakachokunywa, au kubatizwa kama nitakavyobatizwa?”
39 Wakamjibu, “Tunaweza.” Yesu akawaambia, “Kikombe nitakachokunywa mtakinywa kweli, na mtabatizwa kama nitakavyobatizwa.
40 Lakini ni nani atakayeketi kulia au kushoto kwangu si wajibu wangu kupanga, bali nafasi hizo watapewa wale waliotayarishiwa.”
41 Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, walianza kuchukizwa na Yakobo na Yohane.
42 Yesu akawaita, akawaambia, “Mnajua kwamba wale wanaofikiriwa kuwa watawala wa mataifa huwatawala watu wao kwa mabavu, na wakuu hao huwamiliki watu wao.
43 Lakini kwenu isiwe hivyo, ila anayetaka kuwa mkuu kati yenu, sharti awe mtumishi wenu.
44 Anayetaka kuwa wa kwanza, sharti awe mtumishi wa wote.
45 Maana Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, ila alikuja kutumikia, na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi.”
46 Basi, wakafika Yeriko, naye Yesu alipokuwa anatoka katika mji huo akiwa na wanafunzi wake pamoja na umati mkubwa wa watu, kipofu mwombaji aitwaye Bartimayo mwana wa Timayo alikuwa ameketi kando ya barabara.
47 Aliposikia kwamba ni Yesu wa Nazareti aliyekuwa anapita mahali hapo, alianza kupaaza sauti, “Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!”
48 Watu wengi walimkemea ili anyamaze, lakini yeye akazidi kupaaza sauti, “Mwana wa Daudi, nihurumie!”
49 Yesu alisimama, akasema, “Mwiteni.” Basi, wakamwita huyo kipofu, wakamwambia, “Jipe moyo! Simama, anakuita.”
50 Naye akatupilia mbali vazi lake, akaruka juu, akamwendea Yesu.
51 Yesu akamwuliza, “Unataka nikufanyie nini?” Huyo kipofu akamwambia, “Mwalimu, naomba nipate kuona.”
52 Yesu akamwambia, “Nenda, imani yako imekuponya.” Mara huyo kipofu akaweza kuona, akamfuata Yesu njiani.