Amosi
1
1 Maneno ya Amosi, mmoja wa wachunga wanyama wa Tekoa: yale aliyoyaona kuhusu Israeli miaka miwili kabla ya tetemeko la ardhi, wakati Uzia alikuwa mfalme wa Yuda, na Yeroboamu mwana wa Yehoashi alikuwa mfalme wa Israeli.
2 Alisema:
“Bwana ananguruma toka Sayuni,
pia ananguruma kutoka Yerusalemu;
malisho ya wachunga wanyama yanakauka,
kilele cha Karmeli kinanyauka.”
Hukumu Juu Ya Majirani Wa Israeli
3 Hili ndilo asemalo Bwana:
“Kwa dhambi tatu za Dameski,
hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu.
Kwa sababu aliipura Gileadi
kwa vyombo vya chuma vyenye meno.
4 Nitatuma moto juu ya nyumba ya Hazaeli
ambao utateketeza ngome za Ben-Hadadi.
5 Nitalivunja lango la Dameski;
nitamwangamiza mfalme aliyeko katika Bonde la Aveni,
na yeye ambaye anaishika fimbo ya utawala katika Beth-Edeni.
Watu wote wa Aramu watakwenda uhamishoni huko Kiri,”
asema Bwana.
6 Hili ndilo asemalo Bwana:
“Kwa dhambi tatu za Gaza,
hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu.
Kwa sababu walichukua mateka jumuiya nzima
na kuwauza kwa Edomu,
7 nitatuma moto juu ya kuta za Gaza
ambao utateketeza ngome zake.
8 Nitamwangamiza mfalme wa Ashdodi
na yeye aishikaye fimbo ya utawala katika Ashkeloni.
Nitaugeuza mkono wangu dhidi ya Ekroni,
hadi Mfilisti wa mwisho atakapokufa,”
asema Bwana Mwenyezi.
9 Hili ndilo asemalo Bwana:
“Kwa dhambi tatu za Tiro,
hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu.
Kwa sababu ameuza jumuiya nzima ya mateka kwa Edomu,
na kutokujali mapatano ya undugu,
10 Nitatuma moto kwenye kuta za Tiro
ambao utateketeza ngome zake.”
11 Hili ndilo Bwana asemalo:
“Kwa dhambi tatu za Edomu,
hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu.
Kwa sababu alimfuatia ndugu yake kwa upanga,
alikataa kuonyesha huruma yoyote,
kwa sababu hasira yake kali iliendelea kupanda wakati wote
na ghadhabu iliwaka bila kuzuiliwa.
12 Nitatuma moto juu ya Temani
ambao utateketeza ngome za Bosra.”
13 Hili ndilo asemalo Bwana:
“Kwa dhambi tatu za Amoni,
hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu.
Kwa sababu aliwatumbua wanawake wajawazito wa Gileadi
ili kuongeza mipaka yake.
14 Nitatuma moto kwenye kuta za Raba
ambao utateketeza ngome zake
katikati ya vilio vya vita katika siku ya mapigano,
katikati ya upepo mkali katika siku ya dhoruba.
15 Mfalme wake atakwenda uhamishoni,
yeye pamoja na maafisa wake,”
asema Bwana.