10
Vibao Vingine Vya Amri Kumi
(Kutoka 34:1-10)
1 Wakati ule Bwana aliniambia, “Chonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza uje kwangu juu mlimani. Pia utengeneze Sanduku la mbao.
2 Nitaandika juu ya vibao maneno yaliyokuwa katika vile vibao vya kwanza, ambavyo ulivivunja. Kisha utaviweka ndani ya Sanduku.”
3 Hivyo nikatengeneza Sanduku kwa mti wa mshita, nikachonga pia vibao vya mawe kama vile vya kwanza, kisha nikakwea mlimani nikiwa na vibao viwili mikononi mwangu.
4 Bwana akaandika juu ya hivi vibao kile alichokuwa amekiandika kabla, Amri Kumi alizokuwa amewatangazia juu mlimani, kutoka kwenye moto siku ile ya kusanyiko. Bwana akanikabidhi.
5 Kisha nikashuka kutoka mlimani na kuweka vibao ndani ya Sanduku nililokuwa nimelitengeneza, kama Bwana alivyoniagiza, navyo viko huko sasa.
6 (Waisraeli walisafiri kutoka visima vya Yaakani hadi Mosera. Huko Aroni alifariki na kuzikwa, naye Eleazari mwanawe akachukua nafasi yake kama kuhani.
7 Kutoka pale, walisafiri hadi Gudgoda wakaendelea mpaka Yotbatha, nchi yenye vijito vya maji.
8 Wakati huo Bwana aliteua kabila la Lawi kulibeba Sanduku la Agano la Bwana, kusimama mbele za Bwana ili kutoa huduma, na kutangaza baraka kwa Jina lake, kama wanavyofanya mpaka leo.
9 Hiyo ndiyo sababu ya Walawi kutokuwa na sehemu wala urithi miongoni mwa ndugu zao; Bwana ndiye urithi wao, kama Bwana Mungu wao alivyowaambia.)
10 Basi nilikaa mlimani kwa siku arobaini usiku na mchana, kama nilivyofanya mara ya kwanza, pia Bwana alinisikiliza hata wakati huu. Haikuwa nia yake kuwaangamiza.
11 Bwana akaniambia, “Nenda, ukawaongoze watu katika njia yao ili kwamba waweze kuingia na kuimiliki nchi ile niliyowaapia baba zao kuwapa.”
Mche Bwana
12 Na sasa, ee Israeli, Bwana Mungu wako anataka nini kwako ila kumcha Bwana Mungu wako, kwenda katika njia zake, kumpenda na kumtumikia Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote,
13 na kuyashika maagizo ya Bwana na amri zake ninazokupa leo kwa mafanikio yako mwenyewe?
14 Mbingu, hata mbingu za juu sana, dunia na kila kitu kilichomo ndani yake, ni mali ya Bwana Mungu wako.
15 Hata hivyo Bwana alikuwa na shauku na baba zako, akawapenda na akawachagua ninyi, wazao wao, kuliko mataifa yote, kama ilivyo leo.
16 Kwa hiyo tahirini mioyo yenu, na msiwe na shingo ngumu tena.
17 Kwa kuwa Bwana Mungu wenu ni Mungu wa miungu na Bwana wa mabwana, Mungu mkuu, mwenye uweza na wa kutisha, ambaye hana upendeleo na hapokei rushwa.
18 Huwapigania yatima na wajane, humpenda mgeni, akimpa chakula na mavazi.
19 Nanyi wapendeni wageni, kwa kuwa ninyi wenyewe mlikuwa wageni huko Misri.
20 Mche Bwana Mungu wako na umtumikie yeye. Shikamana naye kwa uthabiti na kuapa kwa jina lake.
21 Yeye ni sifa yako; yeye ni Mungu wako, ambaye alikutendea yale maajabu makubwa na ya kutisha uliyoyaona kwa macho yako mwenyewe.
22 Baba zako walioshuka kwenda Misri jumla yao walikuwa sabini, na sasa Bwana Mungu wako amekufanya wengi kama nyota za angani.