27
Madhabahu Katika Mlima Ebali
1 Mose na wazee wa Israeli wakawaagiza watu: “Yashikeni maagizo haya yote ninayowaagiza leo.
2 Mtakapokuwa mmevuka Mto Yordani na kuingia katika nchi awapayo Bwana Mungu wenu, msimamishe mawe makubwa na mkayatie lipu.
3 Andikeni juu yake maneno yote ya sheria hii wakati mtakapokuwa mmevuka na kuingia katika nchi awapayo Bwana Mungu wenu, nchi itiririkayo maziwa na asali, kama vile Bwana, Mungu wa baba zenu, alivyowaahidi.
4 Mtakapokuwa mmevuka Yordani, simamisheni mawe haya juu ya Mlima Ebali, kama ninavyowaagiza leo, mkayatie lipu.
5 Huko mjengeeni Bwana Mungu wenu madhabahu, madhabahu ya mawe. Msitumie kifaa chochote cha chuma juu yake.
6 Jengeni madhabahu ya Bwana Mungu wenu kwa mawe ya shambani, na mtoe sadaka za kuteketezwa juu yake kwa Bwana Mungu wenu.
7 Toeni sadaka za amani juu yake, mkizila na kufurahia mbele za Bwana Mungu wenu.
8 Nanyi mtaandika maneno yote ya sheria hii kwa wazi sana juu ya mawe haya ambayo mmesimamisha.”
Laana Kutoka Mlima Ebali
9 Kisha Mose na makuhani, ambao ni Walawi, wakawaambia Israeli wote, “Nyamaza ee Israeli, sikiliza! Sasa umekuwa taifa la Bwana Mungu wako.
10 Mtii Bwana Mungu wako, na kufuata amri zake na maagizo ninayokupa leo.”
11 Siku ile ile Mose akawaagiza watu:
12 Mtakapovuka Mto Yordani, makabila haya yatasimama juu ya Mlima Gerizimu kubariki watu: Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari, Yosefu na Benyamini.
13 Makabila haya yatasimama juu ya Mlima Ebali kwa kutamka laana: Reubeni, Gadi, Asheri, Zabuloni, Dani na Naftali.
14 Nao Walawi watawasomea watu wote wa Israeli kwa sauti kubwa:
15 “Alaaniwe mtu afanyaye sanamu ya kuchonga au mwenye kusubu sanamu, kitu ambacho ni chukizo kwa Bwana, kazi ya mikono ya fundi stadi, na kuisimamisha kwa siri.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”
16 “Alaaniwe mtu amdharauye baba yake na mama yake.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”
17 “Alaaniwe mtu asogezaye jiwe la mpaka wa jirani yake.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”
18 “Alaaniwe mtu ampotoshaye kipofu njiani.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”
19 “Alaaniwe mtu apotoshaye haki ya mgeni, yatima au mjane.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”
20 “Alaaniwe mtu akutanaye kimwili na mke wa baba yake, kwa maana anadharau malazi ya baba yake.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”
21 “Alaaniwe mtu akutanaye kimwili na mnyama yeyote.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”
22 “Alaaniwe mtu akutanaye kimwili na dada yake, binti wa baba yake au binti wa mama yake.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”
23 “Alaaniwe mtu akutanaye kimwili na mama mkwe wake.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”
24 “Alaaniwe mtu amuuaye jirani yake kwa siri.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”
25 “Alaaniwe mtu apokeaye rushwa ili kumuua mtu asiye na hatia.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”
26 “Alaaniwe mtu yule ambaye hatashikilia maneno ya sheria hii kwa kuyatekeleza.”
Kisha watu wote watasema, “Amen!”