33
Mose Anayabariki Makabila
Hii ndiyo baraka Mose mtu wa Mungu aliyotamka kwa Waisraeli kabla ya kifo chake. Alisema:
Bwana alikuja kutoka Mlima Sinai,
akachomoza kama jua juu yao
kutoka Mlima Seiri,
akaangaza kutoka Mlima Parani.
Alikuja pamoja na watakatifu makumi elfu
kutoka kusini,
kutoka materemko ya mlima wake.
Hakika ni wewe ambaye huwapenda watu,
watakatifu wako wote wamo mkononi mwako.
Miguuni pako wote wanasujudu
na kutoka kwako wanapokea mafundisho,
sheria ile Mose aliyotupa sisi,
tulio milki ya kusanyiko la Yakobo.
Alikuwa mfalme juu ya Yeshuruni*
wakati viongozi wa watu walipokusanyika,
pamoja na makabila ya Israeli.
 
“Reubeni na aishi, asife,
wala watu wake wasiwe wachache.”
Akasema hili kuhusu Yuda:
“Ee Bwana, sikia kilio cha Yuda,
mlete kwa watu wake.
Kwa mikono yake mwenyewe hujitetea.
Naam, uwe msaada wake
dhidi ya adui zake!”
Kuhusu Lawi alisema:
“Thumimu yako na Urimu yako ulimpa,
mtu yule uliyemfadhili.
Ulimjaribu huko Masa
na kushindana naye
kwenye maji ya Meriba.
Alinena hivi kuhusu baba yake na mama yake,
‘Mimi siwahitaji kamwe.’
Akawasahau jamaa zake,
asiwatambue hata watoto wake,
lakini akaliangalia neno lako
na kulilinda Agano lako.
10 Humfundisha Yakobo mausia yako
na Israeli sheria yako.
Hufukiza uvumba mbele zako
na sadaka nzima za kuteketezwa
juu ya madhabahu yako.
11 Ee Bwana, bariki ustadi wake wote,
nawe upendezwe na kazi ya mikono yake.
Vipige viuno vya wale wainukao dhidi yake;
wapige adui zake hata wasiinuke tena.”
12 Kuhusu Benyamini akasema:
“Mwache mpenzi wa Bwana
apumzike salama kwake,
kwa maana humkinga mchana kutwa,
na yule Bwana ampendaye
hupumzika kati ya mabega yake.”
13 Kuhusu Yosefu akasema:
Bwana na aibariki nchi yake
kwa umande wa thamani
kutoka mbinguni juu,
na vilindi vya maji
vilivyotulia chini;
14 pamoja na vitu vilivyo bora sana
viletwavyo na jua,
na vitu vizuri sana vinavyoweza
kutolewa na mwezi;
15 pamoja na zawadi bora sana
za milima ya zamani
na kwa wingi wa baraka
za vilima vya milele;
16 pamoja na baraka nzuri mno
za ardhi na ukamilifu wake,
na upendeleo wake yeye
aliyeishi kwenye kichaka
kilichokuwa kinawaka moto.
Hivi vyote na vikae juu ya kichwa cha Yosefu,
juu ya paji la uso la aliye mkuu
miongoni mwa ndugu zake.
17 Katika fahari yeye ni kama fahali mzaliwa wa kwanza;
pembe zake ni pembe za nyati,
na kwa pembe hizo atapiga mataifa,
hata yaliyo miisho ya dunia.
Hivyo ndivyo yalivyo makumi elfu ya Efraimu;
hivyo ndivyo yalivyo maelfu ya Manase.”
18 Kuhusu Zabuloni akasema:
“Shangilia, Zabuloni, wakati wa kutoka nje,
nawe Isakari, katika mahema yako.
19 Watawaita mataifa kwenye mlima,
na huko mtatoa dhabihu za haki;
watajifurahisha kwa wingi uliojaza bahari,
kwa hazina zilizofichwa mchangani.”
20 Kuhusu Gadi akasema:
“Atabarikiwa yeye aongezaye milki ya Gadi!
Gadi huishi huko kama simba,
akirarua kwenye mkono au kichwa.
21 Alijichagulia nchi nzuri kuliko zote
kwa ajili yake mwenyewe;
fungu la kiongozi lilikuwa limehifadhiwa
kwa ajili yake.
Viongozi wa watu walipokusanyika,
alitimiza haki ya mapenzi ya Bwana,
na hukumu zake kuhusu Israeli.”
22 Kuhusu Dani akasema:
“Dani ni mwana simba,
akiruka kutoka Bashani.”
23 Kuhusu Naftali akasema:
“Naftali amejaa tele upendeleo wa Bwana,
naye amejaa baraka yake;
atarithi magharibi na kusini.”
24 Kuhusu Asheri akasema:
“Aliyebarikiwa zaidi sana katika wana ni Asheri;
yeye na apate upendeleo kwa ndugu zake,
yeye na anawe miguu yake kwenye mafuta.
25 Makomeo ya malango yako yawe chuma na shaba,
nazo nguvu zako zitakuwa sawa na siku zako.
 
26 “Hakuna mwingine kama Mungu wa Yeshuruni,
ambaye hupanda juu ya mbingu ili akusaidie,
na juu ya mawingu katika utukufu wake.
27 Mungu wa milele ni kimbilio lako,
na chini kuna mikono ya milele.
Atamfukuza adui yako mbele yako,
akisema, ‘Mwangamize yeye!’
28 Hivyo Israeli ataishi salama peke yake.
Mzao wa Yakobo ni salama
katika nchi ya nafaka na divai mpya,
mahali ambapo mbingu
hudondosha umande.
29 Ee Israeli, wewe umebarikiwa!
Ni nani kama wewe,
taifa lililookolewa na Bwana?
Yeye ni ngao yako na msaada wako,
na upanga wako uliotukuka.
Adui zako watatetemeka mbele yako,
nawe utapakanyaga
mahali pao pa juu.”
* 33:5 Yeshuruni maana yake ni Yeye aliye mnyofu, yaani Israeli. 33:8 Thumimu na Urimu maana yake Nuru na Kweli; vifaa hivi viliwekwa kwenye kifuko cha kifuani cha kisibau cha kuhani mkuu ili kujua mapenzi ya Mungu kwenye mambo ya kutatanisha. 33:29 Utapakanyaga mahali pao pa juu maana yake mtakanyaga juu ya miili yao.