6
1 Nimeona ubaya mwingine chini ya jua, nao unalemea sana wanadamu:
2 Mungu humpa mwanadamu utajiri, mali na heshima, hivyo hakukosa chochote moyo wake unachokitamani. Lakini Mungu hamwezeshi kuvifurahia, badala yake mgeni ndiye anayevifurahia. Hili ni ubatili, ni ubaya unaosikitisha.
3 Mtu anaweza kuwa na watoto mia moja naye akaishi miaka mingi, lakini haidhuru kuwa ataishi muda mrefu kiasi gani, kama hawezi kufurahia mafanikio yake na kwamba hapati mazishi ya heshima, ninasema afadhali mtoto aliyezaliwa akiwa amekufa kuliko yeye.
4 Kuzaliwa kwake hakuna maana, huondokea gizani na gizani jina lake hufunikwa.
5 Ingawa hakuwahi kuliona jua wala kujua kitu chochote, yeye ana pumziko zaidi kuliko mtu huyo,
6 Hata kama huyo mtu ataishi miaka elfu mara mbili na zaidi, lakini akashindwa kufurahia mafanikio yake, je, wote hawaendi sehemu moja?
7 Juhudi zote za binadamu ni kwa ajili ya kinywa chake,
hata hivyo hamu yake kamwe haitoshelezwi.
8 Mtu mwenye hekima ana faida gani
zaidi ya mpumbavu?
Mtu maskini anapata faida gani
kwa kujua jinsi ya kujistahi
mbele ya watu wengine?
9 Ni bora kile ambacho jicho linakiona
kuliko hamu isiyotoshelezwa.
Hili nalo ni ubatili,
ni kukimbiza upepo.
10 Lolote lililopo limekwisha kupewa jina,
naye mwanadamu alivyo ameshajulikana;
hakuna mtu awezaye kushindana
na mwenye nguvu kuliko yeye.
11 Maneno yanavyokuwa mengi,
ndivyo yanavyokosa maana,
Je, hilo linamfaidia vipi yeyote?
12 Kwa maana ni nani anayejua lililo jema kwa ajili ya maisha ya mwanadamu, katika siku chache na za ubatili anazopita kama kivuli? Ni nani awezaye kumwambia yatakayotokea chini ya jua baada ya yeye kuondoka?