11
Hukumu Juu Ya Viongozi Wa Israeli
1 Ndipo Roho akaniinua na kunileta mpaka kwenye lango la nyumba ya Bwana linalotazama upande wa mashariki. Pale kwenye ingilio la lango kulikuwepo wanaume ishirini na watano, nami nikaona miongoni mwao Yaazania mwana wa Azuri na Pelatia mwana wa Benaya, viongozi wa watu.
2 Bwana akaniambia, “Mwanadamu, hawa ndio wafanyao hila na kutoa mashauri potovu katika mji huu.
3 Wao husema, ‘Je, hivi karibuni hautakuwa wakati wa kujenga nyumba? Mji huu ni chungu cha kupikia, nasi ndio nyama.’
4 Kwa hiyo toa unabii dhidi yao, tabiri, Ewe mwanadamu.”
5 Kisha Roho wa Bwana akaja juu yangu, naye akaniambia niseme: “Hili ndilo Bwana asemalo: Hili ndilo ninyi mnalosema, ee nyumba ya Israeli, lakini ninajua mnalowaza mioyoni mwenu.
6 Mmewaua watu wengi katika mji huu na kujaza barabara zake maiti.
7 “Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi: maiti ulizozitupa huko ni nyama na mji huu ni chungu, lakini nitawaondoa mtoke huko.
8 Mnaogopa upanga, nao upanga huo ndio nitakaouleta juu yenu, asema Bwana Mwenyezi.
9 Nitawaondoa mtoke katika mji na kuwatia mikononi mwa wageni nami nitawaadhibu.
10 Mtaanguka kwa upanga, nami nitatimiza hukumu dhidi yenu katika mipaka ya Israeli. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Bwana.
11 Mji huu hautakuwa chungu kwa ajili yenu, wala hamtakuwa nyama ndani yake. Nitatoa hukumu dhidi yenu katika mipaka ya Israeli.
12 Nanyi mtajua ya kuwa Mimi ndimi Bwana, kwa kuwa hamkufuata amri zangu wala kuzishika sheria zangu, bali mmefuata mwenendo wa mataifa yanayowazunguka.”
13 Basi nilipokuwa ninatoa unabii, Pelatia mwana wa Benaya akafa. Ndipo nikaanguka kifudifudi, nikalia kwa sauti kuu nikasema, “Ee Bwana Mwenyezi! Je utaangamiza kabisa mabaki ya Israeli?”
14 Neno la Bwana likanijia kusema:
15 “Mwanadamu, ndugu zako, ndugu zako ambao ni wa uhusiano wa damu na nyumba yote ya Israeli, ndio wale ambao watu wa Yerusalemu wamesema, ‘Wako mbali na Bwana; nchi hii tulipewa sisi kuwa milki yetu.’
Ahadi Ya Kurudi Kwa Israeli
16 “Kwa hiyo sema, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ingawa niliwapeleka mbali miongoni mwa mataifa na kuwatawanya katika nchi mbalimbali, lakini kwa kitambo kidogo mimi nimekuwa mahali patakatifu kwao katika nchi walizokwenda.’
17 “Kwa hiyo sema: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitawakusanyeni kutoka mataifa na kuwarudisha kutoka nchi ambazo mmetawanywa, nami nitawarudishia nchi ya Israeli.’
18 “Watairudia nchi na kuondoa vinyago vyote vya upotovu na sanamu zote za machukizo.
19 Nitawapa moyo mmoja na kuweka roho mpya ndani yao, nitaondoa kutoka ndani yao moyo wa jiwe na kuwapa moyo wa nyama.
20 Kisha watafuata amri zangu na kuwa waangalifu kutii sheria zangu. Watakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wao.
21 Lakini kwa wale ambao mioyo yao imeambatana na vinyago vyao vya upotovu na sanamu zao za machukizo, nitaleta juu ya vichwa vyao yale waliyotenda asema Bwana Mwenyezi.”
22 Ndipo wale makerubi, wenye magurudumu pembeni mwao, wakakunjua mabawa yao, nao utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwa juu yao.
23 Basi utukufu wa Bwana ukapaa juu kutoka mji, ukatua juu ya mlima ulio upande wa mashariki ya mji.
24 Roho akaniinua na kunileta mpaka kwa watu wa uhamisho huko Ukaldayo nikiwa katika yale maono niliyopewa na Roho wa Mungu.
Ndipo maono niliyokuwa nimeyaona yakanitoka,
25 nami nikawaeleza wale watu wa uhamisho kila kitu Bwana alichokuwa amenionyesha.