33
Wajibu Wa Ezekieli Kuwa Mlinzi Kwa Watu Wake
1 Neno la Bwana likanijia kusema:
2 “Mwanadamu, sema na watu wako uwaambie, ‘Nitakapoleta upanga dhidi ya nchi, nao watu wa nchi wakamchagua mmoja wa watu wao na kumfanya awe mlinzi wao,
3 naye auonapo upanga unakuja dhidi ya nchi na kupiga tarumbeta kuonya watu,
4 kama mtu yeyote asikiapo sauti ya tarumbeta hakukubali kuonywa, basi upanga ujapo na kuutoa uhai wake, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe.
5 Kwa kuwa alisikia sauti ya tarumbeta lakini hakukubali maonyo, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe. Kama angekubali maonyo, angelijiokoa mwenyewe.
6 Lakini kama mlinzi akiona upanga unakuja na asipige tarumbeta kuonya watu na upanga ukija na kutoa uhai wa mmoja wao, yule mtu ataondolewa kwa sababu ya dhambi yake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwa mlinzi huyo.’
7 “Mwanadamu, nimekufanya wewe kuwa mlinzi kwa ajili ya nyumba ya Israeli, kwa hiyo sikia neno nisemalo na uwape maonyo kutoka kwangu.
8 Nimwambiapo mtu mwovu, ‘Ewe mtu mwovu, hakika utakufa,’ nawe hukusema neno la kumwonya ili atoke katika njia zake, yule mtu mwovu atakufa kwa ajili ya dhambi yake, mimi nitaitaka damu yake mkononi mwako.
9 Lakini kama utamwonya huyo mtu mwovu aache njia zake mbaya naye hafanyi hivyo, atakufa kwa ajili ya dhambi yake, lakini utakuwa umejiokoa mwenyewe.
10 “Mwanadamu, sema na nyumba ya Israeli uwaambie, ‘Hili ndilo mnalosema: “Makosa yetu na dhambi zetu zimetulemea, nasi tunadhoofika kwa sababu ya hayo. Tutawezaje basi kuishi?” ’
11 Waambie, ‘Hakika kama mimi niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, sifurahii kifo cha watu waovu, bali kwamba wageuke kutoka njia zao mbaya wapate kuishi. Geukeni! Geukeni kutoka njia zenu mbaya! Kwa nini mkafe, ee nyumba ya Israeli?’
12 “Kwa hiyo, mwanadamu, waambie watu wako, ‘Haki ya mtu mwenye haki haitamwokoa wakati anapoacha kutii, wala uovu wa mtu mwovu hautamsababisha yeye kuanguka anapotubu na kuacha uovu. Mtu mwenye haki, kama akitenda dhambi, hataishi kwa sababu ya uadilifu wake wa awali.’
13 Kama nikimwambia mtu mwenye haki kwamba hakika utaishi, lakini akategemea hiyo haki yake na kutenda uovu, hakuna tendo lolote la haki alilotenda litakalokumbukwa, atakufa kwa ajili ya uovu alioutenda.
14 Nami kama nikimwambia mtu mwovu, ‘Hakika utakufa,’ kisha akageuka kutoka dhambi yake na kufanya lile lililo haki na sawa,
15 kama akirudisha kile alichochukua rehani kwa ajili ya deni, akarudisha alichoiba na kufuata amri zile ziletazo uzima, wala hafanyi uovu, hakika ataishi, hatakufa.
16 Hakuna dhambi yoyote aliyoitenda itakayokumbukwa juu yake. Ametenda lile lililo haki na sawa, hakika ataishi.
17 “Lakini watu wako wanasema, ‘Njia ya Bwana si sawa.’ Lakini ni njia zao ambazo si sawa.
18 Kama mtu mwenye haki akigeuka kutoka uadilifu wake na kufanya uovu, atakufa kwa ajili ya huo uovu.
19 Naye mtu mwovu kama akigeuka kutoka uovu wake na kufanya lile lililo haki na sawa, kwa kufanya hivyo ataishi.
20 Lakini, ee nyumba ya Israeli, unasema, ‘Njia ya Bwana si sawa.’ Lakini nitamhukumu kila mmoja wenu sawasawa na njia zake mwenyewe.”
Anguko La Yerusalemu Laelezewa
21 Mwaka wa kumi na mbili wa uhamisho wetu, mwezi wa kumi, siku ya tano, mtu aliyekuwa ametoroka kutoka Yerusalemu akanijia na kusema, “Mji wa Yerusalemu umeanguka!”
22 Basi jioni kabla mtu huyo hajaja, mkono wa Bwana, ulikuwa juu yangu, naye alifungua kinywa changu kabla ya mtu yule aliyenijia asubuhi hajafika. Basi kinywa changu kilifunguliwa na sikuweza tena kunyamaza.
23 Ndipo neno la Bwana likanijia kusema:
24 “Mwanadamu, watu wanaoishi katika magofu hayo katika nchi ya Israeli wanasema hivi, ‘Abrahamu alikuwa mtu mmoja tu, hata hivyo akaimiliki nchi. Lakini sisi ni wengi, hakika tumepewa nchi kuwa milki yetu.’
25 Kwa hiyo waambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kwa kuwa mnakula nyama pamoja na damu na kuinulia sanamu zenu macho na kumwaga damu, je, mtaimiliki nchi?
26 Mnategemea panga zenu, mnafanya mambo ya machukizo na kila mmoja wenu humtia unajisi mke wa jirani yake. Je, mtaimiliki nchi?’
27 “Waambie hivi: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Hakika kama niishivyo, wale waliobaki katika magofu wataanguka kwa upanga, wale walio nje mashambani nitawatoa wararuliwe na wanyama pori, nao wale walio katika ngome na kwenye mapango watakufa kwa tauni.
28 Nitaifanya nchi kuwa ukiwa na utupu na kiburi cha nguvu zake zitafikia mwisho, nayo milima ya Israeli itakuwa ukiwa ili mtu yeyote asipite huko.
29 Kisha watajua kuwa Mimi ndimi Bwana, nitakapokuwa nimeifanya nchi kuwa ukiwa na utupu kwa sababu ya mambo yote ya machukizo waliyotenda.’
30 “Kwa habari yako wewe, mwanadamu, watu wako wanaongea habari zako wakiwa karibu na kuta na kwenye milango ya nyumba, wakiambiana kila mmoja na mwenzake, ‘Njooni msikie ujumbe ule utokao kwa Bwana.’
31 Watu wangu wanakujia, kama wafanyavyo, nao wanaketi mbele yako kama watu wangu na kusikiliza maneno yako, lakini hawayatendi. Kwa maana udanganyifu u katika midomo yao, lakini mioyo yao ina tamaa ya faida isiyo halali.
32 Naam, mbele yao umekuwa tu kama yeye aimbaye nyimbo za mapenzi kwa sauti nzuri za kuvutia na kupiga vyombo kwa ustadi, kwa kuwa wanasikia maneno yako lakini hawayatendi.
33 “Wakati mambo haya yote yatakapotimia, kwa kuwa hakika yatatokea, ndipo watakapojua kwamba nabii amekuwepo miongoni mwao.”