37
Bonde La Mifupa Mikavu
1 Mkono wa Bwana ulikuwa juu yangu, naye akanitoa nje kwa Roho wa Bwana na kuniweka katikati ya bonde lililokuwa limejaa mifupa tele.
2 Akanipitisha pande zote kwenye hiyo mifupa, nami nikaona mifupa mingi sana ndani ya lile bonde, mifupa iliyokuwa imekauka sana.
3 Akaniuliza, “Mwanadamu, mifupa hii yaweza kuishi?”
Nikajibu, “Ee Bwana Mwenyezi, wewe peke yako wajua.”
4 Ndipo akaniambia, “Itabirie mifupa hii na uiambie, ‘Enyi mifupa mikavu, sikieni neno la Bwana!
5 Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo kwa hii mifupa: Nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi.
6 Nitawawekea mishipa, nami nitaifanya nyama ije juu yenu na kuwafunika kwa ngozi. Nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtakuwa hai. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana.’ ”
7 Basi nikatabiri kama nilivyoamriwa. Wakati nilipokuwa ninatabiri, kukawa na sauti, sauti ya kugongana, nayo mifupa ikasogeleana, mfupa kwa mfupa mwenziwe.
8 Nikatazama, mishipa na nyama vikatokea juu ya mifupa na ngozi ikaifunika, lakini hapakuwepo pumzi ndani yake.
9 Ndipo aliponiambia, “Utabirie upepo, tabiri, mwanadamu na uuambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Njoo kutoka pande nne, ee pumzi, nawe upulizie pumzi ndani ya hawa waliouawa, ili wapate kuishi.’ ”
10 Hivyo nikatabiri kama alivyoniamuru, nayo pumzi ikawaingia, wakawa hai na wakasimama kwa miguu yao, jeshi kubwa mno.
11 Ndipo akaniambia: “Mwanadamu, mifupa hii ni nyumba yote ya Israeli. Nao wanasema, ‘Mifupa yetu imekauka na tumaini letu limetoweka, tumekatiliwa mbali.’
12 Hivyo watabirie na uwaambie: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Enyi watu wangu, nitayafunua makaburi yenu na kuwatoa ndani yake, nami nitawarudisha tena katika nchi ya Israeli.
13 Ndipo ninyi watu wangu, mtakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana, nitakapoyafunua makaburi yenu na kuwatoa humo.
14 Nitatia Roho yangu ndani yenu nanyi mtaishi, nami nitawakalisha katika nchi yenu wenyewe. Ndipo mtakapojua kwamba Mimi Bwana nimenena, nami nitalitenda, asema Bwana!’ ”
Taifa Moja Chini Ya Mfalme Mmoja
15 Neno la Bwana likanijia kusema:
16 “Mwanadamu, chukua fimbo na uandike juu yake, ‘Hii ni kwa ajili ya Yuda na Waisraeli waliofungamana naye.’ Kisha chukua fimbo nyingine, uandike juu yake, ‘Fimbo ya Efraimu, ni kwa ajili ya Yosefu na nyumba yote ya Israeli wanaofungamana naye.’
17 Ziunganishe pamoja kuwa fimbo moja ili kwamba ziwe fimbo moja katika mkono wako.
18 “Watu wako watakapokuuliza, ‘Je, hutatuambia ni nini maana ya jambo hili?’
19 Waambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitaichukua fimbo ya Yosefu, iliyoko mikononi mwa Efraimu na ya makabila ya Israeli yanayofungamana naye na kuiunganisha na fimbo ya Yuda, nikizifanya kuwa fimbo moja, nao watakuwa wamoja katika mkono wangu.’
20 Inua mbele ya macho yao zile fimbo ulizoziandika
21 kisha waambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitawatoa Waisraeli katika mataifa walikokuwa wamekwenda. Nitawakusanya popote walipo na kuwarudisha katika nchi yao wenyewe.
22 Nitawafanya kuwa taifa moja katika nchi, katika milima ya Israeli. Patakuwa na mfalme mmoja juu yao wote na kamwe hawatagawanyika tena kuwa mataifa mawili au kugawanyika katika falme mbili.
23 Hawatajitia tena unajisi kwa sanamu zao na vinyago vyao visivyo na maana wala kwa makosa yao yoyote, kwa maana nitawaokoa kutoka dhambi zao zote zilizowarudisha nyuma, nami nitawatakasa. Wao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao.
24 “ ‘Mtumishi wangu Daudi atakuwa mfalme juu yao, nao wote watakuwa na mchungaji mmoja. Watafuata sheria zangu na kuzishika amri zangu kwa uangalifu.
25 Wataishi katika nchi niliyompa mtumishi wangu Yakobo, nchi ambamo baba zenu waliishi. Wao na watoto wao na watoto wa watoto wao wataishi humo milele, naye Daudi mtumishi wangu atakuwa mkuu wao milele.
26 Nitafanya nao Agano la amani, litakuwa Agano la milele. Nitawafanya imara na kuongeza idadi yao, nami nitaweka mahali patakatifu pangu miongoni mwao milele.
27 Maskani yangu yatakuwa pamoja nao, nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
28 Ndipo mataifa watakapojua kwamba Mimi Bwana ndiye ninayeifanya Israeli kuwa takatifu, wakati mahali patakatifu pangu patakapokuwa miongoni mwao milele.’ ”