7
Mwisho Umewadia
1 Neno la Bwana likanijia kusema:
2 “Mwanadamu, hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo kwa nchi ya Israeli: Mwisho! Mwisho umekuja juu ya pembe nne za nchi.
3 Sasa mwisho umekuja juu yenu nami nitamwaga hasira yangu dhidi yenu. Nitawahukumu sawasawa na matendo yenu na kuwalipiza kwa ajili ya desturi zenu zote za kuchukiza.
4 Sitawaonea huruma wala sitawarehemu, hakika nitalipiza kwa ajili ya matendo yenu na desturi zenu za machukizo miongoni mwenu. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana.
5 “Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Maafa! Maafa ambayo hayajasikiwa yanakuja.
6 Mwisho umewadia! Mwisho umewadia! Umejiinua wenyewe dhidi yenu. Umewadia!
7 Maangamizi yamekuja juu yenu, ninyi mnaoishi katika nchi. Wakati umewadia, siku imekaribia, kuna hofu kuu ya ghafula, wala si furaha, juu ya milima.
8 Ninakaribia kumwaga ghadhabu yangu juu yenu na kumaliza hasira yangu dhidi yenu, nitawahukumu sawasawa na matendo yenu na kuwalipiza kwa ajili ya desturi zenu zote za machukizo.
9 Sitawaonea huruma wala sitawarehemu; nitawalipiza sawasawa na matendo yenu na desturi zenu za machukizo miongoni mwenu. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Bwana ambaye huwapiga kwa mapigo.
10 “Siku imefika! Imewadia! Maangamizi yamezuka ghafula, fimbo imechanua majivuno yamechipua!
11 Jeuri imeinuka kuwa fimbo ya kuadhibu uovu, hakuna hata mmoja wa hao watu atakayeachwa, hata mmoja wa kundi lile, hakuna utajiri, hakuna chenye thamani.
12 Wakati umewadia, siku imefika. Mnunuzi na asifurahi wala muuzaji asihuzunike, kwa maana ghadhabu iko juu ya kundi lote.
13 Muuzaji hatajipatia tena ardhi aliyoiuza wakati wote wawili wangali hai, kwa kuwa maono kuhusu kundi lote hayatatanguka. Kwa sababu ya dhambi zao, hakuna hata mmoja atakayeokoa maisha yake.
14 Wajapopiga tarumbeta na kuweka kila kitu tayari, hakuna hata mmoja atakayekwenda vitani, kwa maana ghadhabu yangu iko juu ya kundi lote.
15 “Nje ni upanga, ndani ni tauni na njaa, wale walioko shambani watakufa kwa upanga, nao wale waliomo mjini njaa na tauni vitawala.
16 Wale wote watakaopona na kutoroka watakuwa milimani, wakiomboleza kama hua wa mabondeni, kila mmoja kwa sababu ya dhambi zake.
17 Kila mkono utalegea na kila goti litakuwa dhaifu kama maji.
18 Watavaa nguo ya gunia na kufunikwa na hofu. Nyuso zao zitafunikwa na aibu na nywele za vichwa vyao zitanyolewa.
19 Watatupa fedha yao barabarani, nayo dhahabu yao itakuwa najisi. Fedha yao na dhahabu yao havitaweza kuwaokoa katika siku hiyo ya ghadhabu ya Bwana. Hawatashibisha njaa yao au kujaza matumbo yao kwa hiyo fedha wala dhahabu, kwa sababu imewaponza wajikwae dhambini.
20 Walijivunia vito vyao vizuri na kuvitumia kufanya sanamu za machukizo na vinyago vya upotovu. Kwa hiyo nitavifanya vitu hivyo kuwa najisi kwao.
21 Nitavitia vyote mikononi mwa wageni kuwa nyara na kuwa vitu vilivyotekwa mikononi mwa watu waovu wa dunia, nao watavinajisi.
22 Nitageuza uso wangu mbali nao, nao waovu wa dunia watapanajisi mahali pangu pa thamani, wanyangʼanyi watapaingia na kupanajisi.
23 “Andaa minyororo, kwa sababu nchi imejaa umwagaji wa damu na mji umejaa udhalimu.
24 Nitaleta taifa ovu kuliko yote ili kumiliki nyumba zao, nitakomesha kiburi cha wenye nguvu na mahali pao patakatifu patatiwa unajisi.
25 Hofu ya ghafula itakapokuja, watatafuta amani, lakini haitakuwepo.
26 Maafa juu ya maafa yatakuja, tetesi ya mabaya juu ya tetesi ya mabaya. Watajitahidi kupata maono kutoka kwa nabii, mafundisho ya sheria toka kwa kuhani yatapotea, vivyo hivyo shauri kutoka kwa wazee.
27 Mfalme ataomboleza, mwana wa mfalme atavikwa kukata tamaa, nayo mikono ya watu wa nchi itatetemeka. Nitawashughulikia sawasawa na matendo yao na kwa kanuni zao wenyewe nitawahukumu. Ndipo watajua kwamba Mimi ndimi Bwana.”