7
1 Kisha Bwana akamwambia Mose, “Tazama, nimekufanya kuwa kama Mungu kwa Farao, naye Aroni, huyo ndugu yako, atakuwa nabii wako.
2 Utasema kila kitu nitakachokuagiza, naye Aroni ndugu yako atamwambia Farao awaachie Waisraeli watoke katika nchi yake.
3 Lakini nitaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu. Ingawa nitazidisha ishara na maajabu katika Misri,
4 hatawasikiliza. Kisha nitaupeleka mkono wangu juu ya Misri, na kwa matendo makuu ya hukumu nitavitoa vikundi vyangu, watu wangu Waisraeli.
5 Nao Wamisri watajua kuwa Mimi ndimi Bwana nitakapounyoosha mkono wangu dhidi ya Misri na kuwatoa Waisraeli watoke humo.”
6 Mose na Aroni wakafanya sawasawa kama vile Bwana alivyowaagiza.
7 Mose alikuwa na umri wa miaka themanini na Aroni alikuwa na umri wa miaka themanini na mitatu walipozungumza na Farao.
Fimbo Ya Aroni Yawa Nyoka
8 Bwana akamwambia Mose na Aroni,
9 “Farao atakapowaambia, ‘Fanyeni muujiza,’ basi mwambie Aroni, ‘Chukua fimbo yako na uitupe chini mbele ya Farao,’ nayo fimbo itakuwa nyoka.”
10 Ndipo Mose na Aroni wakaenda kwa Farao wakafanya sawasawa kama vile Bwana alivyoagiza. Aroni akaitupa ile fimbo yake chini mbele ya Farao na maafisa wake, nayo ikawa nyoka.
11 Farao naye akawaita watu wenye maarifa na wachawi na waganga wa Kimisri, nao wakafanya vivyo hivyo kwa siri ya uganga wao.
12 Kila mmoja alitupa fimbo yake chini, nayo ikawa nyoka. Lakini fimbo ya Aroni ikazimeza zile fimbo zao.
13 Hata hivyo moyo wa Farao ukawa mgumu, naye hakuwasikiliza Mose na Aroni, sawasawa kama vile Bwana alivyokuwa amesema.
Pigo La Kwanza: Damu
14 Kisha Bwana akamwambia Mose, “Moyo wa Farao ni mgumu, anakataa kuwaachia watu kuondoka.
15 Nenda kwa Farao asubuhi wakati anapokwenda mtoni. Ngoja ukingoni mwa Naili ili uonane naye, na uchukue mkononi mwako fimbo ile iliyobadilishwa kuwa nyoka.
16 Kisha umwambie, ‘Bwana, Mungu wa Waebrania, amenituma nikuambie: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu jangwani. Lakini hadi sasa hujasikiliza.
17 Hili ndilo Bwana asemalo: Kwa hili utajua kuwa Mimi ndimi Bwana: Fimbo iliyo mkononi mwangu nitapiga nayo maji ya Naili nayo yatabadilika kuwa damu.
18 Samaki waliomo katika Mto Naili watakufa, nao mto utanuka vibaya, Wamisri hawataweza kunywa hayo maji yake.’ ”
19 Bwana akamwambia Mose, “Mwambie Aroni, ‘Chukua ile fimbo yako unyooshe mkono wako juu ya maji ya Misri, juu ya chemchemi na mifereji, juu ya madimbwi na mabwawa yote,’ navyo vitabadilika kuwa damu. Damu itakuwa kila mahali katika Misri, hata kwenye vyombo vya miti na vya mawe.”
20 Mose na Aroni wakafanya kama vile Bwana alivyokuwa amewaagiza. Akainua fimbo yake machoni pa Farao na maafisa wake na kuyapiga maji ya Mto Naili, na maji yote yakabadilika kuwa damu.
21 Samaki katika Mto Naili wakafa, nao mto ukanuka vibaya sana kiasi kwamba Wamisri hawakuweza kunywa maji yake. Damu ilikuwa kila mahali katika nchi ya Misri.
22 Lakini waganga wa Misri kwa kutumia siri ya uganga wao wakafanya vivyo hivyo, nao moyo wa Farao ukawa mgumu, hakuwasikiliza Mose na Aroni, kama vile Bwana alivyokuwa amesema.
23 Badala yake, Farao akageuka, akaenda kwenye jumba lake la kifalme, wala hakulitia hili moyoni.
24 Nao Wamisri wote wakachimba kandokando ya Mto Naili kupata maji ya kunywa, kwa sababu hawakuweza kunywa maji ya mto.
Pigo La Pili: Vyura
25 Zilipita siku saba baada ya Bwana kuyapiga maji ya Mto Naili.