6
Chukulianeni Mizigo
1 Ndugu zangu, ikiwa mtu ameghafilika akatenda dhambi, basi ninyi mlio wa rohoni, mrejesheni upya mtu huyo kwa roho ya upole. Lakini jihadharini, ili ninyi wenyewe msije mkajaribiwa.
2 Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Kristo.
3 Kama mtu yeyote akijiona kuwa yeye ni bora na kumbe sivyo, basi mtu huyo anajidanganya mwenyewe.
4 Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo aweze kujisifu, bila kujilinganisha na mtu mwingine.
5 Kwa maana, kila mtu atauchukua mzigo wake mwenyewe.
6 Basi, yeye afundishwaye katika neno na amshirikishe mwalimu wake mema yote.
7 Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna.
8 Apandaye kwa mwili, katika mwili wake atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele.
9 Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa.
10 Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waaminio.
Si Kutahiriwa Bali Kuwa Kiumbe Kipya
11 Angalieni herufi kubwa nitumiazo ninapowaandikia kwa mkono wangu mwenyewe!
12 Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili wanataka wawalazimishe kutahiriwa. Sababu pekee ya kufanya hivyo ni kuepuka kuteswa kwa ajili ya msalaba wa Kristo.
13 Hata wale waliotahiriwa wenyewe hawaitii sheria, lakini wanataka ninyi mtahiriwe ili wapate kujivuna kwa habari ya miili yenu.
14 Mungu apishie mbali nisije nikajivunia kitu chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa kwa ulimwengu.
15 Kwa maana katika Kristo Yesu, kutahiriwa au kutokutahiriwa si kitu, bali kule kuwa kiumbe kipya ni kila kitu!
16 Amani na rehema viwe na wote wanaofuata kanuni hii, na juu ya Israeli wa Mungu.
17 Hatimaye, tangu sasa mtu yeyote asinitaabishe, kwa maana nachukua katika mwili wangu chapa zake Yesu.
18 Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja na roho zenu. Amen.