20
Abrahamu Na Abimeleki
1 Basi Abrahamu akaendelea mbele kutoka huko hadi nchi ya Negebu na akaishi kati ya Kadeshi na Shuri. Kwa muda mfupi alikaa Gerari kama mgeni,
2 huko Abrahamu akasema kuhusu Sara mkewe, “Huyu ni dada yangu.” Kisha Abimeleki mfalme wa Gerari akatuma Sara aletwe, naye akamchukua.
3 Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto wakati wa usiku na kumwambia, “Wewe ni kama mfu kwa sababu ya huyu mwanamke uliyemchukua; yeye ni mke wa mtu.”
4 Wakati huo Abimeleki alikuwa bado hajamsogelea, kwa hiyo akasema, “Je, Bwana utaliharibu taifa lisilo na hatia?
5 Hakusema kwangu, ‘Huyu ni dada yangu,’ naye Sara pia hakusema, ‘Huyu ni kaka yangu’? Nimefanya haya kwa dhamiri njema na mikono safi.”
6 Kisha Mungu akamwambia katika ndoto, “Ndiyo, najua ya kwamba umefanya haya kwa dhamiri safi, kwa hiyo nimekuzuia usinitende dhambi. Ndiyo sababu sikukuacha umguse.
7 Sasa umrudishe huyo mke wa mtu, kwa maana ni nabii, naye atakuombea nawe utaishi. Lakini kama hutamrudisha, ujue kwa hakika kuwa wewe na watu wako wote mtakufa.”
8 Kesho yake asubuhi na mapema Abimeleki akawaita maafisa wake wote, na baada ya kuwaambia yote yaliyotokea, waliogopa sana.
9 Kisha Abimeleki akamwita Abrahamu na kumwambia, “Wewe umetufanyia nini? Nimekukosea nini hata ukaleta hatia kubwa namna hii juu yangu na ufalme wangu? Umenifanyia mambo ambayo hayakupasa kufanyika.”
10 Abimeleki akamuuliza Abrahamu, “Ulikuwa na kusudi gani kufanya hivi?”
11 Abrahamu akajibu, “Niliwaza kwamba, ‘Hakika hakuna hofu ya Mungu mahali hapa, nao wataniua kwa sababu ya mke wangu.’
12 Pamoja na hayo, ni kweli kwamba yeye ni dada yangu, binti wa baba yangu ingawa si mtoto wa mama yangu; basi akawa mke wangu.
13 Wakati Bwana aliponifanya nisafiri mbali na nyumbani mwa baba yangu, nilimwambia, ‘Hivi ndivyo utakavyoonyesha pendo lako kwangu: Kila mahali tutakapokwenda, kuhusu mimi sema, “Huyu ni kaka yangu.” ’ ”
14 Kisha Abimeleki akatwaa kondoo na ngʼombe, na watumwa wa kiume na wa kike akampa Abrahamu, akamrudisha Sara kwa mumewe.
15 Abimeleki akasema, “Nchi yangu iko mbele yako, ishi popote unapotaka.”
16 Akamwambia Sara, “Ninampa kaka yako shekeli elfu moja za fedha. Hii ni kufidia kosa lililofanyika dhidi yako mbele ya wote walio pamoja nawe; haki yako imethibitishwa kabisa.”
17 Kisha Abrahamu akamwomba Mungu, naye Mungu akamponya Abimeleki, mke wake, na watumwa wake wa kike kwamba waweze kupata watoto tena,
18 kwa kuwa Bwana alikuwa ameyafunga matumbo ya wote katika nyumba ya Abimeleki kwa sababu ya Sara, mke wa Abrahamu.