45
Yosefu Anajitambulisha
Hapo Yosefu hakuweza kujizuia zaidi mbele ya wote waliokuwa wamesimama karibu naye, akapaza sauti, akasema, “Mwondoeni kila mtu mbele yangu!” Kwa hiyo hapakuwepo mtu yeyote pamoja na Yosefu alipojitambulisha kwa ndugu zake. Naye akalia kwa sauti kubwa kiasi kwamba Wamisri walimsikia, hata watu wa nyumbani mwa Farao wakapata hizo habari.
Yosefu akawaambia ndugu zake, “Mimi ni Yosefu! Je, baba yangu angali hai bado?” Lakini ndugu zake hawakuweza kumjibu, kwa sababu walipatwa na hofu kuu mbele yake.
Ndipo Yosefu akawaambia ndugu zake, “Sogeeni karibu nami.” Waliposogea, akasema, “Mimi ni ndugu yenu Yosefu, yule ambaye mlimuuza Misri! Sasa, msihuzunike wala msijichukie wenyewe kwa kuniuza huku, kwa sababu ilikuwa ni ili kuokoa maisha ya watu ndiyo sababu Mungu alinituma niwatangulie ninyi. Kwa miaka miwili sasa imekuwepo njaa katika nchi, pia kwa miaka mitano ijayo hapatakuwepo kulima wala kuvuna. Lakini Mungu alinitanguliza mbele yenu ili kuhifadhi mabaki kwa ajili yenu katika nchi, na kuokoa maisha yenu kwa wokovu mkuu.
“Kwa hiyo basi, si ninyi mlionileta huku, bali ni Mungu. Alinifanya kuwa baba kwa Farao, bwana wa watu wa nyumbani mwake wote, na mtawala wa Misri yote. Sasa rudini haraka kwa baba yangu na mwambieni, ‘Hili ndilo mwanao Yosefu asemalo: Mungu amenifanya mimi kuwa bwana wa Misri yote. Shuka uje kwangu, wala usikawie. 10 Nawe utaishi katika nchi ya Gosheni na kuwa karibu nami, wewe, watoto wako na wajukuu wako, makundi yako ya kondoo, mbuzi na ngʼombe, pamoja na vyote ulivyo navyo. 11 Nitawatunza huko, kwa sababu bado iko miaka mingine mitano inayokuja ya njaa. La sivyo, wewe na nyumba yako na wote ulio nao mtakuwa fukara.’
12 “Mnaweza kujionea wenyewe, hata ndugu yangu Benyamini, kwamba hakika ni mimi ninayezungumza nanyi. 13 Mwambieni baba yangu juu ya heshima yote niliyopewa huku Misri, na kuhusu kila kitu mlichokiona. Mleteni baba yangu huku haraka.”
14 Ndipo akamkumbatia Benyamini ndugu yake na kulia, naye Benyamini akamkumbatia akilia. 15 Pia akawabusu ndugu zake wote, huku akilia. Baada ya hayo ndugu zake wakazungumza naye.
16 Habari zilipofika kwenye jumba la Farao kwamba ndugu zake Yosefu wamefika, Farao na maafisa wake wote wakafurahi. 17 Farao akamwambia Yosefu, “Waambie ndugu zako, ‘Fanyeni hivi: Pakieni wanyama wenu mrudi mpaka nchi ya Kanaani, 18 mkamlete baba yenu na jamaa zenu kwangu. Nitawapa sehemu nzuri sana ya nchi ya Misri nanyi mtafurahia unono wa nchi.’
19 “Mnaagizwa pia kuwaambia, ‘Fanyeni hivi: Chukueni magari ya kukokotwa kutoka Misri, kwa ajili ya watoto wenu na wake zenu, mkamchukue baba yenu mje. 20 Msijali kamwe kuhusu mali zenu, kwa sababu mema yote ya Misri yatakuwa yenu.’ ”
21 Hivyo wana wa Israeli wakafanya hivyo. Yosefu akawapa magari ya kukokotwa, kama Farao alivyoagiza, pia akawapa mahitaji kwa ajili ya safari yao. 22 Kila mmoja mavazi mapya, lakini Benyamini akampa shekeli 300* za fedha, na jozi tano za nguo. 23 Hivi ndivyo vitu alivyotuma kwa baba yake: punda kumi waliochukua vitu vizuri vya Misri, punda wake kumi waliobeba nafaka, mikate na mahitaji mengine ya safari. 24 Akaagana na ndugu zake walipokuwa wakiondoka, akawaambia, “Msigombane njiani!”
25 Basi wakatoka Misri na kufika kwa baba yao Yakobo katika nchi ya Kanaani. 26 Wakamwambia baba yao, “Yosefu angali hai! Ukweli ni kwamba yeye ndiye mtawala wa Misri yote.” Yakobo akapigwa na bumbuazi; hakuwasadiki. 27 Lakini walipokwisha kumweleza kila kitu ambacho Yosefu alikuwa amewaambia, na alipoona magari ya kukokotwa Yosefu aliyokuwa amempelekea ya kumchukua aende Misri, roho ya baba yao Yakobo ikahuishwa. 28 Ndipo Israeli akasema, “Nimesadiki! Mwanangu Yosefu bado yu hai. Nitakwenda nikamwone kabla sijafa.”
* 45:22 Shekeli 300 za fedha ni sawa na kilo 3.4.