25
Msifuni Bwana
Ee Bwana, wewe ni Mungu wangu,
nitakutukuza na kulisifu jina lako,
kwa maana katika ukamilifu wa uaminifu
umetenda mambo ya ajabu,
mambo yaliyokusudiwa tangu zamani.
Umeufanya mji kuwa lundo la kifusi,
mji wenye ngome kuwa magofu,
ngome imara ya wageni kuwa si mji tena,
wala hautajengwa tena kamwe.
Kwa hiyo mataifa yenye nguvu yatakuheshimu,
miji ya mataifa katili itakuheshimu wewe.
Umekuwa kimbilio la watu maskini,
kimbilio la mhitaji katika taabu yake,
hifadhi wakati wa dhoruba
na kivuli wakati wa hari.
Kwa maana pumzi ya wakatili
ni kama dhoruba ipigayo ukuta
na kama joto la jangwani.
Wewe wanyamazisha makelele ya wageni;
kama vile hari ipunguzwavyo na kivuli cha wingu,
ndivyo wimbo wa wakatili unyamazishwavyo.
 
Juu ya mlima huu Bwana Mwenye Nguvu Zote ataandaa
karamu ya vinono kwa mataifa yote,
karamu ya mvinyo wa zamani,
nyama nzuri sana na divai zilizo bora sana.
Juu ya mlima huu ataharibu
sitara ihifadhiyo mataifa yote,
kile kifuniko kifunikacho mataifa yote,
yeye atameza mauti milele.
Bwana Mwenyezi atafuta machozi katika nyuso zote;
ataondoa aibu ya watu wake duniani kote.
Bwana amesema hili.
 
Katika siku ile watasema,
“Hakika huyu ndiye Mungu wetu;
tulimtumaini, naye akatuokoa.
Huyu ndiye Bwana, tuliyemtumaini;
sisi tushangilie na kufurahia katika wokovu wake.”
 
10 Mkono wa Bwana utatulia juu ya mlima huu,
bali Moabu atakanyagwa chini
kama majani makavu yakanyagwavyo kwenye shimo la mbolea.
11 Watakunjua mikono yao katikati yake,
kama vile mwogeleaji akunjuavyo mikono yake ili aogelee.
Mungu atashusha kiburi chao
licha ya ujanja wa mikono yao.
12 Atabomoa kuta ndefu za maboma yako
na kuziangusha chini,
atazishusha chini ardhini,
mpaka mavumbini kabisa.