44
Israeli Aliyechaguliwa
“Lakini sasa sikiliza, ee Yakobo, mtumishi wangu,
Israeli, niliyemchagua.
Hili ndilo asemalo Bwana,
yeye aliyekuhuluku, aliyekuumba tumboni,
yeye atakayekusaidia:
Usiogope, ee Yakobo, mtumishi wangu,
Yeshuruni,* niliyekuchagua.
Kwa maana nitamimina maji juu ya nchi yenye kiu,
na vijito vya maji juu ya ardhi iliyokauka;
nitamimina Roho wangu juu ya watoto wako,
nayo baraka yangu juu ya wazao wako.
Nao watachipua kama manyasi katika shamba la majani,
kama mierezi kando ya vijito vya maji yatiririkayo.
Mmoja atasema, ‘Mimi ni wa Bwana’;
mwingine atajiita kwa jina la Yakobo;
vilevile mwingine ataandika juu ya mkono wake, ‘Wa Bwana,’
na kujiita kwa jina la Israeli.
Ni Bwana, Siyo Sanamu
“Hili ndilo asemalo Bwana,
Mfalme wa Israeli na Mkombozi,
Bwana Mwenye Nguvu Zote:
Mimi ni wa kwanza na Mimi ni wa mwisho;
zaidi yangu hakuna Mungu.
Ni nani basi aliye kama mimi? Yeye na atangaze.
Yeye atangaze na kuweka mbele yangu
ni kitu gani kilichotokea tangu nilipoumba watu wangu wa kale,
tena ni nini kitakachotokea:
naam, yeye na atoe unabii ni nini kitakachokuja.
Msitetemeke, msiogope.
Je, sikutangaza hili, na kutoa unabii tangu zamani?
Ninyi ni mashahidi wangu.
Je, yuko Mungu zaidi yangu mimi?
Hasha, hakuna Mwamba mwingine;
mimi simjui mwingine.”
 
Wote wachongao sanamu ni ubatili,
navyo vitu wanavyovithamini havifai kitu.
Wale ambao wanazitetea ni vipofu,
ni wajinga, nao waaibika.
10 Ni nani atengenezaye mungu na kusubu sanamu,
ambayo haiwezi kumfaidia kitu chochote?
11 Yeye pamoja na wenziwe wa aina yake wataaibishwa,
mafundi wao si kitu ila ni wanadamu tu.
Wote wakusanyike pamoja na kuwa na msimamo wao,
watashushwa chini kwa hofu na kwa fedheha.
 
12 Muhunzi huchukua kifaa
na kukifanyia kazi kwenye makaa ya moto,
hutengeneza sanamu kwa nyundo,
huifanyiza kwa nguvu za mkono wake.
Huona njaa na kupoteza nguvu zake,
asipokunywa maji huzimia.
13 Seremala hupima kwa kutumia kamba
na huuchora mstari kwa kalamu;
huchonga kwa patasi
na kutia alama kwa bikari.
Huifanyiza katika umbo la binadamu,
la mwanadamu katika utukufu wake wote,
ili iweze kukaa katika sehemu yake ya ibada ya miungu.
14 Hukata miti ya mierezi,
huchukua mtiriza au mwaloni.
Huuacha ukue miongoni mwa miti ya msituni,
au hupanda msunobari, nayo mvua huufanya ukue.
15 Ni kuni ya binadamu:
yeye huchukua baadhi yake na kuota moto,
huwasha moto na kuoka mkate.
Lakini pia huutumia kumtengeneza mungu na akamwabudu,
huitengeneza sanamu na kuisujudia.
16 Sehemu ya kuni huziweka motoni,
akapikia chakula chake,
hubanika nyama na kula hadi ashibe.
Huota moto na kusema,
“Aha! Ninahisi joto, ninaona moto.”
17 Mabaki yake hutengeneza mungu, sanamu yake;
yeye huisujudia na kuiabudu.
Huiomba na kusema,
“Niokoe; wewe ni mungu wangu.”
18 Hawajui chochote, hawaelewi chochote,
macho yao yamefungwa hata hawawezi kuona,
akili zao zimefungwa hata hawawezi kufahamu.
19 Hakuna anayefikiri,
hakuna mwenye maarifa wala ufahamu wa kusema,
“Sehemu yake nilitumia kwa kuni;
hata pia nilioka mkate juu ya makaa yake,
nikabanika nyama na kuila.
Je, nifanye machukizo kwa kile kilichobaki?
Je, nisujudie gogo la mti?”
20 Hujilisha kwa majivu, moyo uliodanganyika humpotosha;
hawezi kujiokoa mwenyewe, au kusema,
“Je, kitu hiki kilichoko katika mkono wangu wa kuume si ni uongo?”
 
21 “Ee Yakobo, kumbuka mambo haya,
ee Israeli, kwa kuwa wewe ni mtumishi wangu.
Nimekuumba wewe, wewe ni mtumishi wangu.
Ee Israeli, sitakusahau.
22 Nimeyafuta makosa yako kama wingu,
dhambi zako kama ukungu wa asubuhi.
Nirudie mimi,
kwa kuwa nimekukomboa wewe.”
 
23 Enyi mbingu, imbeni kwa furaha,
kwa maana Bwana amefanya jambo hili.
Ee vilindi vya dunia, piga kelele.
Enyi milima, pazeni sauti kwa nyimbo,
enyi misitu na miti yenu yote,
kwa maana Bwana amemkomboa Yakobo,
ameuonyesha utukufu wake katika Israeli.
Yerusalemu Kukaliwa
24 “Hili ndilo asemalo Bwana,
Mkombozi wako, aliyekuumba tumboni:
 
“Mimi ni Bwana,
niliyeumba vitu vyote,
niliyezitanda mbingu peke yangu,
niliyeitandaza nchi mwenyewe,
 
25 “mimi huzipinga ishara za manabii wa uongo,
na kuwatia upumbavu waaguzi,
niyapinduaye maarifa ya wenye hekima,
na kuyafanya kuwa upuzi,
26 niyathibitishaye maneno ya watumishi wake,
na kutimiza utabiri wa wajumbe wake,
 
“niambiaye Yerusalemu, ‘Itakaliwa na watu,’
niambiaye miji ya Yuda kuwa, ‘Itajengwa,’
na kuhusu magofu yake, ‘Mimi nitayatengeneza,’
27 niambiaye kilindi cha maji, ‘Kauka,
nami nitakausha vijito vyako,’
28 nisemaye kuhusu Koreshi, ‘Yeye ni mchungaji wangu,
naye atatimiza yote yanipendezayo;
atauambia Yerusalemu, “Ukajengwe tena,”
na kuhusu Hekalu, “Misingi yake na iwekwe.” ’
* 44:2 Yeshuruni hapa maana yake ni Yeye aliye mnyofu, yaani Israeli (ona pia Kum 32:15).