5
Wimbo Wa Shamba La Mizabibu
Nitaimba wimbo kwa ajili ya mmoja nimpendaye,
kuhusu shamba lake la mizabibu:
Mpendwa wangu alikuwa na shamba la mizabibu
kwenye kilima chenye rutuba.
Alililima na kuondoa mawe
na akaliotesha mizabibu bora sana.
Akajenga mnara wa ulinzi ndani yake,
na kutengeneza shinikizo la kukamulia divai pia.
Kisha akatazamia kupata mazao ya zabibu nzuri,
lakini lilizaa matunda mabaya tu.
 
“Basi enyi wakazi wa Yerusalemu na watu wa Yuda,
hukumuni kati yangu na shamba langu la mizabibu.
Ni nini zaidi ambacho kingeweza kufanyika kwa shamba langu la mizabibu
kuliko yale niliyofanya?
Nilipotazamia kupata zabibu nzuri,
kwa nini lilizaa zabibu mbaya tu?
Sasa nitawaambia lile nitakalolitendea
shamba langu la mizabibu:
Nitaondoa uzio wake,
nalo litaharibiwa,
nitabomoa ukuta wake,
nalo litakanyagwa.
Nitalifanya nchi ya ukiwa isiyokaliwa na watu,
halitakatiwa matawi wala kulimwa,
nayo michongoma na miiba itamea huko,
nitaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake.”
 
Shamba la mzabibu la Bwana Mwenye Nguvu Zote
ni nyumba ya Israeli,
na watu wa Yuda
ni bustani yake ya kumpendeza.
Alitazamia haki, lakini akaona umwagaji damu,
alitazamia uadilifu, lakini akasikia vilio vya taabu.
Ole Na Hukumu
Ole wenu mnaoongeza nyumba baada ya nyumba
na kuunganisha mashamba baada ya mashamba
hadi hakuna nafasi iliyobaki,
nanyi mnaishi peke yenu katika nchi.
 
Bwana Mwenye Nguvu Zote amesema nikisikia:
“Hakika nyumba kubwa zitakuwa ukiwa,
nayo majumba ya fahari yatabaki bila kukaliwa.
10 Shamba la mizabibu la eka kumi
litatoa bathi* moja ya divai,
na homeri ya mbegu zilizopandwa
itatoa efa moja tu ya nafaka.”
 
11 Ole wao wale waamkao asubuhi na mapema
wakikimbilia kunywa vileo,
wale wakawiao sana mpaka usiku,
mpaka wamewaka kwa mvinyo.
12 Wana vinubi na zeze kwenye karamu zao,
matari, filimbi na mvinyo,
lakini hawayajali matendo ya Bwana,
wala hawana heshima kwa ajili ya kazi ya mikono yake.
13 Kwa hiyo watu wangu watakwenda uhamishoni
kwa sababu ya kukosa ufahamu,
watu wao wenye vyeo watakufa kwa njaa
na watu wao wengi watakauka kwa kiu.
14 Kwa hiyo kaburi§ limeongeza hamu yake
na kupanua mdomo wake bila kikomo,
ndani mwake watashuka wakuu wao na wingi wa watu,
pamoja na wagomvi wao, na wafanyao sherehe wote.
15 Hivyo mwanadamu atashushwa,
na binadamu kunyenyekezwa,
macho ya wenye majivuno yatanyenyekezwa.
16 Lakini Bwana Mwenye Nguvu Zote atatukuzwa
kwa ajili ya haki yake,
naye Mungu Mtakatifu atajionyesha mwenyewe
kuwa mtakatifu kwa haki yake.
17 Kondoo watajilisha kwenye malisho yao wenyewe,
wana-kondoo watajilisha katika magofu ya matajiri.
 
18 Ole wao wanaovuta dhambi kwa kamba za udanganyifu
na uovu kama kwa kamba za mkokoteni,
19 kwa wale wanaosema, “Mungu na afanye haraka,
aharakishe kazi yake ili tupate kuiona.
Huo mpango wa Aliye Mtakatifu wa Israeli na ukamilike,
tena udhihirike ili tupate kuujua.”
 
20 Ole wao wanaoita ubaya ni wema,
na wema ni ubaya,
wawekao giza badala ya nuru,
na nuru badala ya giza,
wawekao uchungu badala ya utamu,
na utamu badala ya uchungu.
 
21 Ole wao walio na hekima machoni pao wenyewe,
na kujiona wenye akili machoni pao wenyewe.
 
22 Ole wao walio mashujaa kwa kunywa mvinyo,
nao walio hodari katika kuchanganya vileo,
23 wale wanaoachilia wenye hatia kwa kupokea hongo,
lakini huwanyima haki wasio na hatia.
 
24 Kwa hiyo, kama ndimi za moto zirambavyo nyasi,
na kama vile majani makavu yazamavyo katika miali ya moto,
ndivyo mizizi yao itakavyooza
na maua yao yatakavyopeperushwa kama mavumbi;
kwa kuwa wameikataa sheria ya Bwana Mwenye Nguvu Zote
na kulisukumia mbali neno la Aliye Mtakatifu wa Israeli.
25 Kwa hiyo hasira ya Bwana inawaka dhidi ya watu wake,
mkono wake umeinuliwa na anawapiga.
Milima inatetemeka,
maiti ni kama takataka kwenye barabara.
 
Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali,
mkono wake bado umeinuliwa juu.
 
26 Yeye anainua bendera kwa ajili ya mataifa yaliyo mbali,
anapiga filimbi kwa ajili ya wale walio kwenye miisho ya dunia.
Tazama wamekuja,
kwa kasi na kwa haraka!
27 Hakuna hata mmoja wao anayechoka wala kujikwaa,
hakuna hata mmoja anayesinzia wala kulala,
hakuna mkanda uliolegezwa kiunoni,
hakuna gidamu ya kiatu iliyokatika.
28 Mishale yao ni mikali,
pinde zao zote zimevutwa,
kwato za farasi wao ziko kama jiwe la gumegume,
magurudumu ya magari yao ya vita ni kama upepo wa kisulisuli.
29 Ngurumo yao ni kama ile ya simba,
wananguruma kama wana simba,
wanakoroma wanapokamata mawindo yao,
na kuondoka nayo pasipo yeyote wa kuokoa.
30 Katika siku ile watanguruma juu yake
kama ngurumo za bahari.
Kama mtu akiitazama nchi,
ataona giza na dhiki;
hata nuru itatiwa giza kwa mawingu.
* 5:10 Bathi moja ni sawa na lita 22. 5:10 Homeri moja ni sawa na lita 220. 5:10 Efa moja ni sawa na lita 22. § 5:14 Kaburi hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol.