61
Mwaka Wa Upendeleo Wa Bwana
Roho wa Bwana Mwenyezi yu juu yangu,
kwa sababu Bwana amenitia mafuta
kuwahubiria maskini habari njema.
Amenituma kuwaganga waliovunjika moyo,
kuwatangazia mateka uhuru wao,
na hao waliofungwa
habari za kufunguliwa kwao;
kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,
na siku ya kisasi ya Mungu wetu,
kuwafariji wote waombolezao,
na kuwapa mahitaji
wale wanaohuzunika katika Sayuni,
ili kuwapa taji ya uzuri badala ya majivu,
mafuta ya furaha badala ya maombolezo,
vazi la sifa badala ya roho ya kukata tamaa.
Nao wataitwa mialoni ya haki,
pando la Bwana,
ili kuonyesha utukufu wake.
 
Watajenga upya magofu ya zamani
na kupatengeneza mahali palipoachwa ukiwa zamani;
watafanya upya miji iliyoharibiwa,
iliyoachwa ukiwa kwa vizazi vingi.
Wageni watayachunga makundi yenu,
wageni watafanya kazi katika mashamba yenu,
na kutunza mashamba yenu ya mizabibu.
Nanyi mtaitwa makuhani wa Bwana,
mtaitwa watumishi wa Mungu wetu.
Mtakula utajiri wa mataifa,
nanyi katika utajiri wao mtajisifu.
 
Badala ya aibu yao
watu wangu watapokea sehemu maradufu,
na badala ya fedheha
watafurahia katika urithi wao;
hivyo watarithi sehemu maradufu katika nchi yao,
nayo furaha ya milele itakuwa yao.
 
“Kwa maana Mimi, Bwana, napenda haki,
na ninachukia unyangʼanyi na uovu.
Katika uaminifu wangu nitawapa malipo yao
na kufanya agano la milele nao.
Wazao wao watajulikana miongoni mwa mataifa,
na uzao wao miongoni mwa kabila za watu.
Wale wote watakaowaona watatambua
kuwa ni taifa ambalo Bwana amelibariki.”
 
10 Ninafurahia sana katika Bwana,
nafsi yangu inashangilia katika Mungu wangu.
Kwa maana amenivika mavazi ya wokovu,
na kunipamba kwa joho la haki,
kama vile bwana arusi apambavyo
kichwa chake kama kuhani,
na kama bibi arusi ajipambavyo
kwa vito vyake vya thamani.
11 Kwa maana kama vile ardhi ifanyavyo chipukizi kuota,
na bustani isababishavyo mbegu kuota,
ndivyo Bwana Mwenyezi atafanya haki na sifa
zichipuke mbele ya mataifa yote.