41
1 “Je, waweza kumvua Lewiathani kwa ndoano ya samaki,
au kufunga ulimi wake kwa kamba?
2 Waweza kupitisha kamba puani mwake,
au kutoboa taya lake kwa kulabu?
3 Je, ataendelea kukuomba umhurumie?
Atasema nawe maneno ya upole?
4 Je, atafanya agano nawe ili umtwae
awe mtumishi wako maisha yake yote?
5 Je, utamfuga na kumfanya rafiki kama ndege,
au kumfunga kamba kwa ajili ya wasichana wako?
6 Je, wafanyabiashara watabadilishana bidhaa kwa ajili yake?
Watamgawanya miongoni mwa wafanyao biashara?
7 Je, waweza kuijaza ngozi yake kwa vyuma vyenye ncha kali,
au kichwa chake kwa mkuki wa kuvulia samaki?
8 Kama ukiweka mkono wako juu yake,
utavikumbuka hivyo vita na kamwe hutarudia tena!
9 Tumaini lolote la kumtiisha ni kujidanganya;
kule kumwona tu kunamwangusha mtu chini.
10 Hakuna yeyote aliye mkali athubutuye kumchokoza.
Ni nani basi awezaye kusimama dhidi yangu?
11 Ni nani mwenye madai dhidi yangu ili nipate kumlipa?
Kila kitu kilicho chini ya mbingu ni mali yangu.
12 “Sitashindwa kunena juu ya maungo yake,
nguvu zake na umbo lake zuri.
13 Ni nani awezaye kumvua gamba lake la nje?
Ni nani awezaye kumsogelea na lijamu?
14 Nani athubutuye kuufungua mlango wa kinywa chake,
kilichozungukwa na meno yake ya kutisha pande zote?
15 Mgongo wake una safu za ngao
zilizoshikamanishwa imara pamoja;
16 kila moja iko karibu sana na mwenzake,
wala hakuna hewa iwezayo kupita kati yake.
17 Zimeunganishwa imara kila moja na nyingine;
zimengʼangʼaniana pamoja wala haziwezi kutenganishwa.
18 Akipiga chafya mwanga humetameta;
macho yake ni kama mionzi ya mapambazuko.
19 Mienge iwakayo humiminika kutoka kinywani mwake;
cheche za moto huruka nje.
20 Moshi hufuka kutoka puani mwake,
kama kutoka kwenye chungu kinachotokota kwa moto wa matete.
21 Pumzi yake huwasha makaa ya mawe,
nayo miali ya moto huruka kutoka kinywani mwake.
22 Nguvu hukaa katika shingo yake;
utisho hutangulia mbele yake.
23 Mikunjo ya nyama yake imeshikamana imara pamoja;
iko imara na haiwezi kuondolewa.
24 Kifua chake ni kigumu kama mwamba,
kigumu kama jiwe la chini la kusagia.
25 Ainukapo, mashujaa wanaogopa;
hurudi nyuma mbele yake anapokwenda kwa kishindo.
26 Upanga unaomfikia haumdhuru,
wala mkuki au mshale wala fumo.
27 Chuma hukiona kama unyasi,
na shaba kama mti uliooza.
28 Mishale haimfanyi yeye akimbie;
mawe ya kombeo kwake ni kama makapi.
29 Rungu kwake huwa kama kipande cha jani kavu;
hucheka sauti za kugongana kwa mkuki.
30 Sehemu zake za chini kwenye tumbo
zina menomeno na mapengo kama vigae vya chungu,
zikiacha mburuzo kwenye matope
kama chombo chenye meno cha kupuria.
31 Huvisukasuka vilindi kama sufuria kubwa ichemkayo,
na kukoroga bahari kama chungu cha marhamu.
32 Anapopita nyuma yake huacha mkondo unaometameta;
mtu angedhani vilindi vilikuwa na mvi.
33 Hakuna chochote duniani kinacholingana naye:
yeye ni kiumbe kisicho na woga.
34 Yeye huwatazama chini wale wote wenye kujivuna;
yeye ni mfalme juu ya wote wenye kiburi.”