10
Tola
1 Baada ya Abimeleki, Tola mwana wa Pua mwana wa Dodo, mtu wa Isakari, aliyeishi huko Shamiri, katika nchi ya vilima ya Efraimu, akainuka kuokoa Israeli.
2 Akaamua Israeli kwa miaka ishirini na mitatu. Ndipo akafa, naye akazikwa huko Shamiri.
Yairi
3 Baada yake akafuatiwa na Yairi, Mgileadi, ambaye aliamua Israeli kwa miaka ishirini na miwili.
4 Alikuwa na wana thelathini waliopanda punda thelathini. Nao walikuwa na miji thelathini iliyoko Gileadi, inayoitwa Hawoth-Yairi mpaka leo.
5 Yairi akafa, naye akazikwa huko Kamoni.
Yefta
6 Wana wa Israeli wakatenda tena maovu machoni pa Bwana. Wakaabudu Mabaali na Maashtorethi, miungu ya Aramu, miungu ya Sidoni, miungu ya Moabu, miungu ya Waamoni na miungu ya Wafilisti. Kwa kuwa Waisraeli walimwacha Bwana wala hawakuendelea kumtumikia,
7 hivyo hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya Israeli, naye akawatia mikononi mwa Wafilisti na Waamoni,
8 ambao waliwaonea na kuwatesa mwaka ule. Kwa miaka kumi na minane wakawatesa Waisraeli wote upande wa mashariki ya Mto Yordani katika Gileadi, nchi ya Waamori.
9 Waamoni nao wakavuka Yordani ili kupigana na Yuda, Benyamini na nyumba ya Efraimu, nayo nyumba ya Israeli ikawa katika taabu kubwa.
10 Ndipo Waisraeli wakamlilia Bwana wakasema, “Tumetenda dhambi dhidi yako, kumwacha Mungu wetu na kutumikia Mabaali.”
11 Bwana akawaambia, “Wakati Wamisri, Waamori, Waamoni, Wafilisti,
12 Wasidoni, Waamaleki na Wamaoni walipowaonea na ninyi mkanililia na kuomba msaada, je, sikuwaokoa kutoka mikononi mwao?
13 Lakini ninyi mmeniacha mimi na kutumikia miungu mingine, kwa hiyo sitawaokoa tena.
14 Nendeni mkaililie ile miungu mlioichagua. Hiyo miungu na iwaokoe mnapokuwa katika taabu!”
15 Lakini Waisraeli wakamwambia Bwana, “Tumetenda dhambi. Ututendee lile unaloona kuwa jema kwako, lakini twakusihi utuokoe sasa.”
16 Nao wakaiondoa hiyo miungu migeni katikati yao nao wakamtumikia Bwana. Naye akahuzunika kwa sababu ya taabu ya Israeli.
17 Ndipo Waamoni wakaitwa vitani na kupiga kambi huko Gileadi, Waisraeli wakakusanyika na kupiga kambi huko Mispa.
18 Viongozi wa watu wa Gileadi wakaambiana wao kwa wao, “Yeyote yule atakayeanzisha mashambulizi dhidi ya Waamoni atakuwa kiongozi wa wote wakaao Gileadi.”