13
Kuzaliwa Kwa Samsoni
1 Waisraeli wakafanya maovu tena mbele za Bwana. Hivyo Bwana akawatia mikononi mwa Wafilisti kwa muda wa miaka arobaini.
2 Basi palikuwa na mtu mmoja wa Sora, aliyeitwa Manoa, wa kabila la Wadani, naye alikuwa na mke ambaye alikuwa tasa na hakuwa na mtoto.
3 Malaika wa Bwana akamtokea huyo mwanamke na kumwambia, “Wewe ni tasa na huna mtoto, lakini utachukua mimba na utamzaa mtoto mwanaume.
4 Lakini ujihadhari sana usinywe mvinyo wala kileo kingine chochote, wala usile kitu chochote kilicho najisi,
5 kwa kuwa utachukua mimba na utamzaa mtoto mwanaume. Wembe usipite kichwani pake, kwa kuwa huyo mwana atakuwa Mnadhiri wa Mungu, aliyewekwa wakfu kwa ajili ya Mungu tangu tumboni mwa mama yake, naye ataanza kuwaokoa Waisraeli kutoka mikononi mwa Wafilisti.”
6 Ndipo huyo mwanamke akamwendea mumewe na kumweleza kuwa, “Mtu wa Mungu alinijia. Kule kuonekana kwake kulikuwa kama kwa malaika wa Mungu, wa kutisha sana. Sikumuuliza alikotoka wala hakuniambia jina lake.
7 Lakini aliniambia, ‘Utachukua mimba na utazaa mtoto mwanaume. Basi sasa, usinywe mvinyo wala kileo kingine chochote wala usile kitu kilicho najisi, kwa kuwa huyo mtoto atakuwa Mnadhiri wa Mungu tangu tumboni mwa mama yake mpaka kufa kwake.’ ”
8 Ndipo Manoa akamwomba Bwana, akasema: “Ee Bwana, nakusihi, huyo mtu wa Mungu uliyemtuma kwetu aje tena ili atufundishe jinsi ya kumlea huyo mwana atakayezaliwa.”
9 Mungu akamsikia Manoa, naye malaika wa Mungu akamjia tena huyo mwanamke alipokuwa shambani, lakini mumewe Manoa hakuwepo.
10 Basi yule mwanamke akaenda haraka na kumwambia mumewe, “Tazama mtu yule aliyenitokea siku ile yupo hapa!”
11 Manoa akainuka akaandamana na mkewe. Alipomfikia yule mtu akamuuliza, “Je, wewe ndiye yule uliyesema na mke wangu?”
Akasema, “Mimi ndiye.”
12 Basi Manoa akamuuliza, “Wakati maneno yako yatakapotimia, masharti ya maisha ya mtoto huyu yatakuwa nini na kazi yake itakuwa ni nini?”
13 Malaika wa Bwana akamjibu, “Mke wako hana budi kufanya yale yote niliyomwambia.
14 Kamwe asile kitu chochote kitakachotoka katika mzabibu, wala asinywe mvinyo wa aina yoyote wala kileo chochote wala asile kitu chochote kilicho najisi. Hana budi kufanya kila kitu nilichomwagiza.”
15 Manoa akamjibu yule malaika wa Bwana, “Twakuomba usubiri kwanza ili tuweze kuandaa mwana-mbuzi kwa ajili yako.”
16 Malaika wa Bwana akamjibu, “Hata kama utanizuia, sitakula chochote kwako. Lakini ukitaka kuandaa sadaka ya kuteketezwa, mtolee Bwana hiyo sadaka.” (Kwa kuwa Manoa hakujua kuwa alikuwa malaika wa Bwana.)
17 Ndipo Manoa akamuuliza yule malaika wa Bwana, “Jina lako ni nani, ili kwamba tuweze kukupa heshima hapo hayo uliyonena yatakapotimia?”
18 Akamjibu, “Kwa nini unauliza Jina langu? Ni Jina la ajabu.”
19 Ndipo Manoa akamchukua mwana-mbuzi, pamoja na sadaka ya unga, naye akamtolea Bwana dhabihu hapo juu ya mwamba. Naye yule malaika wa Bwana akafanya jambo la ajabu wakati Manoa na mkewe wakiwa wanaangalia:
20 Mwali wa moto kutoka hapo madhabahuni ulipowaka kuelekea mbinguni, malaika wa Bwana akapaa ndani ya huo mwali. Manoa na mkewe, kwa kuona jambo hili, wakaanguka chini kifudifudi.
21 Malaika wa Bwana hakumtokea tena Manoa na mkewe. Ndipo Manoa akatambua kuwa huyo alikuwa malaika wa Bwana.
22 Manoa akamwambia mkewe, “Hakika tutakufa, kwa kuwa tumemwona Mungu.”
23 Lakini mkewe akamwambia, “Ikiwa Bwana alikuwa amekusudia kutuua, asingelipokea sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya unga kutoka mikononi mwetu, wala asingelituonyesha mambo haya yote wala kututangazia mambo kama haya wakati huu.”
24 Yule mwanamke akazaa mtoto wa kiume akamwita jina lake Samsoni. Kijana akakua, naye Bwana akambariki.
25 Roho wa Bwana akaanza kumsukuma wakati alipokuwa huko Mahane-Dani, kati ya Sora na Eshtaoli.