3
Mataifa Yaliyobaki Katika Ile Nchi
Haya ndiyo mataifa Bwana aliyoyaacha ili kuwajaribu Waisraeli wote ambao hawakujua vita vyovyote vya Kanaani (alifanya hivi ili tu kuwafundisha wazao wa Waisraeli ambao hawakuwa wamejua vita hapo awali): wafalme watano wa Wafilisti, Wakanaani wote, Wasidoni, Wahivi waishio katika milima ya Lebanoni kuanzia Mlima wa Baal-Hermoni hadi Lebo-Hamathi. Waliachwa ili kuwajaribu Waisraeli kuona kama wangetii amri za Bwana, alizokuwa amewapa baba zao kwa mkono wa Mose.
Waisraeli wakaishi miongoni mwa Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. Wakawaoa binti zao, nao wakawatoa binti zao waolewe na wana wa hayo mataifa, na kuitumikia miungu yao.
Othnieli
Waisraeli wakafanya maovu machoni pa Bwana, wakamsahau Bwana Mungu wao na kutumikia Mabaali na Maashera. Hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya Israeli, hivyo akawauza na kuwatia mikononi mwa Kushan-Rishathaimu mfalme wa Aramu-Naharaimu* ambaye Israeli walikuwa chini yake wakimtumikia kwa muda wa miaka minane. Waisraeli walipomlilia Bwana, yeye akawainulia mwokozi, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu, ambaye aliwaokoa. 10 Roho wa Bwana akaja juu yake, hivyo akawa mwamuzi wa Israeli, akaenda vitani. Bwana akamtia Kushan-Rishathaimu mfalme wa Aramu mikononi mwa Othnieli, naye akamshinda. 11 Hivyo nchi ikawa na amani kwa muda wa miaka arobaini, mpaka Othnieli mwana wa Kenazi alipofariki.
Ehudi
12 Waisraeli wakafanya maovu mbele za Bwana tena, kwa kuwa walifanya maovu hayo Bwana akamtia nguvu Egloni mfalme wa Moabu dhidi ya Israeli. 13 Egloni akawataka Waamoni na Waamaleki waungane naye, akaja kuishambulia Israeli, nao wakatwaa Mji wa Mitende 14 Waisraeli wakawa chini ya Egloni mfalme wa Moabu kwa muda wa miaka kumi na minane.
15 Waisraeli wakamlilia tena Bwana, naye akawapa mwokozi: Ehudi, mtu wa shoto, mwana wa Gera, Mbenyamini. Waisraeli wakatuma kwa Egloni mfalme wa Moabu ushuru kwa mkono wa Ehudi. 16 Basi Ehudi alikuwa ametengeneza upanga wenye ukatao kuwili, urefu wake ni kama dhiraa moja, akaufunga upanga huo ndani ya nguo yake kwenye paja lake la mkono wa kuume. 17 Akamkabidhi ushuru Egloni mfalme wa Moabu, ambaye alikuwa mtu mnene sana. 18 Baada ya Ehudi kumkabidhi ule ushuru, wale watu waliokuwa wameubeba huo ushuru aliwaruhusu waende zao. 19 Yeye mwenyewe akafuatana nao hadi kwenye sanamu ya kuchora kwenye mawe karibu na Gilgali, ndipo yeye akarudi, akafika kwa Egloni na kusema, “Ee Mfalme, ninao ujumbe wa siri kwa ajili yako.”
Mfalme akasema, “Nyamazeni kimya!” Nao wale waliomhudumia wote wakamwacha, wakatoka nje.
20 Ndipo Ehudi akamsogelea alipokuwa ameketi peke yake kwenye chumba cha juu cha jumba lake la kifalme la majira ya kiangazi, na kusema, “Ninao ujumbe kutoka kwa Mungu kwa ajili yako.” Mfalme alipokuwa anainuka kutoka kwenye kiti chake, 21 Ehudi akaunyoosha mkono wake wa kushoto na kuufuta ule upanga aliokuwa ameufunga kwenye paja lake la kulia, akamdunga Mfalme Egloni tumboni mwake. 22 Hata mpini nao ukazama tumboni pamoja na upanga wenyewe, nao upanga ukatokea mgongoni mwake. Ehudi hakuuchomoa huo upanga, nayo mafuta yakashikamana juu ya upanga. 23 Ehudi akatoka nje barazani; akamfungia milango ya chumba cha juu na kuifunga kwa funguo.
24 Baada ya kuondoka, watumishi wakaja na kukuta milango ya chumba cha juu imefungwa kwa funguo. Wakasema, “Bila shaka amejipumzisha kwenye chumba cha ndani cha nyumba yake ya majira ya kiangazi.” 25 Wakangoja hata wakawa na fadhaa, basi wakati hakufungua milango ya chumba, wakachukua funguo na kuifungua. Tazama wakaona bwana wao amelala sakafuni, amekufa.
26 Walipokuwa wangali wanangoja, Ehudi akatoroka, akapita hapo kwenye sanamu ya kuchora kwenye mawe na kukimbilia Seira. 27 Alipofika huko, akapiga tarumbeta katika nchi ya vilima ya Efraimu, nao Waisraeli wakateremka pamoja naye kutoka vilimani, yeye akiwa anawaongoza.
28 Akawaagiza, “Nifuateni, kwa kuwa Bwana amewatia Moabu, adui zenu, mikononi mwenu.” Kwa hiyo wakateremka wakamfuata, wakavishika vivuko vya Yordani kuelekea Moabu, wala hawakuacha mtu yeyote kuvuka. 29 Wakati huo wakawaua Wamoabu watu waume wapatao 10,000 ambao wote walikuwa wenye nguvu na mashujaa; hakuna mtu yeyote aliyetoroka. 30 Siku ile Moabu wakashindwa na Israeli, nayo nchi ikawa na amani kwa miaka themanini.
Shamgari
31 Baada ya Ehudi akaja Shamgari mwana wa Anathi, aliyewapiga Wafilisti 600 kwa fimbo iliyochongoka ya kuongozea ngʼombe. Naye pia akawaokoa Waisraeli.
* 3:8 Yaani Mesopotamia ya Kaskazini-Magharibi. 3:13 Yaani Yeriko. 3:16 Dhiraa moja ni sawa na sentimita 45.