11
Kifo Cha Lazaro
Basi mtu mmoja jina lake Lazaro alikuwa mgonjwa. Yeye alikuwa akiishi Bethania kijiji cha Maria na Martha dada zake. Huyu Maria, ambaye Lazaro kaka yake alikuwa mgonjwa, ndiye yule ambaye alimpaka Bwana mafuta na kuifuta miguu yake kwa nywele zake. Hivyo hawa dada wawili walituma ujumbe kwa Yesu kumwambia, “Bwana, yule umpendaye ni mgonjwa.”
Lakini Yesu aliposikia hayo, akasema, “Ugonjwa huu hautaleta mauti bali umetokea ili kudhihirisha utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu apate kutukuzwa kutokana na ugonjwa huu.” Pamoja na hivyo, ingawa Yesu aliwapenda Martha, Maria na Lazaro ndugu yao, baada ya kusikia kwamba Lazaro ni mgonjwa, aliendelea kukawia huko alikokuwa kwa siku mbili zaidi.
Ndipo akawaambia wanafunzi wake, “Haya, turudi Uyahudi.”
Wanafunzi wake wakamwambia, “Rabi, Wayahudi walikuwa wanataka kukupiga mawe, nawe unataka kurudi huko?”
Yesu akawajibu, “Si kuna saa kumi na mbili za mchana katika siku moja? Wala watembeao mchana hawawezi kujikwaa kwa maana wanaona nuru ya ulimwengu huu. 10  Lakini wale watembeao usiku hujikwaa kwa sababu hakuna nuru ndani yao.”
11 Baada ya kusema haya, Yesu akawaambia, “Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini naenda kumwamsha.”
12 Wanafunzi wakamwambia, “Bwana, kama amelala usingizi ataamka.” 13 Hata hivyo, Yesu alikuwa anazungumzia kuwa Lazaro amekufa, lakini wanafunzi wake hawakuelewa, walidhani kwamba anasema Lazaro amelala usingizi tu.
14 Kwa hiyo Yesu akawaambia waziwazi, “Lazaro amekufa. 15  Hata hivyo nafurahi kwa kuwa sikuwepo huko kabla ya Lazaro kufa, ili mpate kuamini. Lakini sasa twendeni kwake.”
16 Tomaso aliyeitwa Pacha akawaambia wanafunzi wenzake, “Sisi nasi twendeni tukafe pamoja naye.”
Yesu Ndiye Ufufuo Na Uzima
17 Yesu alipowasili huko alikuta Lazaro amekuwa kaburini siku nne. 18 Basi Bethania ulikuwa karibu na Yerusalemu umbali wa karibu maili mbili,* 19 na Wayahudi wengi walikuwa wamekuja kuwafariji Martha na Maria kwa ajili ya kufiwa na ndugu yao. 20 Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja, alitoka kwenda kumlaki, ila Maria alibaki nyumbani.
21 Martha akamwambia Yesu, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, ndugu yangu hangalikufa. 22 Lakini sasa ninajua kuwa chochote utakachomwomba Mungu, atakupa.”
23 Yesu akamwambia, “Ndugu yako atafufuka.”
24 Martha akamjibu, “Ninajua ya kuwa atafufuka wakati wa ufufuo wa wafu siku ya mwisho.”
25 Yesu akamwambia, “Mimi ndiye huo ufufuo na uzima. Yeye aniaminiye mimi, hata akifa atakuwa anaishi 26  na yeyote aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je, unasadiki haya?”
27 Martha akamwambia, “Ndiyo Bwana, ninaamini ya kuwa wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yeye ajaye ulimwenguni.”
Yesu Alia
28 Baada ya kusema haya Martha alikwenda, akamwita Maria dada yake faraghani na kumwambia, “Mwalimu yuko hapa anakuita.” 29 Maria aliposikia hivyo, akaondoka upesi akaenda mpaka alipokuwa Yesu. 30 Yesu alikuwa hajaingia kijijini, bali alikuwa bado yuko mahali pale alipokutana na Martha. 31 Wale Wayahudi waliokuwa pamoja na Maria nyumbani wakimfariji walipoona ameondoka haraka na kutoka nje, walimfuata wakidhani ya kwamba alikuwa anakwenda kule kaburini kulilia huko.
32 Maria alipofika mahali pale Yesu alipokuwa, alipiga magoti miguuni Pake na kusema, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, ndugu yangu hangalikufa.”
33 Yesu alipomwona Maria akilia na wale Wayahudi waliokuja pamoja naye pia wakilia, Yesu alisikia uchungu moyoni, akafadhaika sana. 34 Akauliza, “Mmemweka wapi?”
Wakamwambia, “Bwana, njoo upaone.”
35 Yesu akalia machozi.
36 Ndipo Wayahudi wakasema, “Tazama jinsi alivyompenda Lazaro!”
37 Lakini wengine wakasema, “Je, yule aliyefungua macho ya kipofu, hakuweza kumfanya na huyu asife?”
Yesu Amfufua Lazaro
38 Yesu kwa mara nyingine akiwa amefadhaika sana, akafika penye kaburi. Hilo kaburi lilikuwa pango ambalo jiwe lilikuwa limewekwa kwenye ingilio lake. 39 Yesu akasema, “Liondoeni hilo jiwe.”
Martha ndugu yake yule aliyekuwa amekufa akasema, “Lakini Bwana, wakati huu atakuwa ananuka kwani amekwisha kuwa kaburini siku nne.”
40 Yesu akamwambia, “Sikukuambia kwamba kama ukiamini utauona utukufu wa Mungu?”
41 Kwa hiyo wakaliondoa lile jiwe kutoka kaburini. Yesu akainua macho yake juu akasema, “Baba, ninakushukuru kwa kuwa wanisikia. 42  Ninajua ya kuwa wewe hunisikia siku zote, lakini nimesema haya kwa ajili ya umati huu uliosimama hapa, ili wapate kuamini ya kuwa wewe umenituma.”
43 Baada ya kusema haya, Yesu akapaza sauti yake akaita, “Lazaro, njoo huku!” 44 Yule aliyekuwa amekufa akatoka nje, mikono yake na miguu yake ikiwa imeviringishiwa vitambaa vya kitani na leso usoni pake.
Yesu akawaambia, “Mfungueni, mwacheni aende zake.”
Shauri La Kumuua Yesu
(Mathayo 26:1-5; Marko 14:1-2; Luka 22:1-2)
45 Hivyo Wayahudi wengi waliokuwa wamekuja kumfariji Maria, walipoona yale Yesu aliyoyatenda wakamwamini. 46 Lakini baadhi yao wakaenda kwa Mafarisayo na kuwaambia mambo Yesu aliyoyafanya. 47 Kwa hiyo viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakaita mkutano wa baraza.
Wakaulizana, “Tufanyeje? Huyu mtu anafanya ishara nyingi. 48 Kama tukimwacha aendelee hivi, kila mtu atamwamini, nao Warumi watakuja na kupaharibu mahali petu patakatifu na taifa letu.”
49 Mmoja wao aliyeitwa Kayafa, ambaye alikuwa kuhani mkuu mwaka huo, akasema, “Ninyi hamjui kitu chochote! 50 Hamjui kwamba ni afadhali mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, kuliko taifa lote liangamie?”
51 Hakusema haya kutokana na mawazo yake mwenyewe bali kama kuhani mkuu mwaka huo, alitabiri kuwa Yesu angelikufa kwa ajili ya taifa la Wayahudi, 52 wala si kwa ajili ya taifa hilo pekee, bali pia kwa ajili ya watoto wa Mungu waliotawanyika, ili kuwaleta pamoja na kuwafanya wawe wamoja. 53 Hivyo tangu siku hiyo wakawa wanafanya mipango ili wamuue Yesu.
54 Kwa hiyo Yesu akawa hatembei hadharani miongoni mwa Wayahudi, bali alijitenga akaenda sehemu iliyo karibu na jangwa kwenye kijiji kiitwacho Efraimu. Akakaa huko na wanafunzi wake.
55 Basi Pasaka ya Wayahudi ilipokuwa imekaribia, watu wengi walitoka vijijini wakaenda Yerusalemu kabla ya Pasaka ili wakajitakase. 56 Watu wakawa wanamtafuta Yesu, nao waliposimama kwenye eneo la Hekalu waliulizana, Je, mtu huyu hatakuja kamwe kwenye Sikukuu? 57 Viongozi wa makuhani na Mafarisayo walikuwa wametoa amri kuwa yeyote atakayejua mahali Yesu aliko, lazima atoe taarifa ili wapate kumkamata.
* 11:18 Maili mbili ni kama kilomita tatu. 11:27 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta.