13
Mkanda Wa Kitani
Hili ndilo Bwana aliloniambia: “Nenda ununue mkanda wa kitani, ujivike kiunoni mwako, lakini usiuache uguse maji.” Kwa hiyo nikanunua mkanda, kama Bwana alivyoniagiza, nikajivika kiunoni.
Ndipo neno la Bwana likanijia kwa mara ya pili: “Chukua mkanda ulionunua ambao umeuvaa kiunoni mwako, uende sasa Frati uufiche ndani ya ufa mdogo kwenye mwamba.” Ndipo nikaenda na kuuficha ule mkanda huko Frati, kama Bwana alivyoniamuru.
Baada ya siku nyingi Bwana akaniambia, “Nenda sasa Frati ukauchukue ule mkanda niliokuambia uufiche huko.” Hivyo nikaenda Frati na kuuchimbua ule mkanda kutoka pale nilipokuwa nimeuficha, lakini sasa ulikuwa umeharibika na haufai tena kabisa.
Ndipo neno la Bwana likanijia: “Hili ndilo Bwana asemalo: ‘Vivyo hivyo ndivyo nitakavyokiharibu kiburi cha Yuda na kiburi kikuu cha Yerusalemu. 10 Watu hawa waovu, wanaokataa kusikiliza maneno yangu, wafuatao ukaidi wa mioyo yao na kufuata miungu mingine kuitumikia na kuiabudu, watakuwa kama mkanda huu ambao haufai kabisa! 11 Kwa maana kama vile mkanda ufungwavyo kiunoni mwa mtu, ndivyo nilivyojifunga nyumba yote ya Israeli na nyumba yote ya Yuda,’ asema Bwana, ‘ili wawe watu wangu kwa ajili ya utukufu wangu, sifa na heshima yangu. Lakini hawajasikiliza.’
Viriba Vya Mvinyo
12 “Waambie: ‘Hili ndilo Bwana, Mungu wa Israeli, asemalo: kila kiriba inapasa kijazwe mvinyo.’ Kama wao wakikuambia, ‘Kwani hatujui kwamba kila kiriba inapasa kijazwe mvinyo?’ 13 Kisha uwaambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: nitawajaza ulevi wote waishio katika nchi hii, pamoja na wafalme waketio juu ya kiti cha enzi cha Daudi, makuhani, manabii na wale wote waishio Yerusalemu. 14 Nitawagonganisha kila mmoja na mwenzake, baba na wana wao, asema Bwana. Sitawarehemu wala kuwahurumia ili niache kuwaangamiza.’ ”
Tishio La Kutekwa
15 Sikieni na mzingatie,
msiwe na kiburi,
kwa kuwa Bwana amenena.
16 Mpeni utukufu Bwana Mungu wenu,
kabla hajaleta giza,
kabla miguu yenu haijajikwaa
juu ya vilima vitakavyotiwa giza.
Mlitarajia nuru,
lakini ataifanya kuwa giza nene
na kuibadili kuwa huzuni kubwa.
17 Lakini kama hamtasikiliza,
nitalia sirini
kwa ajili ya kiburi chenu;
macho yangu yatalia kwa uchungu,
yakitiririka machozi,
kwa sababu kundi la kondoo la Bwana
litachukuliwa mateka.
 
18 Mwambie mfalme na mamaye,
“Shukeni kutoka kwenye viti vyenu vya enzi,
kwa kuwa taji zenu za utukufu
zitaanguka kutoka vichwani mwenu.”
19 Miji iliyoko Negebu itafungwa,
wala hapatakuwa na mtu wa kuifungua.
Watu wa Yuda wote watapelekwa uhamishoni,
wakichukuliwa kabisa waende mbali.
 
20 Inua macho yako uone
wale wanaokuja kutoka kaskazini.
Liko wapi lile kundi ulilokabidhiwa,
kondoo wale uliojivunia?
21 Utasema nini Bwana atakapowaweka juu yako
wale ulioungana nao kama marafiki wako maalum?
Je, hutapatwa na utungu kama mwanamke
aliye katika utungu wa kuzaa?
22 Nawe kama ukijiuliza,
“Kwa nini haya yamenitokea?”
Ni kwa sababu ya dhambi zako nyingi
ndipo marinda yako yameraruliwa
na mwili wako umetendewa vibaya.
23 Je, Mkushi aweza kubadili ngozi yake
au chui kubadili madoadoa yake?
Vivyo hivyo nawe huwezi kufanya mema
wewe uliyezoea kutenda mabaya.
 
24 “Nitawatawanya kama makapi
yapeperushwayo na upepo wa jangwani.
25 Hii ndiyo kura yako,
fungu nililokuamuria,”
asema Bwana,
“kwa sababu umenisahau mimi
na kuamini miungu ya uongo.
26 Nitayafunua marinda yako mpaka juu ya uso wako
ili aibu yako ionekane:
27 uzinzi wako na kulia kwako kama farasi kulikojaa tamaa,
ukahaba wako usio na aibu!
Nimeyaona matendo yako ya machukizo
juu ya vilima na mashambani.
Ole wako, ee Yerusalemu!
Utaendelea kuwa najisi mpaka lini?”