34
Onyo Kwa Sedekia
Wakati Nebukadneza mfalme wa Babeli na jeshi lake lote, pamoja na falme zote na mataifa katika himaya aliyotawala walipokuwa wakipigana dhidi ya Yerusalemu pamoja na miji yote inayoizunguka, neno hili lilimjia Yeremia kutoka kwa Bwana: “Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli, kusema: Nenda kwa Sedekia mfalme wa Yuda umwambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Ninakaribia kuutia mji huu mikononi mwa mfalme wa Babeli, naye atauteketeza kwa moto. Hutaweza kuepuka mkono wake, bali hakika utatekwa na kukabidhiwa kwake. Utamwona mfalme wa Babeli kwa macho yako mwenyewe, naye atazungumza nawe ana kwa ana. Nawe utakwenda Babeli.
“ ‘Lakini sikia ahadi ya Bwana, ee Sedekia mfalme wa Yuda. Hili ndilo asemalo Bwana kukuhusu: Hutakufa kwa upanga, utakufa kwa amani. Kama vile watu walivyowasha moto wa maziko kwa heshima ya baba zako, wafalme waliokutangulia, ndivyo watu watakavyowasha moto kwa heshima yako na kuomboleza, wakisema: “Ole, Ee Bwana!” Mimi mwenyewe ninaweka ahadi hii, asema Bwana.’ ”
Ndipo nabii Yeremia akamwambia Sedekia mfalme wa Yuda mambo haya yote huko Yerusalemu, wakati jeshi la mfalme wa Babeli lilipokuwa likipigana dhidi ya Yerusalemu na miji mingine ya Yuda ambayo bado ilikuwa imara, yaani Lakishi na Azeka. Hii ilikuwa miji pekee yenye ngome iliyobaki katika Yuda.
Uhuru Kwa Watumwa
Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Bwana, baada ya Mfalme Sedekia kufanya agano na watu wote huko Yerusalemu ili kutangaza uhuru kwa watumwa. Kila mmoja alipaswa kuwaacha huru watumwa wake wa Kiebrania, wanawake na wanaume. Hakuna yeyote aliyeruhusiwa kumshikilia Myahudi mwenzake kama mtumwa. 10 Kwa hiyo maafisa wote na watu walioingia katika agano hili wakakubali kwamba watawaacha huru watumwa wao wa kiume na wa kike, na hawatawashikilia tena kama watumwa. Wakakubali na wakawaacha huru. 11 Lakini baadaye wakabadili mawazo yao, na kuwarudisha wale watumwa waliokuwa wamewaacha huru, wakawafanya tena watumwa.
12 Ndipo neno la Bwana likamjia Yeremia kusema: 13 “Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: Nilifanya agano na baba zenu nilipowatoa Misri, kutoka nchi ya utumwa. Nilisema, 14 ‘Kila mwaka wa saba, kila mmoja wenu ni lazima amwache huru mtumwa ambaye ni Mwebrania mwenzenu aliyejiuza kwenu. Baada ya kukutumikia kwa miaka sita, ni lazima umwache huru aende zake.’ Hata hivyo baba zenu hawakunisikiliza wala kunijali. 15 Hivi karibuni tu mlitubu na kufanya yaliyo sawa machoni pangu: Kila mmoja wenu aliwatangazia uhuru Waebrania wake. Hata mlifanya agano mbele zangu ndani ya nyumba iitwayo kwa Jina langu. 16 Lakini sasa mmegeuka na kulinajisi jina langu. Kila mmoja wenu amemrudisha mtumwa wa kiume na wa kike ambao mlikuwa mmewaacha huru waende zao walikotaka. Mmewalazimisha kuwa watumwa wenu tena.
17 “Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana: Hamkunitii mimi. Hamkutangaza uhuru kwa ndugu zenu. Hivyo sasa, ninawatangazia ninyi ‘uhuru,’ asema Bwana: ‘uhuru’ ili kuanguka kwa upanga, tauni na njaa. Nitawafanya mwe chukizo kwa falme zote za dunia. 18 Watu waliovunja agano langu, na ambao hawakutunza masharti ya agano walilofanya mbele zangu, nitawafanya kama ndama waliyemkata vipande viwili, kisha wakatembea kati ya vile vipande vya huyo ndama. 19 Viongozi wa Yuda na Yerusalemu, maafisa wa mahakama, makuhani na watu wote wa nchi waliopita kati ya vile vipande vya ndama, 20 nitawatia mikononi mwa adui zao wanaotafuta uhai wao. Maiti zao zitakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi.
21 “Nitamtia Sedekia mfalme wa Yuda na maafisa wake mikononi mwa adui zao wanaotafuta uhai wao, kwa jeshi la mfalme wa Babeli, lililokuwa limeondoka kwenu. 22 Nitatoa amri, asema Bwana, nami nitawarudisha tena katika mji huu. Watapigana dhidi yake, wautwae na kuuteketeza kwa moto. Nami nitaiangamiza miji ya Yuda hivyo pasiwe na yeyote atakayeweza kuishi humo.”