49
Ujumbe Kuhusu Amoni
Kuhusu Waamoni:
 
Hili ndilo asemalo Bwana:
“Je, Israeli hana wana?
Je, hana warithi?
Kwa nini basi Moleki amechukua milki ya Gadi?
Kwa nini watu wake wanaishi katika miji yake?
Lakini siku zinakuja,”
asema Bwana,
“nitakapopiga kelele ya vita
dhidi ya Raba mji wa Waamoni;
utakuwa kilima cha magofu,
navyo vijiji vinavyouzunguka
vitateketezwa kwa moto.
Kisha Israeli atawafukuza
wale waliomfukuza,”
asema Bwana.
“Lia kwa huzuni, ee Heshboni, kwa kuwa Ai umeangamizwa!
Pigeni kelele, enyi wakazi wa Raba!
Vaeni nguo za gunia na kuomboleza,
kimbieni hapa na pale ndani ya kuta,
kwa kuwa Moleki atakwenda uhamishoni,
yeye pamoja na makuhani na maafisa wake.
Kwa nini unajivunia mabonde yako,
kujivunia mabonde yako yaliyozaa sana?
Ee binti usiye mwaminifu, unayeutumainia utajiri wako na kusema,
‘Ni nani atakayenishambulia?’
Nitaleta hofu kuu juu yako
kutoka kwa wale wote wanaokuzunguka,”
asema Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote.
“Kila mmoja wenu ataondolewa,
wala hakuna hata mmoja atakayekusanya wakimbizi.
 
“Lakini hatimaye,
nitarudisha mateka wa Waamoni,”
asema Bwana.
Ujumbe Kuhusu Edomu
Kuhusu Edomu:
 
Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote:
“Je, hakuna tena hekima katika Temani?
Je, shauri limewapotea wenye busara?
Je, hekima yao imechakaa?
Geuka na ukimbie, jifiche katika mapango marefu kabisa,
wewe uishiye Dedani,
kwa kuwa nitaleta maafa juu ya Esau
wakati nitakapomwadhibu.
Je, kama wachuma zabibu wangekuja kwako,
wasingebakiza zabibu chache?
Kama wezi wangekujia usiku,
je, si wangeiba tu kiasi ambacho wangehitaji?
10 Lakini nitamvua Esau nguo abaki uchi,
nitayafunua maficho yake,
ili asiweze kujificha.
Watoto wake, jamaa na majirani wataangamia,
naye hatakuwepo tena.
11 Waache yatima wako; nitayalinda maisha yao.
Wajane wako pia
wanaweza kunitumaini mimi.”
12 Hili ndilo asemalo Bwana: “Kama wale wasiostahili kukinywea kikombe ni lazima wakinywe, kwa nini wewe usiadhibiwe? Hutakwepa kuadhibiwa, ni lazima ukinywe. 13 Ninaapa kwa nafsi yangu,” asema Bwana, “kwamba Bosra utakuwa magofu na kitu cha kutisha, cha aibu na cha kulaania; miji yake yote itakuwa magofu milele.”
14 Nimesikia ujumbe kutoka kwa Bwana:
Mjumbe alitumwa kwa mataifa kusema,
“Jikusanyeni ili kuushambulia!
Inukeni kwa ajili ya vita!”
 
15 “Sasa nitakufanya uwe mdogo miongoni mwa mataifa,
aliyedharauliwa miongoni mwa watu.
16 Vitisho vyako na kiburi cha moyo wako
vimekudanganya,
wewe unayeishi katika majabali ya miamba,
wewe unayedumu katika miinuko ya kilima.
Ujapojenga kiota chako juu sana kama cha tai,
nitakushusha chini kutoka huko,”
asema Bwana.
17 “Edomu atakuwa kitu cha kuogofya;
wote wapitao karibu
watashangaa na kuzomea
kwa sababu ya majeraha yake yote.
18 Kama vile Sodoma na Gomora zilivyoangamizwa,
pamoja na miji iliyokuwa jirani nayo,”
asema Bwana,
“vivyo hivyo hakuna mtu yeyote atakayeishi humo.
Naam, hakuna mtu yeyote atakayekaa humo.
 
19 “Kama simba anayepanda kutoka vichaka vya Yordani
kuja kwenye nchi ya malisho mengi,
ndivyo nitamfukuza Edomu kutoka nchi yake ghafula.
Ni nani aliye mteule nitakayemweka kwa ajili ya jambo hili?
Ni nani aliye kama mimi,
na ni nani awezaye kunipinga?
Tena ni mchungaji yupi awezaye
kusimama kinyume nami?”
20 Kwa hiyo, sikia kile Bwana alichokipanga dhidi ya Edomu,
kile alichokusudia dhidi ya wale waishio Temani:
Aliye mchanga katika kundi ataburutwa mbali;
yeye ataharibu kabisa malisho yao kwa sababu yao.
21 Kwa sauti ya anguko lao, dunia itatetemeka.
Kilio chao kitasikika hadi Bahari ya Shamu.*
22 Tazama! Tai atapaa juu angani na kuruka chini kwa ghafula,
akitandaza mabawa yake juu ya Bosra.
Katika siku hiyo, mioyo ya mashujaa wa Edomu
itakuwa kama moyo wa mwanamke katika utungu wa kuzaa.
Ujumbe Kuhusu Dameski
23 Kuhusu Dameski:
“Hamathi na Arpadi imetahayarika,
kwa kuwa wamesikia habari mbaya.
Wamevunjika moyo na wametaabika
kama bahari iliyochafuka.
24 Dameski amedhoofika,
amegeuka na kukimbia,
hofu ya ghafula imemkamata sana;
amepatwa na uchungu na maumivu,
maumivu kama ya mwanamke katika utungu wa kuzaa.
25 Kwa nini mji ambao unajulikana haujaachwa,
mji ambao ninaupenda?
26 Hakika, vijana wake wanaume wataanguka barabarani;
askari wake wote watanyamazishwa siku hiyo,”
asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.
27 “Nitatia moto kuta za Dameski;
utaangamiza ngome za Ben-Hadadi.”
Ujumbe Kuhusu Kedari Na Hazori
28 Kuhusu Kedari na falme za Hazori, ambazo Nebukadneza mfalme wa Babeli alizishambulia:
 
Hili ndilo asemalo Bwana:
“Inuka, ushambulie Kedari
na kuwaangamiza watu wa mashariki.
29 Hema zao na makundi yao ya kondoo yatachukuliwa;
vibanda vyao vitatwaliwa
pamoja na mali zao zote na ngamia zao.
Watu watawapigia kelele,
‘Hofu kuu iko kila upande!’
 
30 “Kimbieni haraka!
Kaeni kwenye mapango marefu sana, ninyi mkaao Hazori,”
asema Bwana.
“Nebukadneza, mfalme wa Babeli amepanga shauri baya dhidi yenu;
amebuni hila dhidi yenu.
 
31 “Inuka na ulishambulie taifa lililo starehe,
linaloishi kwa kujiamini,”
asema Bwana,
“taifa lisilo na malango wala makomeo;
watu wake huishi peke yao.
32 Ngamia wao watakuwa nyara,
nayo makundi yao makubwa ya ngʼombe yatatekwa.
Wale walio maeneo ya mbali
nitawatawanya pande zote,
nami nitaleta maafa juu yao
kutoka kila upande,”
asema Bwana.
33 “Hazori itakuwa makao ya mbweha,
mahali pa ukiwa milele.
Hakuna yeyote atakayeishi humo;
hakuna mtu atakayekaa ndani yake.”
Ujumbe Kuhusu Elamu
34 Hili ndilo neno la Bwana lililomjia nabii Yeremia kuhusu Elamu, mapema katika utawala wa Sedekia mfalme wa Yuda:
 
35 Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo:
“Tazama, nitavunja upinde wa Elamu,
ulio tegemeo la nguvu zao.
36 Nitaleta pepo nne dhidi ya Elamu
toka pande nne za mbingu,
nitawatawanya katika hizo pande nne,
wala hapatakuwa na taifa
ambalo watu wa Elamu waliofukuzwa
hawatakwenda.
37 Nitamfadhaisha Elamu mbele ya adui zao,
mbele yao wale wanaotafuta uhai wao;
nitaleta maafa juu yao,
naam, hasira yangu kali,”
asema Bwana.
“Nitawafuatia kwa upanga
mpaka nitakapowamaliza.
38 Nitaweka kiti changu cha enzi huko Elamu
na kumwangamiza mfalme wake na maafisa wake,”
asema Bwana.
 
39 “Lakini nitarudisha mateka wa Elamu
katika siku zijazo,”
asema Bwana.
* 49:21 Kwa Kiebrania ni Bahari ya Mafunjo.