5
Basi wafalme wote wa Waamori magharibi ya Yordani na wafalme wote wa Kanaani waliokuwa kwenye pwani waliposikia jinsi Bwana alivyoukausha Mto Yordani mbele ya Waisraeli hata tulipokwisha kuvuka, mioyo yao ikayeyuka kwa hofu, wala hawakuwa na ujasiri kuwakabili Waisraeli.
Tohara Huko Gilgali
Wakati huo Bwana akamwambia Yoshua, “Tengeneza visu vya mawe magumu sana na uwatahiri Waisraeli tena.” Kwa hiyo Yoshua akatengeneza visu vya mawe magumu sana na kutahiri Waisraeli huko Gibeath-Haaralothi.*
Hii ndiyo sababu ya Yoshua kufanya hivyo: Wanaume wote waliotoka Misri, wote wenye umri wa kwenda vitani, walikufa jangwani wakiwa njiani baada ya kuondoka Misri. Watu wote waliotoka Misri walikuwa wametahiriwa, lakini watu wote waliozaliwa jangwani wakiwa safarini toka Misri walikuwa hawajatahiriwa. Waisraeli walitembea jangwani miaka arobaini mpaka wanaume wote wale waliokuwa na umri wa kwenda vitani wakati waliondoka Misri walipokwisha kufa, kwa kuwa hawakumtii Bwana. Kwa maana Bwana alikuwa amewaapia kuwa wasingeweza kuona nchi ambayo alikuwa amewaahidi baba zao katika kuapa kutupatia, nchi inayotiririka maziwa na asali. Kwa hiyo akawainua wana wao baada yao na hawa ndio hao ambao Yoshua aliwatahiri. Walikuwa hawajatahiriwa bado kwa sababu walikuwa safarini. Baada ya taifa lote kutahiriwa, waliendelea kukaa kambini mpaka walipokuwa wamepona.
Bwana akamwambia Yoshua, “Leo nimeiondoa aibu ya Wamisri kutoka kwenu.” Basi mahali pale pakaitwa Gilgali hadi leo.
10 Jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi, wakiwa kambini huko Gilgali katika tambarare za Yeriko, Waisraeli wakaadhimisha Pasaka. 11 Siku iliyofuata Pasaka, katika siku ile ile, wakala mazao ya nchi, mikate isiyotiwa chachu na nafaka za kukaanga. 12 Mana ilikoma siku iliyofuata baada ya Waisraeli kula chakula kilichotoka katika nchi; hapakuwa na mana tena kwa ajili ya Waisraeli, ila mwaka huo walikula mazao ya nchi ya Kanaani.
Jemadari Wa Jeshi La Bwana
13 Basi wakati Yoshua alipokuwa karibu na Yeriko, akainua macho, akaona mtu aliyesimama mbele yake, akiwa na upanga mkononi uliofutwa kwenye ala. Yoshua akamwendea na kumuuliza, “Je, wewe uko upande wetu au upande wa adui zetu?”
14 Akajibu, “La, siko upande wowote, lakini mimi nimekuja nikiwa jemadari wa jeshi la Bwana.” Yoshua akaanguka kifudifudi hadi chini, akasujudu, akamuuliza, “Je, Bwana, una ujumbe gani kwa mtumishi wako?” 15 Jemadari wa jeshi la Bwana akajibu, “Vua viatu vyako, kwa maana mahali hapa unaposimama ni patakatifu.” Naye Yoshua akafanya hivyo.
* 5:3 Gibeath-Haaralothi maana yake ni Kilima cha Magovi.