18
Eliya Na Obadia
Baada ya muda mrefu, katika mwaka wa tatu, neno la Bwana likamjia Eliya kusema, “Nenda ukajionyeshe kwa Ahabu na mimi nitanyesha mvua juu ya nchi.” Kwa hiyo Eliya akaenda kujionyesha kwa Ahabu.
Wakati huu njaa ilikuwa kali sana katika Samaria, naye Ahabu alikuwa amemwita Obadia ambaye alikuwa msimamizi wa jumba lake la kifalme. (Obadia alimcha Bwana sana. Wakati Yezebeli alipokuwa akiwaua manabii wa Bwana, Obadia alikuwa amewachukua manabii mia moja na kuwaficha katika mapango mawili, hamsini kwenye kila moja na akawa akiwapa chakula na maji.) Ahabu alikuwa amemwambia Obadia, “Nenda katika nchi yote kwenye vijito vyote na mabonde. Huenda tunaweza kupata majani ya kuwalisha farasi na nyumbu wapate kuishi ili tusilazimike kuwaua hata mmoja wa wanyama wetu.” Kwa hiyo wakagawanya nchi waliyokusudia kutafuta majani, Ahabu akaenda upande mmoja na Obadia upande mwingine.
Wakati Obadia alipokuwa akitembea njiani, Eliya akakutana naye. Obadia akamtambua, akamsujudia hadi nchi na kusema, “Je, hivi kweli ni wewe, bwana wangu Eliya?”
Eliya akamjibu, “Ndiyo, nenda ukamwambie bwana wako Ahabu, ‘Eliya yuko hapa.’ ”
Obadia akamuuliza, “Ni kosa gani nimefanya, hata ukaamua kumkabidhi mtumishi wako mkononi mwa Ahabu ili aniue? 10 Hakika kama Bwana Mungu wako aishivyo, hakuna taifa hata moja au ufalme ambapo bwana wangu hajamtuma mtu kukutafuta. Kila wakati taifa au ufalme walipodai kwamba haupo huko, aliwafanya waape kwamba hawakuweza kukupata. 11 Lakini sasa unaniambia niende kwa bwana wangu na kusema, ‘Eliya yuko hapa.’ 12 Sijui ni wapi Roho wa Bwana ataamua kukupeleka wakati nitakapokuacha. Kama nikienda kumwambia Ahabu na asikupate, ataniua. Hata hivyo mimi mtumishi wako nimemwabudu Bwana tangu ujana wangu. 13 Je, hukusikia, bwana wangu, nilifanya nini wakati Yezebeli alipokuwa akiua manabii wa Bwana? Niliwaficha manabii wa Bwana mia moja katika mapango mawili, hamsini katika kila moja, nami nikawapatia chakula na maji. 14 Nawe sasa unaniambia niende kwa bwana wangu na kumwambia, ‘Eliya yuko hapa.’ Yeye ataniua!”
15 Eliya akasema, “Kama Bwana Mwenye Nguvu Zote aishivyo, yeye ninayemtumikia, hakika nitajionyesha kwa Ahabu leo.”
Eliya Juu Ya Mlima Karmeli
16 Basi Obadia akaenda kukutana na Ahabu na kumwambia, naye Ahabu akaenda kukutana na Eliya. 17 Ahabu alipomwona Eliya, akamwambia, “Je, ni wewe, mtaabishaji wa Israeli?”
18 Eliya akamjibu, “Mimi sijaitaabisha Israeli. Lakini wewe na jamaa ya baba yako ndio mnaofanya hivyo. Mmeziacha amri za Bwana na mkafuata Mabaali. 19 Sasa waite watu kutoka Israeli yote tukutane nao juu ya Mlima Karmeli. Nawe uwalete hao manabii wa Baali mia nne na hamsini na hao manabii mia nne wa Ashera, walao chakula mezani mwa Yezebeli.”
20 Ndipo Ahabu akatuma ujumbe katika Israeli yote na kuwakusanya manabii hao juu ya mlima Karmeli. 21 Eliya akasimama mbele ya watu na kusema, “Mtasitasita katika mawazo mawili hadi lini? Ikiwa Bwana ndiye Mungu, mfuateni yeye; lakini ikiwa Baali ni Mungu, basi mfuateni yeye.”
Lakini watu hawakusema kitu.
22 Kisha Eliya akawaambia, “Ni mimi peke yangu nabii wa Bwana aliyebaki, lakini Baali ana manabii mia nne na hamsini. 23 Leteni mafahali wawili. Wao na wajichagulie mmoja, wamkate vipande vipande na waweke juu ya kuni lakini wasiiwashie moto. Nitamwandaa huyo fahali mwingine na kumweka juu ya kuni lakini sitawasha moto. 24 Kisha mliitie jina la mungu wenu, nami nitaliitia jina la Bwana Mungu yule ambaye atajibu kwa moto, huyo ndiye Mungu.”
Kisha watu wote wakasema, “Hilo unalosema ni jema.”
25 Eliya akawaambia manabii wa Baali, “Chagueni mmoja kati ya hawa mafahali na mwe wa kwanza kumwandaa, kwa kuwa ninyi mko wengi sana. Liitieni jina la mungu wenu, lakini msiwashe moto.” 26 Kwa hiyo wakamchukua yule fahali waliyepewa, nao wakamwandaa.
Kisha wakaliitia jina la Baali kutoka asubuhi hadi adhuhuri, wakapiga kelele, “Ee Baali, utujibu!” Lakini hapakuwa na jibu; hakuna aliyejibu. Nao wakacheza kuizunguka madhabahu waliyoijenga.
27 Wakati wa adhuhuri, Eliya akaanza kuwadhihaki, akisema, “Pigeni kelele zaidi! Hakika yeye ni mungu! Labda amezama katika mawazo mazito, au ana shughuli nyingi, au amesafiri. Labda amelala usingizi mzito, naye ni lazima aamshwe.” 28 Kwa hiyo wakapiga kelele zaidi na kama ilivyokuwa desturi yao wakajichanja wenyewe kwa visu na vyembe, mpaka damu ikachuruzika. 29 Adhuhuri ikapita, nao wakaendelea na utabiri wao wa kiwazimu mpaka wakati wa dhabihu ya jioni. Lakini hapakuwa na jibu, hakuna aliyejibu, hakuna aliyeangalia.
30 Kisha Eliya akawaambia watu wote, “Sogeeni karibu nami.” Watu wote wakamkaribia, naye akakarabati madhabahu ya Bwana, ambayo ilikuwa imevunjwa. 31 Eliya akachukua mawe kumi na mawili, moja kwa ajili ya kila kabila la wana wa Yakobo, ambaye neno la Bwana lilimjia, likisema, “Jina lako litakuwa Israeli.” 32 Kwa mawe hayo, akajenga madhabahu katika jina la Bwana, na akachimba handaki kuizunguka, ukubwa wa kutosha vipimo viwili vya mbegu. 33 Akapanga kuni, akamkata yule fahali vipande vipande na kuvipanga juu ya kuni. Kisha akawaambia, “Jazeni mapipa manne maji na kuyamwaga juu ya sadaka ya kuteketezwa na juu ya kuni.”
34 Akawaambia, “Fanyeni hivyo tena.” Nao wakafanya hivyo tena.
Akaagiza, “Fanyeni kwa mara ya tatu.” Nao wakafanya hivyo kwa mara ya tatu. 35 Maji yakatiririka kuizunguka madhabahu na hata kujaza lile handaki.
36 Wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, nabii Eliya akasogea mbele na kuomba, akisema: “Ee Bwana, Mungu wa Abrahamu, na Isaki na Israeli, ijulikane leo kwamba wewe ndiye Mungu katika Israeli na ya kwamba mimi ni mtumishi wako na nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. 37 Unijibu mimi, Ee Bwana, nijibu mimi, ili watu hawa wajue kwamba wewe, Ee Bwana, ndiwe Mungu, na kwamba unaigeuza mioyo yao ikurudie tena.”
38 Kisha moto wa Bwana ukashuka na kuiteketeza ile dhabihu, zile kuni, yale mawe, ule udongo, na pia kuramba yale maji yaliyokuwa ndani ya handaki.
39 Wakati watu wote walipoona hili, wakaanguka kifudifudi na kulia, “Bwana: yeye ndiye Mungu! Bwana: yeye ndiye Mungu!”
40 Kisha Eliya akawaamuru, “Wakamateni hao manabii wa Baali. Msimwache hata mmoja atoroke!” Wakawakamata, naye Eliya akawaleta mpaka Bonde la Kishoni na kuwachinja huko.
41 Eliya akamwambia Ahabu, “Nenda, ukale na kunywa, kwa kuwa kuna sauti ya mvua kubwa.” 42 Hivyo Ahabu akaondoka ili kula na kunywa. Lakini Eliya akapanda kileleni mwa Karmeli, akasujudu na akaweka kichwa chake katikati ya magoti yake.
43 Akamwambia mtumishi wake, “Nenda ukatazame kuelekea bahari.” Akaenda na kutazama.
Akasema, “Hakuna kitu chochote huko.”
Mara saba Eliya akasema, “Nenda tena.”
44 Mara ya saba, mtumishi akaleta taarifa, “Wingu dogo kama mkono wa mwanadamu linainuka kutoka baharini.”
Hivyo Eliya akasema, “Nenda ukamwambie Ahabu, ‘Tandika gari lako na ushuke kabla mvua haijakuzuia.’ ”
45 Wakati ule ule anga likawa jeusi kwa mawingu, upepo ukainuka na mvua kubwa ikanyesha, naye Ahabu akaenda zake Yezreeli. 46 Nguvu za Bwana zikamjia Eliya, naye akajikaza viuno, akakimbia mbele ya Ahabu njia yote hadi maingilio ya Yezreeli.