20
Ugonjwa Wa Hezekia
(2 Nyakati 32:24-26; Isaya 38:1-8, 21-22)
Katika siku hizo, Hezekia akaugua, naye akawa karibu kufa. Nabii Isaya mwana wa Amozi akaenda kwake na kumwambia, “Hili ndilo asemalo Bwana: Tengeneza mambo ya nyumba yako, kwa sababu utakufa, hutapona.”
Hezekia akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana: “Ee Bwana, kumbuka jinsi nilivyoenenda mbele zako kwa uaminifu na kujitoa kwa moyo wangu wote, na kufanya yaliyo mema machoni pako.” Naye Hezekia akalia kwa uchungu.
Kabla Isaya hajaondoka katika ua wa kati, neno la Bwana likamjia, akaambiwa: “Rudi ukamwambie Hezekia, kiongozi wa watu wangu, ‘Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa baba yako Daudi: Nimeyasikia maombi yako na nimeona machozi yako; nitakuponya. Siku ya tatu kuanzia sasa utapanda kwenda Hekalu la Bwana. Nitakuongezea miaka kumi na mitano katika maisha yako. Nami nitakuokoa wewe pamoja na mji huu mkononi mwa mfalme wa Ashuru. Nitaulinda mji huu kwa ajili yangu, na kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi!’ ”
Kisha Isaya akasema, “Tengenezeni dawa ya kubandika ya tini.” Wakafanya hivyo na kuiweka kwenye jipu, naye akapona.
Hezekia alikuwa amemuuliza Isaya, “Kutakuwa na ishara gani kwamba Bwana ataniponya mimi, na kwamba nitapanda kwenda Hekalu la Bwana siku ya tatu tangu leo?”
Isaya akajibu, “Hii ndiyo ishara ya Bwana kwako kwamba Bwana atafanya kile alichoahidi: Je, kivuli kiende hatua kumi mbele, au kivuli kirudi nyuma hatua kumi?”
10 Hezekia akasema, “Ni jambo rahisi kwa kivuli kutangulia mbele hatua kumi, kuliko kukifanya kirudi nyuma hatua kumi.”
11 Ndipo nabii Isaya akamwita Bwana, naye Bwana akakifanya kivuli kurudi nyuma hatua kumi ambazo kilikuwa kimeshuka kwenye ngazi ya Ahazi.
Wajumbe Kutoka Babeli
(Isaya 39:1-8)
12 Wakati huo Merodaki-Baladani, mwana wa Baladani mfalme wa Babeli, akamtumia Hezekia barua na zawadi, kwa sababu alikuwa amesikia habari za kuugua kwa Hezekia. 13 Hezekia akawapokea wale wajumbe na kuwaonyesha vitu vyote vile vilivyokuwa katika ghala zake: yaani fedha, dhahabu, vikolezo na mafuta safi, ghala la silaha na kila kitu kilichokuwa katika hazina zake. Hapakuwa na kitu chochote katika jumba lake la kifalme au katika ufalme wake wote ambacho Hezekia hakuwaonyesha.
14 Ndipo nabii Isaya akaenda kwa Mfalme Hezekia na kumuuliza, “Watu hao walisema nini, na wametoka wapi?”
Hezekia akamjibu, “Wametoka nchi ya mbali. Walikuja kutoka Babeli.”
15 Nabii akauliza, “Waliona nini katika jumba lako la kifalme?”
Hezekia akajibu, “Waliona kila kitu katika jumba langu la kifalme. Hakuna kitu chochote katika hazina yangu ambacho sikuwaonyesha.”
16 Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno la Bwana: 17 Hakika wakati unakuja ambapo vitu vyote katika jumba lako la kifalme, na vyote ambavyo baba zako waliweka akiba mpaka siku hii, vitachukuliwa kwenda Babeli. Hakuna chochote kitakachosalia, asema Bwana. 18 Nao baadhi ya wazao wako, nyama yako na damu yako mwenyewe watakaozaliwa kwako, watachukuliwa mbali, nao watakuwa matowashi katika jumba la mfalme wa Babeli.”
19 Hezekia akamjibu Isaya, “Neno la Bwana ulilosema ni jema.” Kwa kuwa alifikiri, “Lakini si patakuwa na amani na usalama wakati wa uhai wangu?”
20 Matukio mengine ya utawala wa Hezekia, mafanikio yake yote, na jinsi alivyotengeneza bwawa na mfereji ambao ulileta maji katika mji, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? 21 Hezekia akafa, akazikwa pamoja na baba zake. Naye Manase mwanawe akawa mfalme baada yake.