Mambo Ya Walawi
1
Sadaka Ya Kuteketezwa
1 Bwana akamwita Mose na kusema naye kutoka kwenye Hema la Kukutania, akamwambia,
2 “Sema na Waisraeli na uwaambie, ‘Yeyote miongoni mwenu aletapo sadaka ya mnyama kwa Bwana, alete mnyama kama sadaka yake kutoka kundi lake la ngʼombe au la kondoo na mbuzi.
3 “ ‘Kama sadaka hiyo ni ya kuteketezwa kutoka kwenye kundi la ngʼombe, atamtoa ngʼombe dume asiye na dosari. Ni lazima amlete kwenye ingilio la Hema la Kukutania ili aweze kukubalika kwa Bwana.
4 Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha sadaka ya kuteketezwa, nayo itakubaliwa kwa niaba yake ili kufanya upatanisho kwa ajili yake.
5 Atamchinja yule fahali mchanga mbele za Bwana, kisha wana wa Aroni walio makuhani wataleta damu na kuinyunyiza pande zote za madhabahu yaliyo penye ingilio la Hema la Kukutania.
6 Ataichuna hiyo sadaka ya kuteketezwa na kuikata vipande vipande.
7 Wana wa Aroni kuhani wataweka moto juu ya madhabahu na kupanga kuni juu ya huo moto.
8 Kisha wana wa Aroni walio makuhani watapanga vile vipande vya nyama, pamoja na kichwa na mafuta ya huyo mnyama juu ya zile kuni zinazowaka juu ya madhabahu.
9 Ataziosha sehemu za ndani na miguu yake kwa maji, naye kuhani atavichoma vyote juu ya madhabahu. Hii ni sadaka ya kuteketezwa, sadaka iliyotolewa kwa moto, yenye harufu nzuri ya kumpendeza Bwana.
10 “ ‘Kama sadaka ni ya kuteketezwa kutoka kwenye kundi la kondoo au mbuzi, atamtoa mnyama dume asiye na dosari.
11 Atamchinjia upande wa kaskazini wa madhabahu mbele za Bwana, nao wana wa Aroni walio makuhani watanyunyizia damu yake pande zote za madhabahu.
12 Atamkata vipande vipande, naye kuhani atavipanga, pamoja na kichwa na mafuta ya mnyama juu ya zile kuni zinazowaka juu ya madhabahu.
13 Ataosha sehemu za ndani na miguu kwa maji, naye kuhani atavileta vyote na kuvichoma juu ya madhabahu. Hii ni sadaka ya kuteketezwa, sadaka iliyotolewa kwa moto, harufu nzuri ya kumpendeza Bwana.
14 “ ‘Kama sadaka ya kuteketezwa inayotolewa kwa Bwana ni ndege, atamtoa hua au kinda la njiwa.
15 Kuhani atamleta kwenye madhabahu, naye atamvunja shingo na kumnyofoa kichwa na kumchoma juu ya madhabahu. Damu yake itachuruzishwa ubavuni mwa madhabahu.
16 Ataondoa kifuko cha chakula pamoja na uchafu wake na kuvitupa upande wa mashariki wa madhabahu, mahali pale penye majivu.
17 Atampasua na kumweka wazi katika mabawa yake, lakini asimwachanishe kabisa, kisha kuhani ataichoma juu ya zile kuni zinazowaka juu ya madhabahu. Hii ni sadaka ya kuteketezwa, sadaka iliyotolewa kwa moto, harufu nzuri ya kumpendeza Bwana.