10
Kifo Cha Nadabu Na Abihu
Nadabu na Abihu, wana wa Aroni, wakachukua vyetezo vyao, wakaweka moto ndani yake na kuongeza uvumba; kisha wakamtolea Bwana moto usio halali, kinyume na agizo la Mungu. Hivyo moto ukaja kutoka kwa uwepo wa Bwana na kuwaramba, nao wakafa mbele za Bwana. Kisha Mose akamwambia Aroni, “Hili ndilo alilonena Bwana wakati aliposema:
“ ‘Miongoni mwa wale watakaonikaribia
nitajionyesha kuwa mtakatifu;
machoni pa watu wote
nitaheshimiwa.’ ”
Aroni akanyamaza.
Mose akawaita Mishaeli na Elisafani, wana wa Uzieli mjomba wake Aroni, akawaambia, “Njooni hapa. Ondoeni miili ya binamu zenu mbele ya mahali patakatifu, mkaipeleke nje ya kambi.” Hivyo wakaja na kuwaondoa, wakiwa bado wamevalia makoti yao ya ibada, wakawapeleka nje ya kambi, kama Mose alivyoamuru.
Ndipo Mose akamwambia Aroni pamoja na wanawe, Eleazari na Ithamari, “Msifunue vichwa vyenu wala msirarue mavazi yenu, la sivyo mtakufa na Bwana ataikasirikia jumuiya nzima. Lakini ndugu zenu, nyumba yote ya Israeli, wanaweza kuwaombolezea wale ambao Bwana amewaangamiza kwa moto. Msitoke nje ya ingilio la Hema la Kukutania, la sivyo mtakufa, kwa sababu mafuta ya Bwana ya upako yako juu yenu.” Hivyo wakafanya kama vile Mose alivyosema.
Kisha Bwana akamwambia Aroni, “Wewe na wanao msinywe mvinyo wala kinywaji kingine kilichochachuka wakati mwingiapo katika Hema la Kukutania, la sivyo mtakufa. Hili litakuwa Agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo. 10 Ni lazima mtenganishe kilicho kitakatifu na kile kilicho cha kawaida, kati ya yaliyo najisi na yaliyo safi, 11 na lazima mwafundishe Waisraeli amri zote ambazo Bwana aliwapa kupitia Mose.”
12 Mose akamwambia Aroni pamoja na wanawe waliosalia, Eleazari na Ithamari, “Chukueni sadaka ya nafaka iliyobaki kutoka sadaka zilizotolewa kwa Bwana kwa moto, muile hapo kando ya madhabahu ikiwa imeandaliwa bila chachu, kwa sababu ni takatifu sana. 13 Mtaila katika mahali patakatifu kwa sababu ni fungu lenu na fungu la wana wenu la sadaka zilizotolewa kwa Bwana kwa moto, kwa maana hivyo ndivyo nilivyoamriwa. 14 Lakini wewe na wanao na binti zako mwaweza kula kidari kile kilichoinuliwa na paja lile lililotolewa. Mtavila mahali safi pa kawaida ya ibada; mmepewa wewe na watoto wako kuwa fungu lenu la sadaka za amani za Waisraeli. 15 Paja lile lililotolewa na kidari kile kilichoinuliwa lazima viletwe pamoja na sehemu za mafuta ya sadaka za kuteketezwa kwa moto, ili kuinuliwa mbele za Bwana kama sadaka ya kuinuliwa. Hili litakuwa fungu lako la kawaida na wanao, kama Bwana alivyoagiza.”
16 Mose alipouliza kuhusu mbuzi atolewaye kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na kukuta kwamba ameteketezwa, aliwakasirikia Eleazari na Ithamari, wana wa Aroni waliobaki, akawauliza, 17 “Kwa nini hamkula sadaka ya dhambi katika eneo la mahali patakatifu? Ni takatifu sana. Mlipewa ninyi ili kuondoa hatia ya jumuiya kwa ajili ya kuwafanyia upatanisho mbele za Bwana. 18 Kwa kuwa damu yake haikuletwa ndani ya Mahali Patakatifu, mngemla mbuzi huyo katika sehemu ya mahali patakatifu kama nilivyoagiza.”
19 Aroni akamjibu Mose, “Leo wanangu wametoa sadaka zao za dhambi na sadaka zao za kuteketezwa mbele za Bwana, lakini mambo kama haya yamenitokea mimi. Je, Bwana angependezwa kama ningekuwa nimekula sadaka ya dhambi leo?” 20 Mose aliposikia haya, akaridhika.