12
Utakaso Baada Ya Kuzaa Mtoto
Bwana akamwambia Mose, “Waambie Waisraeli: ‘Mwanamke ambaye atapata mimba na kuzaa mtoto wa kiume atakuwa najisi kwa kawaida ya ibada kwa siku saba, kama anavyokuwa najisi wakati wa siku zake za hedhi. Mvulana atatahiriwa siku ya nane. Kisha ni lazima huyo mwanamke asubiri kwa siku thelathini na tatu, ndipo atakaswe kutoka damu kwake. Hataruhusiwa kugusa kitu chochote kilicho kitakatifu au kuingia mahali patakatifu, mpaka siku za kutakaswa kwake zimetimia. Kama akimzaa mtoto wa kike, mwanamke huyo atakuwa najisi kwa majuma mawili, kama wakati wake wa hedhi. Kisha atasubiri kwa siku sitini na sita, ndipo atatakaswa kutoka damu kwake.
“ ‘Siku zake za utakaso kwa ajili ya mwana au binti zitakapotimia, mwanamke huyo atamletea kuhani kwenye ingilio la Hema la Kukutania mwana-kondoo mwenye umri wa mwaka mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, na kinda la njiwa au hua kwa ajili ya sadaka ya dhambi. Atavitoa mbele za Bwana ili kufanya upatanisho kwa ajili yake, na kisha atakuwa safi kwa desturi ya ibada kutokana na kutokwa damu kwake.
“ ‘Haya ndiyo masharti kwa ajili ya mwanamke atakayezaa mtoto wa kiume au wa kike. Kama huyo mwanamke hana uwezo wa kumpata mwana-kondoo, ataleta hua wawili au makinda mawili ya njiwa, moja kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa na mwingine kwa ajili ya sadaka ya dhambi. Kwa njia hii, kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atakuwa safi.’ ”