15
Kutokwa Na Umajimaji Usababishao Unajisi
Bwana akawaambia Mose na Aroni, “Semeni na Waisraeli mwaambie: ‘Wakati mtu yeyote anapotokwa na usaha mwilini, usaha huo ni najisi. Iwe unaendelea kutiririka kutoka mwilini mwake au umeziba, utamfanya kuwa najisi. Hivi ndivyo usaha wake utakavyomletea unajisi:
“ ‘Kitanda chochote atakacholalia mtu mwenye kutokwa na usaha kitakuwa najisi, na chochote atakachokalia kitakuwa najisi. Yeyote atakayegusa kitanda chake ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi mpaka jioni. Yeyote atakayeketi juu ya kitu chochote alichokalia mwenye kutokwa na usaha, ni lazima afue nguo zake, na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi mpaka jioni.
“ ‘Yeyote atakayemgusa mtu mwenye kutokwa na usaha, ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi mpaka jioni.
“ ‘Ikiwa mtu mwenye kutokwa na usaha atamtemea mate mtu yeyote ambaye ni safi, mtu huyo ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi mpaka jioni.
“ ‘Kila tandiko ambalo mtu huyo atalikalia wakati wa kupanda mnyama litakuwa najisi, 10 na yeyote atakayegusa kitu chochote alichokuwa amekalia atakuwa najisi mpaka jioni. Yeyote atakayeinua vitu hivyo ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi mpaka jioni.
11 “ ‘Yeyote atakayeguswa na mtu anayetokwa na usaha bila kunawa mikono yake kwa maji, ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi mpaka jioni.
12 “ ‘Chungu cha udongo kitakachoguswa na mtu huyo ni lazima kivunjwe, na kifaa chochote cha mbao kitaoshwa kwa maji.
13 “ ‘Wakati mtu atakapotakasika kutoka usaha wake, anapaswa kuhesabu siku saba kwa utakaso wake. Ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji safi, naye atatakasika. 14 Siku ya nane, atachukua hua wawili au makinda mawili ya njiwa, aje mbele za Bwana kwenye ingilio la Hema la Kukutania, na kumpa kuhani. 15 Kuhani atavitoa dhabihu, mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi na huyo mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. Kwa njia hii atafanya upatanisho mbele za Bwana kwa ajili ya huyo mtu kwa sababu ya kutokwa usaha kwake.
16 “ ‘Wakati mtu akitokwa na shahawa, ni lazima aoge mwili mzima kwa maji, na atakuwa najisi mpaka jioni. 17 Vazi lolote ama ngozi yoyote yenye shahawa juu yake ni lazima ioshwe kwa maji, na itakuwa najisi mpaka jioni. 18 Ikiwa mtu atalala na mwanamke, na kukawa na kutoka kwa shahawa, ni lazima wote waoge kwa maji, nao watakuwa najisi mpaka jioni.
19 “ ‘Ikiwa mwanamke atatokwa na damu ya kawaida ya mwezi, atakuwa najisi kwa siku saba, na yeyote atakayemgusa atakuwa najisi mpaka jioni.
20 “ ‘Chochote atakacholalia wakati wake wa hedhi kitakuwa najisi, na chochote atakachokikalia kitakuwa najisi. 21 Yeyote atakayegusa kitanda chake ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi mpaka jioni. 22 Yeyote atakayegusa chochote atakachokalia ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi mpaka jioni. 23 Kiwe ni kitanda ama chochote alichokuwa amekikalia, ikiwa mtu yeyote atakigusa, atakuwa najisi mpaka jioni.
24 “ ‘Ikiwa mwanaume atalala naye na ile damu ya mwezi ikamgusa, atakuwa najisi kwa siku saba; kitanda chochote atakachokilalia huyo mwanaume kitakuwa najisi.
25 “ ‘Ikiwa mwanamke atatokwa na damu kwa siku nyingi zaidi ya siku zake za mwezi, au amekuwa na damu inayoendelea zaidi ya kipindi chake, atakuwa najisi kwa kipindi chote cha shida hiyo, kama ilivyokuwa katika siku za hedhi yake. 26 Kitanda chochote atakachokilalia huyo mwanamke wakati anaendelea kutokwa na damu kitakuwa najisi, kama kilivyokuwa kitanda chake wakati wa siku zake za hedhi, na chochote atakachokalia kitakuwa najisi, kama wakati wake wa hedhi. 27 Yeyote agusaye vitu hivyo atakuwa najisi; ni lazima afue nguo zake na kuoga kwa maji, naye atakuwa najisi mpaka jioni.
28 “ ‘Wakati atakapotakasika kutoka hedhi yake, ni lazima ahesabu siku saba, na baada ya hapo atakuwa safi kwa kawaida ya ibada. 29 Siku ya nane ni lazima achukue hua wawili au makinda mawili ya njiwa, na kumletea kuhani kwenye mlango wa Hema la Kukutania. 30 Kuhani atatoa dhabihu, mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na huyo mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. Kwa njia hii, atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana kwa sababu ya unajisi wa kutokwa damu kwake.
31 “ ‘Ni lazima uwatenge Waisraeli kutokana na vitu ambavyo vinawafanya najisi, ili wasife katika unajisi wao kwa kunajisi makao yangu,* ambayo yapo katikati yao.’ ”
32 Haya ni masharti kwa ajili ya mtu mwenye kutokwa na usaha, kwa ajili ya yeyote atakayetokwa na shahawa, 33 kwa ajili ya mwanamke katika siku zake za hedhi, kwa ajili ya mwanaume au mwanamke atokwaye na usaha, na kwa ajili ya mwanaume alalaye na mwanamke ambaye ni najisi kwa kawaida ya ibada.
* 15:31 Yaani maskani ya Mungu.