19
Sheria Mbalimbali
Bwana akamwambia Mose, “Sema na kusanyiko lote la Israeli na uwaambie: ‘Kuweni watakatifu, kwa kuwa mimi, Bwana Mungu wenu, ni mtakatifu.
“ ‘Kila mmoja wenu ni lazima amheshimu mama yake na baba yake, na pia ni lazima kuzishika Sabato zangu. Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.
“ ‘Msiabudu sanamu, wala msijitengenezee miungu ya shaba. Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.
“ ‘Mnapotoa dhabihu ya sadaka ya amani kwa Bwana, toeni kwa namna ambayo itakubaliwa kwa niaba yenu. Sadaka hiyo italiwa siku iyo hiyo mnayoitoa, au kesho yake; chochote kitakachobaki hadi siku ya tatu lazima kiteketezwe kwa moto. Kama sehemu yoyote ya sadaka hiyo italiwa siku ya tatu, itakuwa si safi, nayo haitakubaliwa. Yeyote atakayekula atawajibishwa, kwa sababu amenajisi kitu kilicho kitakatifu kwa Bwana; mtu huyo lazima akatiliwe mbali na watu wake.
“ ‘Wakati uvunapo mavuno ya nchi yako, usivune hadi kwenye mipaka ya shamba lako, wala usikusanye mabaki ya mavuno yako. 10 Usirudi mara ya pili katika shamba lako la mizabibu, wala usiokote zabibu zilizoanguka chini. Ziache kwa ajili ya maskini na mgeni. Mimi ndimi Bwana Mungu wako.
11 “ ‘Usiibe.
“ ‘Usiseme uongo.
“ ‘Msidanganyane.
12 “ ‘Usiape kwa uongo kwa Jina langu, na hivyo kulinajisi jina la Mungu wako. Mimi ndimi Bwana.
13 “ ‘Usimdhulumu wala kumwibia jirani yako.
“ ‘Usishikilie mshahara wa kibarua usiku kucha hadi asubuhi.
14 “ ‘Usimlaani kiziwi, wala usiweke kikwazo mbele ya kipofu, lakini umche Mungu wako. Mimi ndimi Bwana.
15 “ ‘Usipotoshe haki; usionyeshe kumpendelea maskini, wala upendeleo kwa mwenye cheo, bali mwamulie jirani yako kwa haki.
16 “ ‘Usieneze uchochezi miongoni mwa watu wako.
“ ‘Usifanye kitu chochote kile kinachohatarisha maisha ya jirani yako. Mimi ndimi Bwana.
17 “ ‘Usimchukie ndugu yako moyoni mwako. Karipia jirani yako kwa uwazi ili usishiriki hatia yake.
18 “ ‘Usijilipizie kisasi wala kuwa na kinyongo dhidi ya mmoja wa jamaa yako, lakini mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe. Mimi ndimi Bwana.
19 “ ‘Mtazishika amri zangu.
“ ‘Usiwaache wanyama wako wa kufugwa wakazaana na wengine wa aina tofauti.
“ ‘Usipande mbegu za aina mbili katika shamba lako.
“ ‘Usivae nguo iliyofumwa kwa nyuzi za aina mbili tofauti.
20 “ ‘Kama mwanaume anakutana kimwili na mwanamke ambaye ni msichana mtumwa aliyeposwa na mwanaume mwingine, lakini ambaye hajakombolewa wala hajapewa uhuru, lazima iwepo adhabu inayofaa. Hata hivyo hawatauawa, kwa sababu msichana alikuwa bado hajaachwa huru. 21 Lakini huyo mtu lazima alete kondoo dume kwenye ingilio la Hema la Kukutania kwa ajili ya sadaka ya hatia kwa Bwana. 22 Kupitia kwa huyo kondoo dume wa sadaka ya hatia, kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana kwa ajili ya dhambi aliyotenda, naye atasamehewa dhambi yake.
23 “ ‘Mtakapoingia katika hiyo nchi na kupanda aina yoyote ya mti wa matunda, hesabuni matunda yake kama yaliyokatazwa. Kwa miaka mitatu mtayahesabu kwamba yamekatazwa; hayaruhusiwi kuliwa. 24 Katika mwaka wa nne matunda yote ya mti huo yatakuwa matakatifu, sadaka ya sifa kwa Bwana. 25 Bali katika mwaka wa tano mnaweza kula matunda ya mti huo. Kwa njia hii mavuno yenu yataongezewa. Mimi ndimi Bwana Mungu wako.
26 “ ‘Msile nyama yoyote yenye damu ndani yake.
“ ‘Msifanye uaguzi wala uchawi.
27 “ ‘Msikate nywele za kichwa denge, wala kunyoa pembe za ndevu zenu.
28 “ ‘Msichanje chale miili yenu kwa ajili ya mfu, wala msijichore alama juu ya miili yenu. Mimi ndimi Bwana.
29 “ ‘Usimdhalilishe binti yako kwa kumfanya kahaba, la sivyo nchi itageukia ukahaba na kujaa uovu.
30 “ ‘Shika Sabato zangu na kuheshimu mahali pangu patakatifu. Mimi ndimi Bwana.
31 “ ‘Msiende kwa waaguzi, wala msitafute wapunga pepo, kwa maana watawanajisi. Mimi ndimi Bwana Mungu wako.
32 “ ‘Uwapo mbele ya mzee, simama ili kuonyesha heshima kwa wazee, nawe umche Mungu wako. Mimi ndimi Bwana.
33 “ ‘Wakati mgeni anaishi pamoja nawe katika nchi yako, usimnyanyase. 34 Mgeni anayeishi pamoja nawe ni lazima umtendee kama mmoja wa wazawa wa nchi yako. Mpende kama unavyojipenda mwenyewe, kwa maana ulikuwa mgeni katika nchi ya Misri. Mimi ndimi Bwana Mungu wako.
35 “ ‘Usitumie vipimo vya udanganyifu unapopima urefu, kupima uzito, wala kupima wingi. 36 Tumia mizani halali, mawe ya kupimia uzito halali, efa* halali, na hini halali. Mimi ndimi Bwana Mungu wako, ambaye alikutoa katika nchi ya Misri.
37 “ ‘Shika amri zangu zote na sheria zangu zote, nawe uzifuate. Mimi ndimi Bwana.’ ”
* 19:36 Efa kilikuwa kipimo cha vitu vikavu. 19:36 Hini kilikuwa kipimo cha vitu vimiminika.