22
Matumizi Ya Sadaka Takatifu
Bwana akamwambia Mose, “Mwambie Aroni na wanawe kushughulikia kwa uangalifu sadaka takatifu Waisraeli wanazoziweka wakfu kwangu, ili wasilinajisi Jina langu takatifu. Mimi ndimi Bwana.
“Waambie: ‘Katika vizazi vijavyo, ikiwa yeyote wa wazao wako ni najisi kwa taratibu za kiibada, naye akakaribia sadaka takatifu zile Waisraeli wanazoweka wakfu kwa Bwana, mtu huyo lazima akatiliwe mbali na uso wangu. Mimi ndimi Bwana.
“ ‘Ikiwa mzao wa Aroni ana ugonjwa wa ngozi unaoambukiza au anatokwa na usaha mwilini, hawezi kula sadaka takatifu mpaka atakasike. Pia atakuwa najisi ikiwa atagusa kitu chochote kilicho najisi kwa kugusa maiti au mtu aliyetokwa na shahawa, au ikiwa atagusa kitu chochote kitambaacho kimfanyacho mtu najisi, au mtu yeyote awezaye kumtia unajisi, hata unajisi uwe gani. Mtu anayegusa kitu chochote cha aina hiyo atakuwa najisi mpaka jioni. Kamwe hatakula sadaka yoyote takatifu mpaka yeye mwenyewe awe ameoga kwa maji. Wakati jua linapotua, atakuwa safi, na baadaye anaweza kula sadaka takatifu, kwa kuwa ni vyakula vyake. Kamwe asile nyama ya mzoga wala iliyoraruliwa na wanyama pori, naye akatiwa unajisi kwa hilo. Mimi ndimi Bwana.
“ ‘Makuhani lazima washike maagizo yangu ili wasiwe na hatia, wakafa kwa kuyadharau. Mimi ndimi Bwana ninayewafanya watakatifu.
10 “ ‘Hakuna mtu yeyote asiye wa jamaa ya kuhani anayeruhusiwa kula sadaka takatifu, hata mgeni wa kuhani au mfanyakazi wake haruhusiwi kuila. 11 Lakini ikiwa kuhani amenunua mtumwa kwa fedha, au mtumwa amezaliwa katika nyumba ya kuhani huyo, mtumwa huyo aweza kula chakula cha huyo kuhani. 12 Ikiwa binti wa kuhani ameolewa na mtu asiye kuhani, binti huyo haruhusiwi kula chochote cha matoleo matakatifu. 13 Lakini ikiwa binti wa kuhani amekuwa mjane au amepewa talaka, naye hana watoto, na akarudi kuishi na jamaa ya baba yake kama wakati wa usichana wake, binti huyo anaweza kula chakula cha baba yake. Hata hivyo, mtu asiyeruhusiwa hawezi kula chochote katika chakula hiki.
14 “ ‘Ikiwa mtu yeyote amekula sadaka takatifu kwa makosa, lazima atoe malipo ya sadaka hiyo kwa kuhani na kuongeza sehemu ya tano ya thamani ya sadaka hiyo. 15 Kamwe makuhani wasiinajisi sadaka takatifu ambayo Waisraeli wameitoa kwa Bwana 16 kwa kuwaruhusu kuzila sadaka hizo takatifu, na hivyo kuwaletea hatia ya kudaiwa malipo. Mimi ndimi Bwana niwafanyaye watakatifu.’ ”
Dhabihu Zisizokubalika
17  Bwana akamwambia Mose, 18 “Sema na Aroni na wanawe, na Waisraeli wote uwaambie: ‘Ikiwa mmoja wenu, aliye Mwisraeli au mgeni anayeishi katika nchi ya Israeli, atatoa matoleo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa kwa moto kwa Bwana, iwe kutimiza nadhiri au kuwa sadaka ya hiari, 19 lazima mtoe mnyama dume asiye na dosari, akiwa ngʼombe, mbuzi au kondoo, ili aweze kukubalika kwa niaba yako. 20 Kamwe usitoe kitu chochote chenye dosari kwa sababu hakitakubaliwa kwa niaba yako. 21 Mtu yeyote aletapo sadaka ya amani kwa Bwana kutoka kundi la ngʼombe au mbuzi ili kutimiza nadhiri maalum au sadaka ya hiari, lazima sadaka hiyo isiwe na dosari au waa ili ikubalike. 22 Kamwe usimtolee Bwana mnyama aliye kipofu, aliyejeruhiwa wala aliye kilema, au chochote kilicho na uvimbe, au chenye upele au vidonda vinavyotoka usaha. Kamwe chochote cha aina hii kisiwekwe juu ya madhabahu kuwa sadaka iliyotolewa kwa Bwana ya kuteketezwa kwa moto. 23 Lakini waweza ukatoa ngʼombe au kondoo mwenye kilema au aliyedumaa kama sadaka ya hiari, lakini hii haitakubalika kuwa sadaka ya kutimiza nadhiri. 24 Kamwe usimtolee Bwana mnyama ambaye mapumbu yake yamejeruhiwa, au kuhasiwa, au kuraruliwa au kukatwa. Kamwe usifanye hivi katika nchi yako mwenyewe, 25 na kamwe usikubali wanyama wa aina hii kutoka mkono wa mgeni ili kuwatoa wanyama hao kuwa chakula kwa Mungu wako. Wanyama hao hawatakubaliwa kwa niaba yako, kwa sababu wana vilema, nao wana dosari.’ ”
26  Bwana akamwambia Mose, 27 “Wakati ndama, mwana-kondoo au mwana-mbuzi azaliwapo, atabaki na mama yake kwa siku saba. Kuanzia siku ya nane na kuendelea anaweza kukubaliwa kuwa sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa kuteketezwa kwa moto. 28 Usimchinje ngʼombe na ndama wake, au kondoo na kitoto chake siku moja.
29 “Unapomtolea Bwana dhabihu ya shukrani, itoe kwa namna ambayo itakubalika kwa niaba yako. 30 Ni lazima iliwe siku iyo hiyo, pasipo kubakiza chochote mpaka asubuhi. Mimi ndimi Bwana.
31 “Shikeni maagizo yangu na kuyafuata. Mimi ndimi Bwana. 32 Msilinajisi Jina langu takatifu. Lazima nikubalike kuwa mtakatifu kwa Waisraeli. Mimi ndimi Bwana ninayewafanya watakatifu, 33 na niliyewatoa katika nchi ya Misri niwe Mungu wenu. Mimi ndimi Bwana.”