27
Kukomboa Kile Kilicho Cha Bwana
1 Bwana akamwambia Mose,
2 “Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Kama mtu yeyote ataweka nadhiri maalum ili kuweka watu wakfu kwa Bwana, kwa kutoa kiasi cha thamani inayolingana,
3 thamani ya kukomboa mwanaume mwenye kati ya umri wa miaka ishirini na miaka sitini itakuwa shekeli hamsini za fedha, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu;
4 ikiwa ni mwanamke, weka thamani yake kwa shekeli thelathini.
5 Kama ni mtu mwenye umri wa miaka kati ya mitano na ishirini, weka thamani ya mwanaume kuwa shekeli ishirini, na mwanamke shekeli kumi.
6 Kama ni mtu mwenye umri kati ya mwezi mmoja na miaka mitano, weka thamani ya mwanaume kuwa shekeli tano za fedha, na ile ya mwanamke kuwa shekeli tatu za fedha.
7 Kama ni mtu mwenye miaka sitini na zaidi, weka thamani ya mwanaume kuwa shekeli kumi na tano, na mwanamke shekeli kumi.
8 Kama mtu yeyote anayeweka nadhiri ni maskini mno kuweza kulipa kiasi kilichowekwa, atampeleka huyo mtu kwa kuhani, ambaye ataweka thamani yake kulingana na kile mweka nadhiri anachoweza kulipa.
9 “ ‘Kama kile mtu alichokiwekea nadhiri ni mnyama anayekubalika kama sadaka kwa Bwana, mnyama wa namna hiyo aliyetolewa kwa Bwana anakuwa mtakatifu.
10 Mtu haruhusiwi kumbadilisha au kutoa mnyama mzuri kwa mbaya, au mnyama mbaya kwa mzuri. Kama atatoa mnyama badala ya mwingine, wanyama wote wawili, yaani yule aliyetolewa na yule aliyebadiliwa, ni watakatifu.
11 Kama alichokiwekea nadhiri ni mnyama aliye najisi kiibada, yaani yule asiye kubalika kuwa sadaka kwa Bwana, huyo mnyama lazima aletwe kwa kuhani,
12 ambaye ataamua ubora wa mnyama huyo, kama ni mzuri au mbaya. Thamani yoyote atakayoweka kuhani, hivyo ndivyo itakavyokuwa.
13 Kama mwenye mnyama atapenda kumkomboa mnyama huyo, lazima aongeze sehemu ya tano ya thamani yake.
14 “ ‘Kama mtu ataweka nyumba yake wakfu kama kitu kitakatifu kwa Bwana, kuhani ataamua ubora wa nyumba hiyo, kama ni nzuri au mbaya. Thamani yoyote kuhani atakayoweka, basi hivyo ndivyo itakavyokuwa.
15 Kama mtu aliyeweka nyumba yake wakfu ataikomboa, lazima aongeze sehemu ya tano ya thamani yake, nayo nyumba itakuwa yake tena.
16 “ ‘Kama mtu anaweka sehemu ya ardhi ya jamaa yake wakfu kwa Bwana, thamani yake itawekwa kulingana na kiasi cha mbegu inayohitajiwa kupandwa katika ardhi hiyo, yaani homeri moja ya mbegu za shayiri kwa shekeli hamsini za fedha.
17 Kama akiweka shamba lake wakfu katika Mwaka wa Yubile, ile thamani iliyokwisha wekwa itakuwa iyo hiyo.
18 Lakini kama akiweka shamba lake wakfu baada ya Yubile, kuhani ataweka thamani kulingana na idadi ya miaka iliyobaki kufikia Mwaka wa Yubile unaofuata, na thamani yake iliyoamuliwa itapunguzwa.
19 Kama mtu anayeweka wakfu shamba anataka kulikomboa, lazima aongeze sehemu ya tano ya thamani yake, nalo shamba litakuwa lake tena.
20 Kama pengine halikomboi shamba hilo, au kama ameliuza kwa mtu mwingine, kamwe haliwezi kukombolewa.
21 Shamba hilo litakapoachiwa mwaka wa Yubile, litakuwa takatifu, kama shamba lililotolewa kwa Bwana, nalo litakuwa mali ya makuhani.
22 “ ‘Kama mtu ameweka wakfu kwa Bwana shamba alilonunua, ambalo si sehemu ya ardhi ya jamaa yake,
23 kuhani ataamua thamani yake hadi Mwaka wa Yubile, naye huyo mtu atalazimika kulipa thamani yake siku hiyo kama kitu kitakatifu kwa Bwana.
24 Katika Mwaka wa Yubile, shamba litarudishwa kwa mtu yule ambaye lilinunuliwa kutoka kwake, yule ambaye ardhi ilikuwa mali yake.
25 Kila thamani lazima iwekwe kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, gera ishirini kwa shekeli.
26 “ ‘Lakini hakuna mtu atakayeweka wakfu mzaliwa wa kwanza wa mnyama, kwa kuwa mzaliwa wa kwanza tayari ni mali ya Bwana; awe ngʼombe au kondoo, ni wa Bwana.
27 Kama ni mmoja wa wanyama walio najisi, aweza kumnunua kwa bei iliyowekwa, akiongeza sehemu ya tano ya thamani yake. Kama hatamkomboa, mnyama huyo atauzwa kwa bei iliyowekwa.
28 “ ‘Lakini chochote kile mtu alicho nacho na akakiweka wakfu kwa Bwana, iwe ni binadamu, au mnyama, au ardhi ya jamaa, hakiwezi kuuzwa au kukombolewa. Chochote kilichowekwa wakfu ni kitakatifu sana kwa Bwana.
29 “ ‘Mtu yeyote aliyewekwa wakfu ili kuangamizwa, hawezi kukombolewa. Mtu kama huyo lazima auawe.
30 “ ‘Zaka ya kila kitu kutoka shambani, iwe ni nafaka kutoka kwa ardhi, au tunda kutoka kwa miti, ni mali ya Bwana; ni takatifu kwa Bwana.
31 Kama mtu akikomboa chochote cha zaka yake, lazima aongeze sehemu ya tano ya thamani yake.
32 Zaka yote ya kundi la ngʼombe au la kondoo na mbuzi, kila mnyama wa kumi apitaye chini ya fimbo ya yule awachungaye, atakuwa mtakatifu kwa Bwana.
33 Yule mnyama wa kumi hatachaguliwa kwa kigezo cha uzuri au ubaya, naye haruhusiwi kubadiliwa. Ikiwa atabadiliwa, basi mnyama yule wa kwanza na huyo aliyebadiliwa wote watahesabiwa kuwa watakatifu, na haiwezekani kuwakomboa.’ ”
34 Haya ndiyo maagizo Bwana aliyompa Mose juu ya Mlima Sinai kwa ajili ya Waisraeli.