Nehemia
1
Maombi Ya Nehemia
1 Maneno ya Nehemia mwana wa Hakalia:
Katika mwezi wa Kisleu katika mwaka wa ishirini, wakati nilikuwa ngomeni katika jumba la kifalme la Shushani,
2 Hanani, mmoja wa ndugu zangu, alikuja kutoka Yuda akiwa na watu wengine, nami nikawauliza kuhusu mabaki ya Wayahudi wale walionusurika kwenda uhamishoni na pia kuhusu Yerusalemu.
3 Wakaniambia, “Wale walionusurika kwenda uhamishoni, wale ambao wamerudi kwenye lile jimbo, wako katika taabu kubwa na aibu. Ukuta wa Yerusalemu umebomoka, na malango yake yamechomwa moto.”
4 Niliposikia mambo haya, niliketi, nikalia. Kwa siku kadhaa niliomboleza na kufunga na kuomba mbele za Mungu wa mbinguni.
5 Kisha nikasema:
“Ee Bwana, Mungu wa mbinguni, mkuu na mwenye kuogofya, ambaye hulishika agano lake la upendo na wale wampendao na kutii amri zake,
6 tega masikio yako, na ufungue macho yako, ili usikie maombi ya mtumishi wako anayoomba mbele yako usiku na mchana kwa ajili ya watumishi wako, watu wa Israeli. Ninaungama dhambi zetu sisi Waisraeli, pamoja na zangu na za nyumba ya baba yangu, tulizotenda dhidi yako.
7 Tumetenda uovu sana mbele zako. Hatukutii amri, maagizo na sheria ulizompa Mose mtumishi wako.
8 “Kumbuka agizo ulilompa Mose mtumishi wako, ukisema, ‘Kama mkikosa uaminifu, nitawatawanya miongoni mwa mataifa,
9 lakini mkinirudia na kutii amri zangu, ndipo hata kama watu wenu walio uhamishoni wako mbali sana katika miisho ya dunia, nitawakusanya kutoka huko na kuwaleta mahali ambapo nimepachagua kuwa makao kwa ajili ya Jina langu.’
10 “Hawa ni watumishi wako na watu wako, uliowakomboa kwa nguvu zako kuu na mkono wako wenye nguvu.
11 Ee Bwana, tega sikio lako na usikie maombi ya huyu mtumishi wako, na maombi ya watumishi wako wanaofurahia kuliheshimu Jina lako. Nipe leo, mimi mtumishi wako, mafanikio kwa kunipa kibali mbele ya mtu huyu.”
Kwa maana nilikuwa mnyweshaji wa mfalme.