9
Waisraeli Waungama Dhambi Zao
1 Katika siku ya ishirini na nne ya mwezi ule ule, Waisraeli walikusanyika pamoja, wakifunga na kuvaa nguo za gunia na kujitia mavumbi vichwani mwao.
2 Wale wa uzao wa Israeli walijitenga na wageni wote. Wakasimama mahali pao, na kuungama dhambi zao na uovu wa baba zao.
3 Wakasimama pale walipokuwa, wakasoma kutoka kwenye kile Kitabu cha Sheria ya Bwana Mungu wao kwa muda wa robo siku, na wakatumia robo nyingine kwa kuungama dhambi na kumwabudu Bwana Mungu wao.
4 Walawi wafuatao walikuwa wamesimama kwenye ngazi: Yeshua, Bani, Kadmieli, Shebania, Buni, Sherebia, Bani na Kenani. Hawa walimlilia Bwana Mungu wao kwa sauti kubwa.
5 Nao Walawi Yeshua, Kadmieli, Bani, Hashabnea, Sherebia, Hodia, Shebania na Pethahia wakasema: “Simameni mkamsifu Bwana Mungu wenu, yeye ambaye ni Mungu tangu milele hata milele.
“Libarikiwe jina lake tukufu, litukuzwe juu ya baraka zote na sifa.
6 Wewe peke yako ndiwe Bwana. Uliziumba mbingu, hata mbingu za mbingu na jeshi lote la mbinguni, dunia na vyote vilivyo ndani yake, na pia bahari na vyote vilivyomo ndani yake. Huvipa vitu vyote uhai, nalo jeshi la mbinguni linakuabudu wewe.
7 “Wewe ni Bwana Mungu uliyemchagua Abramu na kumtoa kutoka Uru ya Wakaldayo, nawe ukamwita Abrahamu.
8 Uliona kuwa moyo wake ni mwaminifu kwako, nawe ukafanya Agano naye kuwapa wazao wake nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wayebusi na Wagirgashi. Umetimiza ahadi yako kwa sababu wewe ni mwenye haki.
9 “Uliona mateso ya baba zetu huko Misri, ukasikia kilio chao huko Bahari ya Shamu.
10 Ulituma ishara za miujiza na maajabu dhidi ya Farao, dhidi ya maafisa wake wote na watu wote wa nchi yake, kwa kuwa ulifahamu jinsi Wamisri walivyowafanyia ufidhuli. Ukajifanyia jina linalodumu hadi leo.
11 Ukagawa bahari mbele yao, ili waweze kupita katikati yake penye nchi kavu, lakini uliwatupa Wamisri waliowafuatilia katika vilindi, kama jiwe kwenye maji mengi.
12 Mchana uliwaongoza kwa nguzo ya wingu, na usiku kwa nguzo ya moto kuwamulikia njia iliyowapasa kuiendea.
13 “Ulishuka katika Mlima Sinai, ukanena nao kutoka mbinguni. Uliwapa masharti na sheria zile ambazo ni za kweli na haki, pia amri na maagizo mazuri.
14 Uliwafahamisha Sabato yako takatifu na ukawapa amri, maagizo na sheria kupitia mtumishi wako Mose.
15 Katika njaa yao uliwapa mkate kutoka mbinguni, na katika kiu yao uliwatolea maji kutoka kwenye mwamba. Uliwaambia waingie na kuimiliki nchi ambayo ulikuwa umeapa kuwapa kwa mkono ulioinuliwa.
16 “Lakini wao, baba zetu, wakawa na kiburi na shingo ngumu, nao hawakutii maagizo yako.
17 Wakakataa kusikiliza na kushindwa kukumbuka miujiza uliyoifanya miongoni mwao. Wakawa na shingo ngumu, na katika uasi wao wakamchagua kiongozi ili warudi kwenye utumwa wao. Lakini wewe ni Mungu mwenye kusamehe, mwenye neema na mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa upendo. Kwa hiyo hukuwaacha,
18 hata wakati walijitengenezea sanamu ya ndama ya kusubu na kusema, ‘Huyu ni mungu wenu, aliyewapandisha kutoka nchi ya Misri,’ au walipofanya makufuru makubwa.
19 “Kwa sababu ya huruma zako kuu hukuwaacha jangwani. Wakati wa mchana ile nguzo ya wingu haikukoma kuwaongoza katika njia yao, wala nguzo ya moto haikuacha kuwamulikia usiku njia iliyowapasa kuiendea.
20 Uliwapa Roho wako mwema ili kuwafundisha. Hukuwanyima mana yako vinywani mwao, nawe ukawapa maji kwa ajili ya kiu yao.
21 Kwa miaka arobaini uliwatunza jangwani. Hawakukosa chochote, na nguo zao hazikuchakaa wala miguu yao haikuvimba.
22 “Uliwapa falme na mataifa, ukiwagawia hata mipaka ya mbali. Wakaimiliki nchi ya Sihoni mfalme wa Heshboni, na nchi ya Ogu mfalme wa Bashani.
23 Uliwafanya wana wao kuwa wengi kama nyota za angani, nawe ukawaleta katika nchi ambayo uliwaambia baba zao kuingia na kuimiliki.
24 Wana wao wakaingia na kuimiliki nchi. Uliwatiisha Wakanaani mbele yao, walioishi katika nchi, ukawatia Wakanaani mikononi mwao, pamoja na wafalme wao na watu wa nchi, wawafanyie kama wapendavyo.
25 Wakateka miji yenye ngome na nchi yenye rutuba, wakamiliki nyumba zilizojazwa na vitu vizuri vya kila aina, visima vilivyochimbwa tayari, mashamba ya mizabibu, mashamba ya mizeituni na miti yenye matunda kwa wingi. Wakala, wakashiba nao wakanawiri sana, wakajifurahisha katika wema wako mwingi.
26 “Lakini hawakukutii nao wakaasi dhidi yako, wakatupa sheria zako nyuma yao. Wakawaua manabii wako, waliowaonya ili wakurudie, na wakafanya makufuru makubwa.
27 Hivyo ukawatia mikononi mwa adui zao, ambao waliwatesa. Lakini walipoteswa, wakakulilia wewe. Kutoka mbinguni uliwasikia, nawe kwa huruma zako kuu ukawapa waokozi, waliowaokoa kutoka mikononi mwa adui zao.
28 “Lakini mara walipokuwa na raha, wakafanya maovu tena machoni pako. Kisha ukawaacha mikononi mwa adui zao, nao wakawatawala. Walipokulilia tena, ukasikia kutoka mbinguni, na kwa huruma zako ukawaokoa kila mara.
29 “Ukawaonya warudi katika sheria yako, lakini wakawa na kiburi na hawakutii amri zako. Wakatenda dhambi dhidi ya maagizo yako ambayo kwayo mtu ataishi kama akiyatii. Kwa ukaidi wakakugeuzia kisogo, wakawa na shingo ngumu na wakakataa kusikiliza.
30 Kwa miaka mingi ulikuwa mvumilivu kwao. Kwa njia ya Roho wako ukawaonya kupitia manabii wako. Hata hivyo hawakujali, basi ukawatia mikononi mwa mataifa jirani.
31 Lakini kwa rehema zako kuu hukuwakomesha wala kuwaacha, kwa kuwa wewe ni Mungu mwenye neema na rehema.
32 “Basi sasa, Ee Mungu wetu, uliye mkuu, mwenye nguvu na Mungu wa kuogofya, mwenye kushika agano lake la upendo, usiache taabu hizi zote zionekane kuwa kitu kidogo mbele za macho yako, taabu hizi zilizotupata, juu ya wafalme wetu na viongozi, juu ya makuhani wetu na manabii, juu ya baba zetu na watu wako wote, tangu siku za wafalme wa Ashuru hadi leo.
33 Katika hayo yote yaliyotupata, umekuwa mwenye haki, na umetenda kwa uaminifu, wakati sisi tumetenda mabaya.
34 Wafalme wetu, viongozi wetu, makuhani wetu na baba zetu hawakufuata sheria yako. Hawakuzingatia amri zako wala maonyo uliyowapa.
35 Hata walipokuwa wangali katika ufalme wao, wakiufurahia wema wako mkuu katika nchi kubwa na yenye rutuba uliyowapa, hawakukutumikia wala kugeuka kutoka njia zao mbaya.
36 “Lakini tazama, sisi ni watumwa leo, watumwa katika nchi uliyowapa baba zetu ili wapate kula matunda yake na vitu vingine vizuri inayozalisha.
37 Kwa sababu ya dhambi zetu, mavuno yake mengi huenda kwa wafalme uliowaweka watutawale. Wanatawala juu ya miili yetu na mifugo yetu kama wapendavyo. Tuko katika dhiki kuu.
Mapatano Ya Watu
38 “Kwa sababu ya haya yote, tunajifunga katika mapatano, na kuyaandika, nao viongozi wetu, Walawi wetu na makuhani wetu wanatia mihuri yao.”