13
Kupeleleza Kanaani
(Kumbukumbu 1:19-33)
Bwana akamwambia Mose, “Watume baadhi ya watu wakaipeleleze nchi ya Kanaani, ambayo ninawapa Waisraeli. Kutoka kwa kila kabila la baba zao, tuma mmoja wa viongozi wao.”
Hivyo kwa agizo la Bwana Mose akawatuma kutoka Jangwa la Parani. Wote walikuwa viongozi wa Waisraeli. Haya ndiyo majina yao:
 
kutoka kabila la Reubeni, Shamua mwana wa Zakuri;
kutoka kabila la Simeoni, Shafati mwana wa Hori;
kutoka kabila la Yuda, Kalebu mwana wa Yefune;
kutoka kabila la Isakari, Igali mwana wa Yosefu;
kutoka kabila la Efraimu, Hoshea mwana wa Nuni;
kutoka kabila la Benyamini, Palti mwana wa Rafu;
10 kutoka kabila la Zabuloni, Gadieli mwana wa Sodi,
11 kutoka kabila la Manase (kabila la Yosefu), Gadi mwana wa Susi;
12 kutoka kabila la Dani, Amieli mwana wa Gemali;
13 kutoka kabila la Asheri, Sethuri mwana wa Mikaeli;
14 kutoka kabila la Naftali, Nabi mwana wa Wofsi;
15 kutoka kabila la Gadi, Geueli mwana wa Maki.
 
16 Haya ndiyo majina ya watu ambao Mose aliwatuma kuipeleleza nchi. (Mose akampa Hoshea mwana wa Nuni jina Yoshua.)
17 Mose alipowatuma wakaipeleleze Kanaani, alisema, “Pandeni kupitia Negebu, mwende mpaka nchi ya vilima. 18 Mwone nchi ni ya namna gani, na kama watu waishio humo wana nguvu au ni wadhaifu, iwapo ni wachache au wengi. 19 Wanaishi katika nchi ya namna gani? Je, ni nzuri au mbaya? Wanaishi katika miji ya namna gani? Je, haina kuta au ngome? 20 Ardhi iko aje? Ina rutuba au la? Je, kuna miti ndani yake au la? Jitahidini kadiri mwezavyo kuleta baadhi ya matunda ya nchi.” (Ulikuwa msimu wa kuiva zabibu za kwanza.)
21 Hivyo wakapanda na kuipeleleza nchi kutoka Jangwa la Sini hadi Rehobu, kuelekea Lebo-Hamathi. 22 Wakapanda kupitia Negebu hadi wakafika Hebroni, mahali ambapo Ahimani, Sheshai na Talmai, wazao wa Anaki, waliishi. (Hebroni ulikuwa umejengwa miaka saba kabla ya mji wa Soani ulioko Misri.) 23 Walipofika katika Bonde la Eshkoli, walivunja tawi lililokuwa na kishada kimoja cha zabibu. Wawili wao wakalichukua lile tawi kwenye mti, pamoja na komamanga na tini. 24 Eneo lile likaitwa Bonde la Eshkoli kwa sababu ya kile kishada cha zabibu ambacho Waisraeli walikikata huko. 25 Mwishoni mwa siku arobaini wakarudi kutoka kuipeleleza nchi.
Taarifa Juu Ya Upelelezi
26 Wakarudi kwa Mose, Aroni na jumuiya yote ya Waisraeli huko Kadeshi kwenye Jangwa la Parani. Hapo ndipo walipotoa habari kwao na kwa kusanyiko lote na kuwaonyesha matunda ya hiyo nchi. 27 Wakampa Mose taarifa hii: “Tuliingia katika nchi uliyotutuma, nayo inatiririka maziwa na asali! Hili hapa tunda lake. 28 Lakini watu wanaoishi huko ni wenye nguvu, na miji yao ina ngome na ni mikubwa sana. Huko tuliona hata wazao wa Anaki. 29 Waamaleki wanaishi Negebu; Wahiti, Wayebusi na Waamori wanaishi katika nchi ya vilima; nao Wakanaani wanaishi karibu na bahari na kando ya Yordani.”
30 Kisha Kalebu akawanyamazisha watu mbele ya Mose na kusema, “Imetupasa kupanda na kuimiliki nchi, kwa maana hakika tunaweza kufanya hivyo.”
31 Lakini watu waliokuwa wamepanda pamoja naye wakasema, “Hatuwezi kuwashambulia wale watu; wana nguvu kutuliko sisi.” 32 Wakaeneza taarifa mbaya miongoni mwa Waisraeli kuhusu nchi waliyoipeleleza. Wakasema, “Nchi tuliyoipeleleza hula watu waishio ndani yake. Watu wote tuliowaona huko ni majitu. 33 Tuliwaona Wanefili huko (wazao wa Anaki wanatokana na Wanefili.) Tulijiona kama panzi machoni petu wenyewe, nao ndivyo walivyotuona.”