17
Kuchipuka Kwa Fimbo Ya Aroni
1 Bwana akamwambia Mose,
2 “Sema na Waisraeli, na ujipatie fimbo kumi na mbili kutoka kwao, moja kutoka kwa kila mmoja wa viongozi wa kabila za baba zao. Andika jina la kila mtu kwenye fimbo yake.
3 Kwenye fimbo ya Lawi andika jina la Aroni, kwa maana ni lazima iwepo fimbo moja kwa kila kiongozi kwa ajili ya kila kabila la baba zao.
4 Ziweke hizo fimbo ndani ya Hema la Kukutania mbele ya Sanduku la Ushuhuda, mahali nikutanapo nawe.
5 Fimbo ya mtu nitakayemchagua itachipuka, nami mwenyewe nitayakomesha haya manungʼuniko ya mara kwa mara ya Waisraeli dhidi yako.”
6 Hivyo Mose akasema na Waisraeli, nao viongozi wao wakampa fimbo kumi na mbili, fimbo moja kwa ajili ya kila kabila la baba zao, nayo fimbo ya Aroni ikiwa miongoni mwa hizo.
7 Mose akaziweka hizo fimbo mbele za Bwana ndani ya Hema la Ushuhuda.
8 Siku iliyofuata Mose aliingia kwenye Hema la Ushuhuda akaona ile fimbo ya Aroni ambayo iliwakilisha jamaa ya Lawi haikuwa tu imechipuka, bali pia ilikuwa imetoa machipukizi, kuchanua maua na kuzaa malozi.
9 Ndipo Mose akaleta zile fimbo zote kwa Waisraeli wote kutoka mbele za Bwana. Wakaziangalia, na kila mtu akaichukua fimbo yake mwenyewe.
10 Bwana akamwambia Mose, “Rudisha fimbo ya Aroni mbele ya Sanduku la Ushuhuda, ili ihifadhiwe kama alama kwa waasi. Hili litakomesha manungʼuniko yao dhidi yangu, ili kwamba wasife.”
11 Mose akafanya kama Bwana alivyomwamuru.
12 Waisraeli wakamwambia Mose, “Tutakufa! Tumepotea, sote tumepotea!
13 Yeyote akaribiaye Maskani ya Bwana atakufa. Je, sisi sote tutakufa?”