32
Makabila Ngʼambo Ya Yordani
(Kumbukumbu 3:12-22)
Kabila la Wareubeni na Wagadi, waliokuwa na makundi makubwa ya ngʼombe, kondoo na mbuzi, waliona kuwa nchi ya Yazeri na nchi ya Gileadi ni nzuri kwa mifugo. Hivyo walimjia Mose, na kuhani Eleazari na viongozi wa jumuiya, na kuwaambia, “Atarothi, Diboni, Yazeri, Nimra, Heshboni, Eleale, Sebamu, Nebo na Beoni, nchi ambayo Bwana ameishinda mbele ya wana wa Israeli, inafaa kwa mifugo, nao watumishi wako wana mifugo. Kama tumepata kibali mbele ya macho yako, nchi hii na ipewe watumishi wako kama milki yetu. Usitufanye tuvuke Yordani.”
Mose akawaambia Wagadi na Wareubeni, “Je, watu wa nchi yenu watakwenda vitani wakati ninyi mmeketi hapa? Kwa nini mmewakatisha Waisraeli tamaa wasivuke katika nchi ambayo Bwana amewapa? Hivi ndivyo baba zenu walivyofanya wakati nilipowatuma kutoka Kadesh-Barnea kuipeleleza nchi. Baada ya kufika kwenye Bonde la Eshkoli na kuitazama nchi, waliwakatisha tamaa Waisraeli wasiingie katika nchi ambayo Bwana alikuwa amewapa. 10 Siku ile hasira ya Bwana iliwaka naye akaapa kiapo hiki: 11 ‘Kwa kuwa hawakunifuata kwa moyo wote, hakuna mtu yeyote mwenye miaka ishirini au zaidi ambaye alikuja kutoka Misri atakayeona nchi niliyoahidi kwa kiapo kwa Abrahamu, Isaki na Yakobo; 12 hakuna hata mmoja isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, Mkenizi, na Yoshua mwana wa Nuni, kwa sababu walimfuata Bwana kwa moyo wote.’ 13 Hasira ya Bwana iliwaka dhidi ya Waisraeli na akawafanya watangetange katika jangwa kwa miaka arobaini, mpaka kizazi chote cha wale waliofanya maovu mbele yake kimeangamia.
14 “Nanyi mko hapa, uzao wa wenye dhambi, mkisimamia mahali pa baba zenu na mkimfanya Bwana kuwakasirikia Waisraeli hata zaidi. 15 Kama mkigeuka na mkiacha kumfuata, atawaacha tena watu hawa wote jangwani, na mtakuwa sababu ya maangamizi yao.”
16 Ndipo wakamjia Mose na kumwambia, “Tungalitaka kujenga mazizi hapa kwa ajili ya mifugo yetu na miji kwa ajili ya wanawake wetu na watoto. 17 Lakini sisi tuko tayari kuchukua silaha zetu na kutangulia mbele ya Waisraeli mpaka tutakapowaleta mahali pao. Wakati huo wanawake wetu na watoto wataishi katika miji yenye ngome, kwa ajili ya ulinzi dhidi ya wenyeji wa nchi. 18 Hatutarudi nyumbani mwetu mpaka kila Mwisraeli apokee urithi wake. 19 Hatutapokea urithi wowote pamoja nao ngʼambo ya Yordani, kwa sababu urithi wetu umekuja kwetu upande wa mashariki ya Yordani.”
20 Kisha Mose akawaambia, “Kama mtafanya jambo hili, kama mtajivika silaha mbele za Bwana kwa ajili ya vita, 21 na kama ninyi nyote mtakwenda mmejivika silaha ngʼambo ya Yordani mbele za Bwana mpaka awe amewafukuza adui zake mbele zake, 22 hadi wakati nchi itakapokuwa imeshindwa mbele za Bwana, ndipo mtaweza kurudi na kuwa huru kutoka masharti yenu kwa Bwana na Israeli. Nayo nchi hii itakuwa milki yenu mbele za Bwana.
23 “Lakini mkishindwa kufanya hili, mtakuwa mnatenda dhambi dhidi ya Bwana; nanyi kuweni na hakika kuwa dhambi yenu itawapata. 24 Jengeni miji kwa ajili ya wanawake na watoto wenu, na mazizi kwa ajili ya mbuzi na kondoo zenu, lakini fanyeni yale mliyoahidi.”
25 Wagadi na Wareubeni wakamwambia Mose, “Sisi watumishi wako tutafanya kama bwana wetu anavyotuagiza. 26 Watoto na wake zetu, makundi ya mbuzi na kondoo, na makundi ya ngʼombe zetu, watabaki hapa katika miji ya Gileadi. 27 Lakini watumishi wenu, kila mwanaume aliyevaa silaha za vita, watavuka ngʼambo kupigana mbele za Bwana, sawa kama bwana wetu anavyosema.”
28 Kisha Mose akatoa amri kuhusu wao kwa kuhani Eleazari, na Yoshua mwana wa Nuni na viongozi wa jamaa za makabila ya Waisraeli. 29 Mose akawaambia, “Ikiwa Wagadi na Wareubeni, kila mwanaume aliyevaa silaha za vita, atavuka Yordani pamoja nanyi mbele za Bwana, basi wakati mtakapoishinda nchi iliyoko mbele yenu, wapeni nchi ya Gileadi kama milki yao. 30 Lakini kama hawatavuka pamoja nanyi wakiwa wamevaa silaha za vita, lazima wakubali kupokea milki yao pamoja nanyi katika nchi ya Kanaani.”
31 Wagadi na Wareubeni wakajibu, “Watumishi wako watafanya lile Bwana alilosema. 32 Tutavuka mbele za Bwana kuingia Kanaani tukiwa tumevaa silaha za vita, lakini mali tutakayoirithi itakuwa ngʼambo hii ya Yordani.”
33 Kisha Mose akawapa Wagadi, Wareubeni, na nusu ya kabila la Manase mwana wa Yosefu ufalme wa Sihoni mfalme wa Waamori, na ufalme wa Ogu mfalme wa Bashani, nchi yote pamoja na miji yake, na nchi inayowazunguka.
34 Wagadi wakajenga Diboni, Atarothi, Aroeri, 35 Atroth-Shofani, Yazeri, Yogbeha, 36 Beth-Nimra na Beth-Harani kama miji iliyozungushiwa ngome, tena wakajenga mazizi kwa ajili ya makundi yao ya mbuzi na kondoo. 37 Nao Wareubeni wakajenga upya miji ya Heshboni, Eleale na Kiriathaimu, 38 pia Nebo na Baal-Meoni (majina ya hiyo miji yalibadilishwa) na Sibma. Miji waliyoijenga upya waliipa majina.
39 Wazao wa Makiri mwana wa Manase walikwenda Gileadi, wakaiteka nchi na kuwafukuza Waamori waliokuwa huko. 40 Kwa hiyo Mose akawapa Wamakiri, wazao wa Manase, nchi ya Gileadi, nao wakakaa huko. 41 Yairi, mzao wa Manase, akateka makao yao, akayaita Hawoth-Yairi. 42 Naye Noba akateka Kenathi na makao yaliyoizunguka, akayaita Noba kwa jina lake.