34
Mipaka Ya Kanaani
1 Bwana akamwambia Mose,
2 “Waamuru Waisraeli na uwaambie: ‘Mtakapoingia nchi ya Kanaani, nchi ambayo itagawanywa kwenu kama urithi itakuwa na mipaka ifuatayo:
3 “ ‘Upande wenu wa kusini utajumuisha sehemu ya Jangwa la Sini kufuata mpaka wa Edomu. Upande wa mashariki mpaka wenu wa kusini utaanzia mwisho wa Bahari ya Chumvi,
4 katiza kusini mwa Pito la Akrabimu, endelea mpaka Sini na kwenda kusini ya Kadesh-Barnea. Kisha mpaka huo utaenda hadi Hasar-Adari hadi Azmoni,
5 mahali ambapo utapinda, na kuunganika na Kijito cha Misri na kumalizikia kwenye Bahari ya Kati.
6 “ ‘Mpaka wenu wa magharibi utakuwa Bahari ya Kati. Huu utakuwa mpaka wenu upande wa magharibi.
7 “ ‘Kwa mpaka wenu wa kaskazini, wekeni alama kuanzia Bahari ya Kati hadi mlima Hori,
8 na kutoka mlima Hori hadi Pito la Hamathi. Kisha mpaka utaenda hadi Sedadi,
9 kuendelea hadi Zifroni, na kuishia Hasar-Enani. Huu utakuwa mpaka wenu upande wa kaskazini.
10 “ ‘Kwa mpaka wenu wa mashariki, wekeni alama kuanzia Hasar-Enani hadi Shefamu.
11 Mpaka utaelekea kusini kuanzia Shefamu hadi Ribla upande wa mashariki wa Aini, na kuendelea kwenye miteremko mashariki mwa Bahari ya Kinerethi.
12 Kisha mpaka utashuka kuelekea Mto Yordani na kuishia katika Bahari ya Chumvi.
“ ‘Hii itakuwa nchi yenu, ikiwa na mipaka yake kila upande.’ ”
13 Mose akawaamuru Waisraeli: “Gawanyeni nchi hii kwa kura kama urithi. Bwana ameagiza kwamba itolewe kwa yale makabila tisa na nusu,
14 kwa sababu jamaa ya kabila la Reubeni, kabila la Gadi, na nusu ya kabila la Manase wamekwishapokea urithi wao.
15 Haya makabila mawili na nusu wamekwishapokea urithi wao upande wa mashariki wa Yordani ngʼambo ya Yeriko, kuelekea mawio ya jua.”
16 Bwana akamwambia Mose,
17 “Haya ndiyo majina ya watu ambao watakusaidia kugawanya nchi kama urithi: Eleazari kuhani na Yoshua mwana wa Nuni.
18 Tena uteue kiongozi mmoja kutoka kila kabila kusaidia kuigawanya nchi.
19 Haya ndiyo majina yao:
“Kalebu mwana wa Yefune,
kutoka kabila la Yuda;
20 Shemueli mwana wa Amihudi,
kutoka kabila la Simeoni;
21 Elidadi mwana wa Kisloni,
kutoka kabila la Benyamini;
22 Buki mwana wa Yogli,
kiongozi kutoka kabila la Dani;
23 Hanieli mwana wa Efodi,
kiongozi kutoka kabila la Manase mwana wa Yosefu;
24 Kemueli mwana wa Shiftani,
kiongozi kutoka kabila la Efraimu mwana wa Yosefu;
25 Elisafani mwana wa Parnaki,
kiongozi kutoka kabila la Zabuloni;
26 Paltieli mwana wa Azani,
kiongozi kutoka kabila la Isakari;
27 Ahihudi mwana wa Shelomi,
kiongozi kutoka kabila la Asheri;
28 Pedaheli mwana wa Amihudi,
kiongozi kutoka kabila la Naftali.”
29 Hawa ndio watu ambao Bwana aliamuru wagawanye urithi kwa Waisraeli katika nchi ya Kanaani.