15
1 Jawabu la upole hugeuza ghadhabu,
bali neno liumizalo huchochea hasira.
2 Ulimi wa mwenye hekima husifu maarifa,
bali kinywa cha mpumbavu hufoka upumbavu.
3 Macho ya Bwana yako kila mahali,
yakiwaangalia waovu na wema.
4 Ulimi uletao uponyaji ni mti wa uzima,
bali ulimi udanganyao huponda roho.
5 Mpumbavu hubeza maonyo ya baba yake,
bali yeyote akubaliye maonyo huonyesha busara.
6 Nyumba ya mwenye haki ina hazina kubwa,
bali mapato ya waovu huwaletea taabu.
7 Midomo ya mwenye hekima hueneza maarifa,
bali sivyo ilivyo mioyo ya wapumbavu.
8 Bwana huchukia sana dhabihu za waovu,
bali maombi ya wanyofu humfurahisha Mungu.
9 Bwana huchukia sana njia ya waovu,
bali huwapenda wale wafuatao haki.
10 Adhabu kali humngoja yeye aachaye njia;
yeye achukiaye maonyo atakufa.
11 Mauti na Uharibifu viko wazi mbele za Bwana:
je, si zaidi sana mioyo ya wanadamu!
12 Mwenye mzaha huchukia maonyo;
hatataka shauri kwa mwenye hekima.
13 Moyo wenye furaha hufanya uso uchangamke,
bali maumivu ya moyoni huponda roho.
14 Moyo wa mwenye ufahamu hutafuta maarifa,
bali kinywa cha mpumbavu hujilisha upumbavu.
15 Siku zote za wanaoonewa ni za taabu,
bali moyo mchangamfu una karamu ya kudumu.
16 Afadhali kuwa na kidogo pamoja na kumcha Bwana,
kuliko mali nyingi pamoja na ghasia.
17 Afadhali chakula cha mboga mahali palipo na upendo
kuliko nyama ya ndama iliyonona pamoja na chuki.
18 Mtu mwepesi wa hasira huchochea ugomvi,
bali mtu mvumilivu hutuliza ugomvi.
19 Njia ya mvivu imezibwa na miiba,
bali njia ya mwenye haki ni barabara kuu.
20 Mwana mwenye hekima huleta furaha kwa baba yake,
bali mtu mpumbavu humdharau mama yake.
21 Upumbavu humfurahisha mtu ambaye hana akili,
bali mtu mwenye ufahamu hushika njia iliyonyooka.
22 Mipango hushindwa kufanikiwa kwa ajili ya kukosa ushauri,
bali kukiwa na washauri wengi hufanikiwa.
23 Mtu hupata furaha katika kutoa jibu linalofaa:
je, ni zuri namna gani neno lililotoka kwa wakati wake!
24 Mapito ya uzima huelekea juu kwa ajili ya wenye hekima
kumwepusha asiende chini kaburini.
25 Bwana hubomoa nyumba ya mtu mwenye kiburi,
bali huilinda mipaka ya mjane isiguswe.
26 Bwana huchukia sana mawazo ya mwovu,
bali mawazo ya wale walio safi humfurahisha yeye.
27 Mtu mwenye tamaa huletea jamaa yake taabu,
bali yeye achukiaye rushwa ataishi.
28 Moyo wa mwenye haki hupima majibu yake,
bali kinywa cha mwovu hufoka ubaya.
29 Bwana yuko mbali na waovu,
bali husikia maombi ya wenye haki.
30 Mtazamo wa tabasamu huleta furaha moyoni,
nazo habari njema huipa mifupa afya.
31 Yeye asikilizaye maonyo yatoayo uzima
atakuwa miongoni mwa wenye hekima.
32 Yeye anayedharau maonyo hujidharau mwenyewe,
bali yeyote anayekubali maonyo hupata ufahamu.
33 Kumcha Bwana humfundisha mtu hekima,
nao unyenyekevu huja kabla ya heshima.