Zaburi 103
Upendo Wa Mungu
Zaburi ya Daudi.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Vyote vilivyomo ndani yangu
vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
wala usisahau wema wake wote,
akusamehe dhambi zako zote,
akuponya magonjwa yako yote,
aukomboa uhai wako na kaburi,
akuvika taji ya upendo na huruma,
atosheleza mahitaji yako kwa vitu vyema,
ili ujana wako uhuishwe kama wa tai.
 
Bwana hutenda haki,
naye huwapa hukumu ya haki wote wanaoonewa.
 
Alijulisha Mose njia zake,
na wana wa Israeli matendo yake.
Bwana ni mwingi wa huruma na mwenye neema;
si mwepesi wa hasira, bali amejaa upendo.
Yeye hatalaumu siku zote,
wala haweki hasira yake milele,
10 yeye hatutendei kulingana na dhambi zetu
wala hatupatilizi kwa kadiri ya maovu yetu.
11 Kama vile mbingu zilivyo juu ya dunia sana,
ndivyo wema wake ulivyo mwingi kwa wanaomcha;
12 kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,
ndivyo Mungu alivyoziweka dhambi zetu mbali nasi.
13 Kama baba alivyo na huruma kwa watoto wake,
ndivyo Bwana anavyowahurumia wale wanaomcha;
14 kwa kuwa anajua tulivyoumbwa,
anakumbuka kwamba sisi tu mavumbi.
15 Kuhusu mwanadamu, siku zake ni kama majani,
anachanua kama ua la shambani;
16 upepo huvuma juu yake nalo hutoweka,
mahali pake hapalikumbuki tena.
17 Lakini kutoka milele hata milele
upendo wa Bwana uko kwa wale wamchao,
nayo haki yake kwa watoto wa watoto wao:
18 kwa wale walishikao agano lake
na kukumbuka kuyatii mausia yake.
 
19  Bwana ameweka imara kiti chake cha enzi mbinguni,
ufalme wake unatawala juu ya vyote.
20 Mhimidini Bwana, enyi malaika zake,
ninyi mlio mashujaa mnaozitii amri zake,
ninyi mnaotii neno lake.
21 Mhimidini Bwana, ninyi jeshi lake lote la mbinguni,
ninyi watumishi wake mnaofanya mapenzi yake.
22 Mhimidini Bwana, kazi zake zote
kila mahali katika milki yake.
 
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.