Zaburi 129
Maombi Dhidi Ya Adui Za Israeli
Wimbo wa kwenda juu.
Wamenionea mno tangu ujana wangu;
Israeli na aseme sasa:
wamenionea mno tangu ujana wangu,
lakini bado hawajanishinda.
Wakulima wamelima mgongo wangu,
na kufanya mifereji yao mirefu.
Lakini Bwana ni mwenye haki;
amenifungua toka kamba za waovu.
 
Wale wote waichukiao Sayuni
na warudishwe nyuma kwa aibu.
Wawe kama majani juu ya paa,
ambayo hunyauka kabla hayajakua;
kwa hayo mvunaji hawezi kujaza vitanga vyake,
wala akusanyaye kujaza mikono yake.
Wale wapitao karibu na wasiseme,
“Baraka ya Bwana iwe juu yako;
tunakubariki katika jina la Bwana.”