Zaburi 132
Maskani Ya Mungu Ya Milele Katika Sayuni
Wimbo wa kwenda juu.
Ee Bwana, mkumbuke Daudi
na taabu zote alizozistahimili.
 
Aliapa kiapo kwa Bwana
na akaweka nadhiri kwa Yule Mwenye Nguvu wa Yakobo:
“Sitaingia nyumbani mwangu
au kwenda kitandani mwangu:
sitaruhusu usingizi katika macho yangu,
wala kope zangu kusinzia,
mpaka nitakapompatia Bwana mahali,
makao kwa ajili ya Yule Mwenye Nguvu wa Yakobo.”
 
Tulisikia habari hii huko Efrathi,
tulikutana nayo katika mashamba ya Yaara:*
“Twendeni kwenye makao yake,
na tuabudu kwenye kiti cha kuwekea miguu yake;
inuka, Ee Bwana, uje mahali pako pa kupumzikia,
wewe na Sanduku la nguvu zako.
Makuhani wako na wavikwe haki,
watakatifu wako na waimbe kwa furaha.”
 
10 Kwa ajili ya Daudi mtumishi wako,
usimkatae mpakwa mafuta wako.
 
11  Bwana alimwapia Daudi kiapo,
kiapo cha uhakika ambacho hatakitangua:
“Nitamweka mmoja wa wazao wako mwenyewe
katika kiti chako cha enzi,
12 kama wanao watashika Agano langu
na sheria ninazowafundisha,
ndipo wana wao watarithi
kiti chako cha enzi milele na milele.”
 
13 Kwa maana Bwana ameichagua Sayuni,
amepaonea shauku pawe maskani yake:
14 “Hapa ni mahali pangu pa kupumzika milele na milele;
hapa ndipo nitakapoketi nikitawala, kwa sababu nimepaonea shauku:
15 Nitambariki kwa kumpa mahitaji tele:
nitashibisha maskini wake kwa chakula.
16 Nitawavika makuhani wake wokovu,
nao watakatifu wake watadumu wakiimba kwa furaha.
 
17 “Hapa nitamchipushia Daudi pembe,
na kuweka taa kwa ajili ya masiya wangu.
18 Adui zake nitawavika aibu,
bali taji kichwani pake itangʼaa sana.”
* Zaburi 132:6 Yaani Kiriath-Yearimu. Zaburi 132:17 Pembe inawakilisha nguvu. Zaburi 132:17 Masiya yaani mpakwa mafuta.