Zaburi 139
Mungu Asiyeweza Kukwepwa
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.
Ee Bwana, umenichunguza
na kunijua.
Unajua ninapoketi na ninapoinuka;
unatambua mawazo yangu tokea mbali.
Unafahamu kutoka kwangu na kulala kwangu;
unaelewa njia zangu zote.
Kabla neno halijafika katika ulimi wangu,
wewe walijua kikamilifu, Ee Bwana.
 
Umenizunguka nyuma na mbele;
umeweka mkono wako juu yangu.
Maarifa haya ni ya ajabu mno kwangu,
ni ya juu sana kwangu kuyafikia.
 
Niende wapi nijiepushe na Roho yako?
Niende wapi niukimbie uso wako?
Kama nikienda juu mbinguni, wewe uko huko;
nikifanya vilindi* kuwa kitanda changu,
wewe uko huko.
Kama nikipanda juu ya mbawa za mapambazuko,
kama nikikaa pande za mbali za bahari,
10 hata huko mkono wako utaniongoza,
mkono wako wa kuume utanishika kwa uthabiti.
 
11 Kama nikisema, “Hakika giza litanificha
na nuru inayonizunguka iwe usiku,”
12 hata giza halitakuwa giza kwako,
usiku utangʼaa kama mchana,
kwa kuwa giza ni kama nuru kwako.
 
13 Kwa maana wewe ndiwe uliyeumba utu wangu wa ndani;
uliniunga pamoja tumboni mwa mama yangu.
14 Ninakusifu kwa sababu nimeumbwa
kwa namna ya ajabu na ya kutisha;
kazi zako ni za ajabu,
ninajua hayo kikamilifu.
15 Umbile langu halikufichika kwako,
nilipoumbwa mahali pa siri.
Nilipoungwa pamoja kwa ustadi katika vilindi vya nchi,
16 macho yako yaliniona kabla mwili wangu haujakamilika.
Siku zangu zote ulizonipangia
ziliandikwa katika kitabu chako
kabla haijakuwepo hata moja.
 
17 Tazama jinsi yalivyo ya thamani mawazo yako kwangu, Ee Mungu!
Jinsi jumla yake ilivyo kubwa!
18 Kama ningezihesabu,
zingekuwa nyingi kuliko mchanga.
Niamkapo,
bado niko pamoja nawe.
 
19 Laiti ungewachinja waovu, Ee Mungu!
Ondokeni kwangu, ninyi wamwaga damu!
20 Wanazungumza juu yako wakiwa na kusudi baya,
adui zako wanatumia vibaya jina lako.
21 Ee Bwana, je, nisiwachukie wanaokuchukia?
Nisiwachukie sana wanaoinuka dhidi yako?
22 Sina kitu zaidi ya chuki dhidi yao,
ninawahesabu ni adui zangu.
 
23 Ee Mungu, nichunguze, uujue moyo wangu,
nijaribu na ujue mawazo yangu.
24 Uone kama kuna njia iletayo machukizo ndani yangu,
uniongoze katika njia ya milele.
* Zaburi 139:8 Vilindi ina maana ya Kuzimu, ambayo ni Sheol kwa Kiebrania.