Zaburi 20
Maombi Kwa Ajili Ya Ushindi
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.
Bwana na akujibu unapokuwa katika dhiki,
jina la Mungu wa Yakobo na liwe kinga yako.
Na akutumie msaada kutoka patakatifu
na akupatie msaada kutoka Sayuni.
Na azikumbuke dhabihu zako zote,
na azikubali sadaka zako za kuteketezwa.
Na akujalie haja ya moyo wako,
na aifanikishe mipango yako yote.
Tutashangilia kwa furaha utakaposhinda,
tutainua bendera zetu kwa jina la Mungu wetu.
Bwana na akupe haja zako zote.
 
Sasa nafahamu kuwa Bwana
humwokoa mpakwa mafuta wake,
humjibu kutoka mbingu yake takatifu
kwa nguvu za wokovu wa mkono wake wa kuume.
Wengine wanatumaini magari ya vita, na wengine farasi,
bali sisi tutalitumainia jina la Bwana, Mungu wetu.
Wao wameshushwa chini na kuanguka,
bali sisi tunainuka na kusimama imara.
 
Ee Bwana, mwokoe mfalme!
Tujibu tunapokuita!