Zaburi 29
Sauti Ya Bwana Wakati Wa Dhoruba
Zaburi ya Daudi.
1 Mpeni Bwana, enyi mashujaa,
mpeni Bwana utukufu na nguvu.
2 Mpeni Bwana utukufu unaostahili jina lake;
mwabuduni Bwana katika uzuri wa utakatifu wake.
3 Sauti ya Bwana iko juu ya maji;
Mungu wa utukufu hupiga radi,
Bwana hupiga radi juu ya maji makuu.
4 Sauti ya Bwana ina nguvu;
sauti ya Bwana ni tukufu.
5 Sauti ya Bwana huvunja mierezi;
Bwana huvunja vipande vipande
mierezi ya Lebanoni.
6 Hufanya Lebanoni irukaruke kama ndama,
Sirioni urukaruke kama mwana nyati.
7 Sauti ya Bwana hupiga kwa miali
ya umeme wa radi.
8 Sauti ya Bwana hutikisa jangwa;
Bwana hutikisa Jangwa la Kadeshi.
9 Sauti ya Bwana huzalisha ayala,
na huuacha msitu wazi.
Hekaluni mwake wote wasema,
“Utukufu!”
10 Bwana huketi akiwa ametawazwa juu ya gharika;
Bwana ametawazwa kuwa Mfalme milele.
11 Bwana huwapa watu wake nguvu;
Bwana huwabariki watu wake kwa kuwapa amani.